Showing posts with label Staarabika na Staarabisha. Show all posts
Showing posts with label Staarabika na Staarabisha. Show all posts

Saturday, September 19, 2015

Jinsi ya kuipokea pole na kumfurahisha mtoaji pole...



Watu wengi katika taifa hili wamejiwekea mazoea hasi kwa jinsi yao ya kupokea pole. Wengine wamekwenda mbali zaidi kiasi cha kwamba kudhania kuwa wakiwa na matatizo, mtu wa karibu yao ni lazima atoe pole. Yaani wanachukulia kuambiwa pole ni haki yao na hivyo kukosa ustaarabu wa kuonesha kuheshimu huruma ya mtu atoaye pole.
Ukimuuliza mtu yoyote, ukiambiwa pole utajibu nini? Jibu lake bila shaka litakuwa ni ‘asante’. Jambo la kujiuliza ni kwamba, unaposema ‘asante’ baada ya kuambiwa pole, una uhakika ina utofauti na ile ya mtu akikuambia ‘hongera’? Katika hatua za kuboresha lugha yako ya kistaarabu, hasa kwa jinsi ya kuipokea pole, huo ndiyo mwanzo. Yaani hakikisha namna unavyoipokea pole kwa kusema ‘asante’ iwe tofauti na kama mtu angekuambia ‘hongera’ baada ya kufanikiwa jambo.
Katika kuimarika kwa lugha yako kwa jinsi ya kuipokea pole, basi ni vema uzingatie taratibu zile za kutoa pole katika nakala hizi. Yaani usitoe ‘asante’ tupu. Jambo unaloweza kuzingatia ili kufanikisha jitihada za kutotoa ‘asante’ tupu ni kugundua kuwa mpaka mtu anakuambia pole, basi ameguswa kwa namna fulani na matatizo yako. Asante yako ni vema ukailenga kwa namna mtu alivyoguswa na matatizo yako. Faida za kufanya hivi ni kumfanya mtu aliyetoa pole kuona kuwa umethamini mchango wake au hisia zake katika matatizo yako na kukufikiria kama mtu atayeweza kuthamini na kusaidia katika matatizo yake.
Katika hatua za mwanzo za kutotoa ‘asante’ tupu, unaweza kujifunza kutumia maneno, ‘asante au nashukuru kwa kuguswa.’ Hapo unamfanya mtu atoaye pole aamini kuwa hakufanya vile kana kwamba ni desturi bali moyo wake umekuwa wa kikarimu na kuweza kugundua au kuguswa na matatizo yako. Yaani si watu wote watakaotoa pole kwako, bali wachache kama yeye.
Zaidi ya kauli hiyo, ‘asante au nashukuru kwa kuguswa’, katika jinsi ya kuipokea pole unaweza kuivalisha ‘asante’ yako mavazi mazuri zaidi au ya kiufalme. Hapo ndipo unapoweza kupeleka mahusiano(urafiki) katika hatua nyingine au kufufua au kuimarisha uhusiano au urafiki. Hatua hii ya kuvalisha mavazi, si ya kuikimbilia kwa haraka kwani unapokosea, inaweza kuleta picha tofauti zaidi. Katika hatua za mwanzo, unaweza kutumia kauli zinazoendana na namna hii, ‘Nashukuru kwa kunifariji. Kiukweli unaelezea hali mbaya uliyokuwa nayo mwanzo na kisha kuelezea hali mpya iliyo bora baada ya kupokea pole’ au kauli ndogo kama ‘sikudhania kama jambo hili lingekugusa. Lakini nashukuru kwamba na wewe umeona jinsi gani linavyonisumbua…’
Nimalizie na kuvisha mavazi ya kiufalme ‘pole’ itokayo kwa mtu unayemjali sana, au mtu aliyetoa ‘pole’ ambayo maneno yake yalifanya usahau shida uliyo nayo, kwa jinsi hii ya kuipokea ‘pole’, ni vema kuitumia mara chache iwezekanavyo. Jinsi hii inakuwa na maelezo mengi ambayo yanazungumzia sifa za ujumla, labda baada ya mtu kuguswa mara nyingi na matatizo yako au kuonesha msaada mkubwa katika matatizo yako. Maelezo haya nahisi yashatumiwa mara nyingi na hivyo swala la kuyaainisha. Unaweza kusema kitu kinachoendana na ‘Nashukuru kwa kuguswa, tena nashukuru sana. Yaani katika watu wangu wa karibu, wewe…’
La kuzingatia: Hata uwe na matatizo kiasi gani, kupewa pole si haki yako. Hivyo ukipewa ‘pole’, shukuru. Ukiwa unapokea pole, jitahidi kujua nini kimemgusa mtu huyo hata kutoa pole na shukuru kufuatia kuguswa huko. Mfano katika msiba, mtu anaweza kuguswa kwa namna kifo kilivyotokea, au familia anayoiacha marehemu, au maisha aliyoishia marehemu(labda muda mfupi) n.k. lakini kwa namna yoyote ile, wataunganishwa na neon ‘pole’. Kazi yako ni kugundua kipi kimemgusa hasa. ‘Pole’ ya kipekee ni vema ikapokea shukrani ya kipekee, na ni vema kukumbuka ‘pole’ siyo ‘mchango wa kutatua matatizo’ ni kuguswa na kutoa kauli za kufariji.
Katika nakala ijayo katika mfululizo wa nakala hizi, jinsi ya kuomba radhi.

