Showing posts with label Chekesha. Show all posts
Showing posts with label Chekesha. Show all posts

Monday, September 7, 2015

Jinsi ya kusimulia vichekesho kwa namna itakayochekesha…



Katika nakala iliyopita katika mfululizo wa nakala hizi, nilizungumzia umuhimu wa kujua kuchekesha bila ya kukariri vichekesho. Lakini, inanipasa kuelezea namna ya kutumia vichekesho katika kuchekesha kwani ndiyo mwanzo wa kujijengea uwezo wa kuchekesha bila kufikiria. Kabla sijaanza kuelezea namna ya kutumia vichekesho ili kuchekesha, nikumbushe kuwa vichekesho kama mpangilio wa maneno pekee, vina mchango mdogo sana katika kuchekesha.
Kama umewahi kuona watu wakielezea jambo na kujikuta wakicheka wenyewe bila ya kukufanya wewe ucheke, jua watu hao walishindwa kuvitumia vichekesho hivyo kuchekesha. Pia, wapo wanaokujulisha kuwa wanatoa vichekesho ili kuchekesha lakini hata wanapomaliza kuelezea vichekesho hivyo, msikilizaji unashindwa kuona kitu cha kuchekesha. Sina shaka kwamba kila mtu ameshatokewa na hilo. Baadhi hujaribu kuelezea zaidi vichekesho vyao pale wanapomaliza na kushindwa kuchekesha lakini hata kwa maelezo ya mara ya pili, bado wapo ambao hufeli kutumia vichekesho hivyo kuchekesha.
Kitu cha kwanza kabisa cha kuzingatia, ni kujua nini hasa ndiyo chanzo cha maelezo fulani kuwa vichekesho. Lazima ujue nini kilichokufanya wewe uelewe kuwa maelezo fulani ni vichekesho na mengine si vichekesho. Pia kama nilivyoelezea katika nakala zilizopita katika mfululizo huu, lazima ujue ni hatua ipi kati ya zile hatua kuu tatu za kufanya mtu acheke ndipo vichekesho hivyo utakavyotumia vitamhakikishia mtu kuwa ni vichekesho.
Chanzo cha kuchekesha kwa vichekesho, mara nyingi huwa ni mhusika ndani ya kichekesho kuelewa tofauti jambo fulani mfano katika kichekesho kimoja, mteja wa kiume kufurahia kusikia atapewa kampani na sekretari wakati bosi akifanya shughuli nyingine lakini sekretari kumbe ni wa kiume na si wa kike au kichekesho kingine ni mchina kupewa jukumu la ‘supplies’ yaani mahitaji na badala yake yeye kuelewa kuwa jukumu lake ni kufanya ‘surprise’ yaani jambo zuri lisilotarajiwa..
Pia katika kutambua hatua gani hasa ndiyo mihimili ya vichekesho, mara nyingi huwa ni katika ule muda ambao mchekeshwaji anahusisha matokeo ya vichekesho yaani mwisho wa vichekesho na ile picha au mwisho ambao yeye aliutabiri, ni vema kuhakikisha kuwa usimuliaji wako wa vichekesho, hauingilii hatua hiyo kwa kujaribu kuchekesha kabla ya hiyo hatua.
Kwa kutambua chanzo, ni lazima umuwezeshe mlengwa kubaini chanzo kama ulivyoona wewe msimuliaji. Yaani kwa mifano ya hapo juu, lazima uhakikishe mlengwa anatambua kuwa kuna ‘supplies’ na ‘surprise’ zenye matamshi yanayoendana lakini maana tofauti na kama kuna sekretari wa kike na wa kiume kabla ya kufika kwa hatua uliyobaini kuwa ndipo kuchekesha kutatokea.
Wanachokosea wengi ni kudhani mlengwa ana uelewa kama aliokuwa nao yeye anayetoa vichekesho. Pia mazingira yanapokuwa tofauti, labda vichekesho wewe ulivisoma lakini sasa unasimulia, au wewe ulihusika katika vichekesho lakini sasa unamuelezea mtu ambaye atakuwa msikilizaji tu, na namna nyingine nyingi. Hivyo jambo kuu au mzizi wa yote ni kujiuliza mara mbili mbili, je mazingira na uelewa uliokuwa nao wakati ukivipata vichekesho hivyo, ndiyo mazingira na uelewa uliopo wakati unavitoa vichekesho hivyo? Mambo hayo yanapoendana, nina imani kuwa vichekesho vyako vitafanya kazi yake ya kuchekesha.
Katika nakala inayofuata katika mfululizo wa nakala hizi tutaangalia mambo ya kuepuka wakati wa kutoa vichekesho… mifano iliyoelezewa hapo juu imetolewa kwa kirefu katika facebook group, www.facebook.com/copykennytz

