Showing posts with label Cheka. Show all posts
Showing posts with label Cheka. Show all posts

Saturday, July 25, 2015

Mambo ya kuzingatia kuhusu kucheka… Cheka panapostahili, kujichekesha sio dili!



Mchango wa Hadhi(Wadhifa) katika kucheka.
Katika nakala iliyopita kwenye mfululizo wa nakala hizi, tuliona jinsi uhusiano na hisia zilivyo na mchango katika kumfanya mtu acheke awapo na watu fulani. Tuliona kwamba mtu anacheka kirahisi awapo na familia yake ama kazini, yaani jinsi uimara wa uhusiano ulivyo au hisia zilizopo ndiyo urahisi wa mtu kucheka ulivyo.
Katika nakala hii tunageukia katika kitu kingine ambacho kina mchango mkubwa katika kumfanya mtu acheke. Wengi tumewahi kulishuhudia hili ingawa kuna uwezekano hatukuliwekea mkazo. Tumeona katika filamu nyingi, pale mkuu au bosi wa kikundi fulani anapotokewa na kitu cha kuchekesha ambacho kinaweza kuwa kikimuaibisha kwa namna moja au nyingine, wale wafuasi hucheka endapo tu mkuu wao ataanzisha au kuruhusu wao kucheka na punde atakaponyamaza, basi nao hufuata.
Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kauli moja, ‘Huhitaji kuwa mchekeshaji, ukishakuwa tajiri basi watu karibu yako hujikuta wakicheka tu hata ukiongea pumba.’ Hakuwa akikosea. Ukweli ni kwamba watu wawapo na watu wenye hadhi kubwa zaidi yao, hujikuta katika hali ya kucheka zaidi kuliko wakiwa na watu wa hadhi ya chini yao au hadhi sawa.
Umewahi kuona namna watu waliokaa meza moja katika baa wanavyocheka? Au kikundi cha watu wa ofisi moja wakicheka? Vicheko huongezeka na watu kuwa huru zaidi endapo mkuu au bosi yupo katika kundi hilo. Mchango wa mkuu au bosi huyo katika kuwafanya watu kucheka ni pale atakapotoa kichekesho ambacho anategemea watu wacheke au atakapoanzisha kucheka kichekesho cha mtu mwingine.
Pia hili tunaweza kuliona katika familia zetu na kama tunakumbuka kipindi tukiwa tunasoma. Kichekesho hicho hicho kikitolewa na kaka au dada nyumbani kitachekesha tofauti kama kitatolewa na mama au baba wa familia. Hivyo hivyo ndivyo ilivyo endapo mwalimu atajaribu kutoa kichekesho kwa wanafunzi wake. Hata kama kichekesho kitakuwa cha kawaida sana au hakichekeshi, bado wanafunzi watajikuta wakicheka.
La kuzingatia… Kucheka uwapo na mtu mwenye hadhi zaidi yako, ni jambo linalotakiwa kutokea bila ya kujifikiria. Kumbuka kucheka kunatokea pale tu mtu awapo na furaha, hivyo kuonesha una furaha kuwa pamoja na mtu huyo ni jambo la msingi. Huhitaji kujichekesha, lakini kuweka akilini kwamba mtu uliyekaa naye ana hadhi zaidi yako na hivyo anakutendea wema kukaa na wewe na kujaribu kukupa furaha kwa kukuchekesha, basi utajikuta ukivielewa vichekesho vyake na kucheka bila pingamizi. Pia, unaweza kutazama namna watu wa kundi moja wanavyocheka na kutambua mkuu katika kikundi hicho.
Katika nakala ijayo; Mchango wa matayarisho ya kucheka kabla ya kucheka…  

Thursday, July 23, 2015

Mambo ya kuzingatia kuhusu kucheka… Cheka panapostahili, kujichekesha sio dili!



Mchango wa Uhusiano na Hisia katika kucheka.
Nakubali kwamba kucheka ni jambo zuri lakini kucheka bila sababu za msingi ni kutokujielewa. Kuna mambo mengi yanayoingiliana na kupelekea mtu kucheka na vinapokosekana vingi vya vitu hivyo lakini bado mtu akaonekana akicheka, basi huyo atakuwa hajielewi na kuwa akijichekesha. Wengi wanadhani kwamba kucheka ni matokeo ya kueleweka kwa kichekesho na kutokufahamu kwamba kichekesho ni sehemu ndogo tu na inayokuja kwenye hatua za mwisho mwisho kati ya mambo ya msingi ya kusababisha kicheko.
Katika mfululizo wa nakala hizi, lengo ni kuainisha sababu za msingi za kicheko ili kuongeza ama kupunguza wastani wako wa kucheka. Usicheke kwa nadra wala usicheke daima, cheka kwa wastani. Msemo usemao kucheka kunaongeza siku za kuishi, usikufanye utake kucheka kila dakika na kuondoa maana halisi ya kicheko.
Jambo la msingi kama si lenye ushawishi mkubwa la kutambua kuhusu kucheka ni kwamba kucheka ni tendo linalohusisha sana hisia kabla ya kitu chochote. Hisia hupelekea kuwepo kwa uhusiano baina ya watu wasiojuana lakini pia ni matokeo ya uhusiano baina ya watu wa familia moja ama ndugu ama majirani, yaani watu waliolazimika kuwa pamoja na kujuana.
Ni rahisi na jambo la kawaida kucheka unapokuwa na mtu mwenye uhusiano naye hata kwa jambo ambalo kiukweli si kichekesho. Watu wengi hucheka zaidi wakiwa nyumbani, kisha kazini kuliko wawapo njiani au kwa watu wasiowajua. Wewe ni shahidi yangu katika hilo. Kama hutaki hilo, na hili je? ‘Katika kundi la watu wengi waliotawanyika, watu watakaokuwa wakicheka zaidi kwenye mazungumzo yao ni wale wenye uhusiano wa kimapenzi kuliko wenye uhusiano wa namna nyingine na mwisho ni kwa wale wasiojuana kabisa.’
Kumbuka kuwa hata kwa wachekeshaji, ni rahisi mtu kucheka kwa yule mchekeshaji ambaye amejiwekea hisia kuwa ni mchekeshaji mzuri kuliko kwa wale ambao bado hajajua uwezo wao wa kuchekesha(hana hisia zozote juu yao) au anaowajua kama wasio na uwezo wa kuchekesha(ana hisia mbaya juu yao). Yaani ni kwamba mtu hucheka kirahisi kwa mchekeshaji ambaye kuna uhusiano uliojificha kwamba huyu ni mchekeshaji na mimi ni mchekeshwaji wake.
La kuzingatia… Unaweza kutumia kicheko chako au cha mtu mwingine kwako(ipo zaidi kwenye nakala zangu za kuchekesha) kupima hali au maendeleo ya uhusiano wenu. Pia waweza kutumia kucheka ili kuongeza nguvu ya uhusiano wako na mtu mwingine (lakini epuka kujichekesha). Katika nakala zangu za kuchekesha, utaweza kujifunza namna ya kujijengea uwezo huo wa kucheka kwa watu unaotaka kuongeza uhusiano nao bila ya kujichekesha.
Katika nakala ijayo; mchango wa hadhi(wadhifa) katika kucheka.
  • Hadithi na Simulizi