Friday, August 14, 2015

Kusema pole siyo kazi, kazi kutoa pole… Jinsi ya kutoa pole kistaarabu.



Watanzania ni wakarimu sana, kila mtu analisifia hilo. Ni jambo la ukweli na la kupewa sifa. Hata mtoto mdogo wa kitanzania anatambua ya kuwa jambo lolote linaloonesha kuwa la kutokufurahisha linapomtokea mtu, basi jambo zuri na la kwanza kabla ya yote ni kumpatia pole mtu aliyefikwa na janga hilo. Matokeo yake ni kwamba tumekuwa kama mashine, yaani ukiona mtu anasikitika basi wewe ni … ‘pole…’ na imepita hiyo.
Sisemi tuache kusema pole kwani vipo vingi vya kurekebisha na inategemea na mtu. Wapo baadhi ya watu ambao kiukweli hupenda kusikia wakiambiwa pole na hivyo kusema pole kwao, hufanya kazi bila matatizo. Lakini linapotokea tatizo kubwa kama ugonjwa au msiba, basi lazima kuwa makini katika kutoa pole. Mfano tuchukulie swala la msiba, mtu wa kwanza kasema pole akaeleweka. Akaenda wa pili naye akaeleweka. Wa tatu, nne na kuendelea. Wewe unasikia kutoka kwa mtu na kwenda kutoa pole kama ya ishirini hivi. Je, unadhani kufika pale na kusema maneno yale yale, “Nasikia umefiwa na [ndugu] yako. Dah, jamani hivi ameondoka kweli, pole sana.” Kutamfanya mfiwa akumbuke kwamba uliguswa? Au unajisikiaje unaporudi kutoka kwenye mazishi mkoani halafu unamwambia mtu kuwa ulikwenda kuzika, halafu unachosikia ni, “Pole ndugu yangu.”? Ongeza thamani ya utu wako kwa kutoa pole kistaarabu.
Mtu aliyestaarabika, hudadisi tatizo na ukubwa wake kabla ya kutoa pole. Pole ya kistaarabu pia huambatana na maneno ya kuisindikiza yaani huvalishwa nguo. Lakini pia katika hali ya kawaida, inaweza kukulazimu kutoa pole zaidi ya moja kama mtu apokeaye pole hiyo atakuwa akisimulia mfuatano wa matatizo au matukio yanayokulazimu kumuonea huruma. La kukumbuka ni kwamba, hata ukitoa pole mia kwa mtu mmoja katika muda mmoja, ni vema pole hizo zikawa zikitofautiana usemaji au utolewaji wake.
Ushauri wangu: Jifunze kutumia kauli ya, “Pole kwa …” ukimalizia na jambo linalokufanya umuonee huruma huyo mtu. Kisha, jifunze kutokukimbilia kusema pole kwani muda mwingi inamkatisha tamaa yule anayekusimulia majanga yake. Kwa kujifunza taratibu unaweza kugundua ni muda upi muafaka wa kutoa pole wakati mtu akikusimulia matatizo yake. Lakini kama unayajua matatizo kabla ya kuambiwa na huyo mtu, pengine umesikia kutoka kwa watu, ni vema kuanza na ‘Pole kwa…’ kisha kuanza kudadisi ukubwa wa tatizo na kama suluhisho limepatikana au la. Lakini katika yote, usisahau kutoa pole mara ujuapo ukubwa wa tatizo hata kama suluhisho limeshapatikana.
Katika nakala ijayo katika mfululizo wa nakala hizi za Lugha ya Maneno tutaangalia Namna ya kupokea pole kwani Kusikia ukiambiwa pole siyo kazi, kazi kuipokea pole unayopewa.

Saturday, July 18, 2015

Lugha ya Maneno

Habari tena wasomaji na watembeleaji wa blogu hii...
Kipengele hiki kinalenga kumpa mtu uwezo wa kuitumia lugha vizuri ikiwa ni kufikisha ujumbe aukusudiao vizuri na pia kuelewa bara bara nini mwingine anachomfikishia. Blogu hii inaamini kwamba utumiaji mzuri wa maneno utaleta mtazamo tofauti wa kimaisha kwa mtu binafsi kama au unaokaribiana na ule utokanao na uwezo wa mtu kuielewa vizuri lugha ya mwili (body language). Kipengele hiki kitachukua muda zaidi na ni ushauri wa blogu hii kwa watu kuwa wajaribu kusoma na kuyaelewa yote katika kipengele hiki wakiuliza maswali penye utata nao wataona utofauti.
  • Hadithi na Simulizi