Thursday, August 13, 2015

Hatua za kufuata katika kuchekesha… Njia maridadi ya kutoa kichekesho

Kabla sijazungumzia hatua za kufuata katika kuchekesha, ningependa kugusia hatua ambazo mtu hufuata wakati wa kucheka. Si mara zote hatua hizi hufuatwa zote na si mara zote hatua hizi hufuatwa kimpangilio. Lakini, izingatiwe kwamba zaidi ya asilimia themanini wakati wa kucheka, hatua hizi hufuatwa.
Mara nyingi katika kucheka, huanza kwa matayarisho au utayari wa kucheka. Ni mara chache sana mtu hucheka bila ya kuwa ametayarishwa ingawa vichekesho visivyopitia mtu kutayarishwa ndivyo husababisha kuchekesha zaidi. Kwa kupitia utayari huo, kucheka kunaweza kutokea kwa namna mbili. Kwanza na mara nyingi ni pale mtu anapotayarishwa naye kujua tukio linalofuata linahusisha kucheka. Mfano, watu wengi hupenda kusema, “Ngoja, nikuchekeshe bwana…” au misemo inayoendana na huo. Mfano mwingine ni pale mtu anaposoma kichekesho kwenye simu yake na kuanza kucheka akijua unamuona. Kisha mtu huyo bila ya kupoteza muda, pengine bado akicheka anamuonesha kichekesho hicho mtu mwingine. Kwa namna hii, mtu anakuwa ametayarishwa kwa kucheka wazi wazi. Pili, ni pale mtu anapotayarishwa bila ya kuwa na uhakika kama kauli zitahusisha kuchekesha au hapana. Utayarishaji huu wa pili, ndio wenye nguvu zaidi katika kuchekesha. Mtu huhisi kitu fulani cha kuchekesha kwamba kitatokea bila ya kuwa na uhakika Kisha kitu hicho kinapokuwa kweli, ndipo mtu anajikuta katika hali ya kucheka.
Hatua ya pili katika kucheka ni kusikia au kuona ama kusoma kichekesho. Hapa mtu husikia kauli au mfuatano wa sentensi wenye lengo la kuchekesha. Sina haja ya kuelezea maana ya kichekesho au namna vichekesho vilivyo kwani naamini hata mtoto atakayezaliwa kesho anajua maana ya kichekesho.
Hatua ya tatu katika kucheka ni mtu kukihusisha kichekesho na sehemu ya ubongo wake itakayokitafakari kichekesho kile na kujenga uhusiano na picha fulani kichwani mwake. Mchekeshwaji hujaribu kutafuta uhusiano baina ya kichekesho na matukio yaliyowahi kutokea huko nyuma ama matukio aliyowahi kuyasikia na kuyajengea picha kichwani au kujenga picha fulani kichwani akitumia wahusika na mandhari anayoitambua vema. Yaani kujaribu kupata picha mtu anayemjua au mahali anapopajua panatokea kilichoelezwa kwenye kichekesho hicho.
Hatua ya mwisho katika kucheka, yaani kucheka kwenyewe kunategemea sana na hatua ya nyuma yake. Kama mtu ataweza kujenga picha fulani au kukumbuka picha fulani inayoendana na kichekesho kwa kutumia wahusika na mandhari aijuayo vema, basi mtu huyu lazima atacheka.

Hatua za kufuata katika kuchekesha…
Baada ya kuelewa hatua zinazofuatwa mara nyingi katika kucheka, ni vema kuzingatia hatua hizo katika kuchekesha pia. Yaani ili kujihakikishia kwamba kichekesho chako hakipotei bure, ni vizuri kama utafuata hatua za kucheka ili kuchekesha.
Katika kumtayarisha mtu kwa kucheka, ni busara kuanza kufanyia mazoezi kumtayarisha mtu bila kumuweka wazi kwamba una nia ya kuchekesha. Baadhi ya watu husema kwamba Tanzania hatuna watu wenye uwezo wa kuchekesha lakini nikitathmini, naona kwamba kinachokosekana ni utayari wa watu kucheka na pengine ni kufeli katika kuwatayarisha watu kucheka. Njia nzuri ya kutayarisha watu kucheka ni kuruka hatua ya kutoa kichekesho na kumpa mlengwa muda wa kutengeneza picha kuhusu maelezo. Yaani kumfanya mtu aende hatua ya tatu hapo juu kabla ya kupita ya pili na kisha kuendelea na kichekesho. Ndiyo, wachekeshaji wengi hasa wale wafanyao ana kwa ana mbele za watu, hutumia njia hiyo ya kutayarisha.
Umewahi kusikia mtu akiuliza, “Niseme nisiseme?” na baada ya hapo kauli inayofuata inavunja watu mbavu? Hapo, mtu hufanya watu kujenga picha mbali mbali na kwa namna moja ama nyingine kuweka uwezekano wa kutokea kichekesho. Hivi karibuni, niliona njia hiyo ikitumiwa na Mhe. Mbowe akitoa hotuba baada ya Mhe. Lowassa kuchukua kadi. Baada ya kuongea mengi, alisema
“Katika ujio huu, kuna mtu mmoja ningependa kumshukuru sana.” Akakaa kimya na kuuliza, “Niseme nisiseme?” Bila shaka alijua alichokuwa akikifanya kwani baada ya kuambiwa aseme(jambo lililokuwa halihitaji kuuliza), Mhe. Mbowe akasema anamshukuru Mhe. Rais na kuweza kuangusha vicheko kwa wanaukawa.
Ukimaliza kumtayarisha mlengwa kwa kucheka, kinachofuata ni kutoa kichekesho kwa namna inayotoa muda mtu kuhusisha kichekesho na ile picha aliyoijenga kichwani. Yaani usikimbilie kusema kichekesho chako mwanzo mpaka mwisho bila kuwa na vituo vya kumpa mtu muda wa kubashiri mwisho wa maelezo yako kabla hujamaliza.
Kimsingi hizo ndizo hatua za kufuata katika kuchekesha. Si nyingi lakini umakini na mazoezi vinahitajika kabla ya vitu uwezo huo wa kuchekesha kukaa kwenye damu.
Katika nakala ijayo, tutaangalia namna ya kuvitumia vichekesho ulivyoviona kwa ajili ya kuchekesha. Hii ni changamoto kwa wengi lakini uvumbuzi unakuja hapa.


Wednesday, August 12, 2015

Umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho…



Kuchekesha bila kukariri vichekesho haimaanishi kuwa na uwezo wa kutunga vichekesho vipya au kuvibadilisha vichekesho vilivyopo. Ninachojaribu kumaanisha kwa umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho ni sababu za kuchekesha bila ya kutumia vichekesho(kifungu cha kauli zenye lengo la kuchekesha.)
Miaka mingi iliyopita, nikiwa mtu ninayejali mambo ya muhimu peke yake, sikuona umuhimu wa kuchekesha wala kucheka vichekesho vya watu. Sisemi maisha yalikuwa mabaya au magumu lakini hali ya sasa ni nzuri zaidi kuliko huko nyuma. Muda ulivyokuwa ukienda mbele nilianza kuona umuhimu wa kujua kuchekesha, acha ile mara moja mara mbili ambayo mtu yeyote anaweza kuchekesha. Nilitamani kuwa na uwezo wa kuchekesha kwa haraka zaidi na mazingira magumu zaidi. Unajua nilichokifanya?
Nilianza kutembelea mitandao mbali mbali inayoandika vichekesho na kuanza kuvikariri vichekesho hivyo. Ingawa vichekesho hivyo vilikuwa kwa lugha ya kiingereza, niliweza kuvibadilisha na kuvisimulia kwa Kiswahili kwa namna ambayo ilichekesha. Kadiri siku zilivyokwenda nami nikawa nikitafuta vichekesho hivyo kwa udi na uvumba ili wale waliouona uwezo wangu wa kuchekesha wasiache kunisikia nikichekesha. Halikuwa jambo baya lakini vichekesho hivyo vikawa kama vikijirudia rudia na kuniboa. Hapo ndipo nikaona umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho.
Umuhimu hasa ni kuwa na uwezo wa kuchekesha muda wote na mahali popote. Lakini bado kuna haja ya kuzungumzia umuhimu wa kuchekesha kwa ujumla wake. Katika hali ya kawaida, faida kubwa ya kuchekesha ni kujenga na/au kuimarisha mahusiano baina ya watu. Ipo wazi kwamba watu wanaochekesha huwa na mahusiano na watu wengi zaidi kuliko wale wasiochekesha lakini ikumbukwe pia kuwa kuchekesha kila wakati huweza kufanya watu wakutoe maana, yaani uonekane mtu asiyeweza kuwa makini. Kama ni mfanyakazi, kumchekesha bosi wako kutaimarisha uhusiano wako na bosi huyo na unajuaje faida ya kuwa karibu zaidi na bosi wako kuliko wafanyakazi wengine?
Umuhimu mwingine wa kuchekesha ni kutumiwa kama ajira. Mifano hai ipo kwa wale wenye vipindi vya kuchekesha na kila stesheni, ina vipindi hivyo. Naomba nisihi kwamba kuchekesha siyo tu kutakupatia ajira ya kuchekesha, bali ajira nyingi zinazohusisha kuhudumia watu wengi basi kuchekesha kwako, kutakuongezea uwezekano wa wewe kupata ajira. Kwani hujawahi kusikia watu wakati wakitafuta mwongozaji wa sherehe wakisema, “Wee? Kuna MC huyo anaitwa Kafupi, yaani balaa kwa kuchekesha. Tumchukue huyo huyo.” Pia hujakutana na wagonjwa wanaompendelea daktari fulani kwa sababu anaongea nao vizuri? Anawachekesha?
Nimeanza na hali ya kawaida, nikafuata yenye umuhimu kidogo na sasa nizungumzie umuhimu wa kuchekesha katika hali ambayo watu wengi hushindwa kufikiria umuhimu wa kuchekesha katika mazingira hayo. Hapa ndipo hasa penye umuhimu wa kuchekesha bila ya kukariri vichekesho. Nazungumzia kuchekesha kama njia ya kukwepa hali tata upande wako. Inaweza kuwa kukwepa swali gumu kwenye mahojiano, kuinua au kubadili mkondo wa ushindi kwenye majibizano na hata kuficha ubaya unaotaka kujitokeza.
Pata picha unakwenda kwenye masaili(mahojiano) ya kazi na umeme umekatika siku hiyo. Ukaenda na shati lililojikunja sana ukiiamini elimu na ujuzi wako kuliko umaridadi wako lakini kati kati ya intavyu, mmoja wa wanaokuhoji akakuuliza, “Kwa nini umevaa shati lililojikunja sana wakati unajua unakwenda kwenye intavyu?”
Katika hali ya kawaida mtu anaweza kujaribu kutoa sababu nyingi, ‘umeme umekatika, nimeibiwa shati langu nililotayarisha, nje tu ya ofisi nimemwagiwa juisi hivyo hili siyo langu.. n.k) ambazo zinaweza kuzua maswali mengine na mwisho wa siku kuonekana mtu ambaye hukujiandaa mapema au kwa kiingereza naomba niseme, ‘careless.’(keyales). Kwa mimi ningejibu au ningeshauri mtu yeyote ili kuondoa umakini wa wale wanaokuuliza katika jambo hilo kwa namna inayofanana na jibu hili.
“Ooh, huu ni utamaduni kwetu. Bibi yangu mzaa babu aliniambia nikitaka kufanikiwa kwenye intavyu kama hizi, nisipige pasi nguo.” Kama bahati mbaya kuna mdudu kwenye nguo na umeulizwa, unaweza sema, “Ooh, kuna mtu ananitakia kila la kheri kutoka kijijini kwetu.”

Kuna kipindi nilikuwa katika masaili ya kupewa ufadhili wa masomo nao ungetegemea uwezo wangu wa kufaulu. Matokeo yangu ya mtihani wa Taifa yalikuwa mazuri lakini mfadhili hakuamini mara moja na katika kutokuamini kwake akauliza, “Lakini nasikia shuleni kwenu wasimamizi wa necta huwa wanalipwa.”
Nadhani unaweza kujua kwamba kukataa kungeleta maswali zaidi na kukubali kungeashiria nisiaminiwe kwa matokeo tu ya necta. Bila ya kutetereka nilimjibu,
“Yah, ofkoz huwa wanalipwa.” Nikavuta muda kidogo na kumalizia, “Na Necta (yaani baraza la mitihani) lakini.” Wote katika chumba walicheka na kutohoji tena kuhusu maswala hayo.
Sasa tumeona umuhimu wa kujua kuchekesha bila ya kukariri vichekesho, katika nakala ijayo tutaona hatua zinazofuatwa katika kucheka na hivyo hatua za kufuata katika kuchekesha…
  • Hadithi na Simulizi