Showing posts with label Za kutisha. Show all posts
Showing posts with label Za kutisha. Show all posts

Wednesday, September 30, 2015

Damu Ya Ukoo Wangu: Sehemu ya 6



" Nashukuru tu Mungu mke wangu umenizalia kidume atakayeweza kuendeleza jina langu. Ni mtoto mzuri tu ambaye hatuna budi kumpokea kwa mikono minne, mi miwili na wewe miwili. Wewe umemuonaje?"
"Mimi nimemuona tofauti mume wangu."
Alisimama akisubiri nimuulize kwa nini jambo ambalo sikuligundua mapema na hivyo muda kupita kabla ya kumuuliza kwa nini na ndipo akanijibu,
"Samahani sana mume wangu nimekuzalia mtoto mlemavu. Inaniuma sana kushindwa kukuzalia mtoto kamilifu kama ulivyokuwa ukisubiria miaka yote tangu tulipooana."
"Mke wangu,.."
Niliita nikitaka kumkatisha kwani niliona si busara kumfanya ajione mwenye makosa mbele ya mipango ya Mungu. Tatizo langu lingejitokeza mbele nami nilikuwa nikiamini lenyewe haikuwa mipango ya Mungu bali ni shetani aliyelileta. Mke wangu baada ya kuona nataka kumkatisha, ndipo sauti yake ikaongezeka uchungu na kuendelea,
"Mume wangu najua jambo hilo limekuvunja sana moyo lakini tafadhali nipo chini ya miguu yako, naomba usimchukie mwanangu kwa kuwa ni kilema, mimi unaweza kunichukia lakini mwanangu hana makosa."
Hapo niligeuka na kulala kiubavu nikimtazama mke wangu kwa huruma. Nikaunyoosha mkono wangu kushika nywele zake nikizishika taratibu na kwa kujiamini nikamwambia,
"Siwezi kumchukia kwa vile ni kilema mke wangu, nakuhakikishia hilo. Wewe ondoa shaka kabisa kwenye jambo hilo."
"Ahsante mume wangu."
Sikusema kitu baada ya shukrani yake nami nikawa nikiwaza jinsi gani mke wangu alikuwa akijaribu kunifanya nimpende mtoto yule ambapo kiukweli nilishapoteza hamu ya kumpenda nikijua hakuwa mwanangu. Nililala tena chali na kuacha kumshika nywele. Baada ya kama dakika tano kupita bila ya kusemekana neno, mke wangu akaita,
"Mume wangu"
"Naam mke wangu"
Niliitika huku nikigeukia tena upande wake. Naye akaweka mkono wake shavuni kwangu na kuuliza,
"Mume wangu hivi kipi kilikukasirisha kule hospitali hadi ukaondoka?"
"Kwa nini unauliza mke wangu, sikukasirika kitu."
"Usinifiche mume wangu. Unajua namna ninavyokupenda mpenzi, nisingependa kukufanya ukasirike hata mara moja mume wangu. Niambie tu kama ni kwa sababu ya ukilema sema tu, mimi mbona ni muelewa."
"Aahsh"
Nilitoa pumzi kwanza kama vile mtu aliyeshangazwa na kuchoshwa sana na kisha nikamuambia,
"Mke wangu naomba uachane na hayo. Cha msingi ni kwamba sina hasira tena na haikuwa kwa vile mtoto ni kilema kwani kama ni ukilema basi bado ningekuwa na hasira maana ukilema haujatoka lakini ona ninavyofurahi mke wangu."
"Huniamini mume wangu. Hudhani kama naweza kukabiliana na kueleza ukweli ndiyo maana unanikwepa na kujaribu kupata ukweli kwa njia zingine."
"Ukweli upi?"
Nilishajua alichokuwa akiongelea ila kwa vile niliona ameanzisha mwenyewe, hivyo ni bora angemaliza mwenyewe.
"Najua unajiuliza kama kweli huyu mtoto ni wako au wa shemeji kwa vile amefanana zaidi na shemeji kuliko wewe."
"Si mimi tu, kila mtu atakayemuona atajiuliza hivyo hivyo kasoro nyie wawili tu."
"Shemeji hahusiki kabisa na mtoto huyu mume wangu, naomba uniamini. Nimekuwa mwaminifu kwako siku zote na hakuna mahusiano yoyote kati yangu na shemeji. Namuheshimu naye ananiheshimu sana. Huyu ni mtoto wetu mume wangu."
"Usijaribu kunishawishi mke wangu, kama ni kweli nitajua tu. Nisiijue damu yangu?"
"Haya usiku mwema lakini kumbuka huyu ni mwanao."
Nikiwa nimelala usiku wa manane, nilijigeuza mwili wangu nami nikahisi mkono wangu ukitua juu ya kitu fulani kigumu ambacho hakikuwa cha kawaida. Ubaridi nilioupata ulifanya macho yangu yafunguke ghafla na kuona vivuli viwili vya watu wakiwa wanamvuta mwanangu huku mke wangu akijitahidi kumzuia mtoto na kuniita kwa kelele. Kuitwa huko nilihisi tu kutokana na namna mke wangu alivyokuwa akitanua mdomo lakini haikutoka sauti yoyote. Watu hao tayari walishafika karibu na mlango wa chumbani naye mke wangu akiwa kama hatua mbili kutoka kitandani.
Niliamka kwa haraka lakini kabla sijafanikiwa kusimama, nikahisi mkono wangu ukivutwa kunizuia nisiende kumsaidia mke wangu. Niligeuka kwa hasira kuangalia nani aliyekuwa akinishika. Hapakuwa na mtu na si kwa sababu ya kuwa na giza bali kweli hapakuwa na mtu kwa maana hata kuona kivuli chake haikuwezekana.
Niliogopa sana na kujaribu kuuvuta mkono wangu kuhakikisha kama kweli nilikuwa nimevutwa na mtu asiyeonekana au ni mawazo yangu tu. Nilijaribu kuuvuta mkono wangu nami nikagundua kuwa kweli ulikuwa umeshikiliwa na mkono wa huyo mtu asiyeonekana, mikono iiyokomaa na ya baridi kama imewekwa kwenye jokofu. Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kwani mke wangu alionekana kushindwa kuwazuia wale watu naye alikuwa akinitegemea mimi. Kwa namna alivyokuwa akiniangalia, alionesha kutokufurahishwa na kitendo cha mimi kutokwenda akishindwa kujua nilikuwa nimezuiliwa. Nilianza kuhisi moyo ukiniuma kwa hofu kuwa mke wangu angedhani nimefanya makusudi.
Ghafla nikasikia sauti ikininong'oneza,
"Usiende kumsaidia mkeo. Mnajitilia mikosi na huyo mtoto, siyo halali yenu huyo. Waachieni waende naye."

[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]

Saturday, September 5, 2015

Damu ya Ukoo Wangu: Sehemu ya 5

Bia pamoja na mziki wa taratibu uliokuwa ukipigwa kwenye baa hiyo vilinisaidia kupoteza muda na mawazo lakini kabla ya kufikia hali ya kutokujitambua, nilipata wazo la kwenda kuwafukuza wote wawili pale nyumbani. Niliondoka kwenye baa hiyo nikijiongelea na kujisikitikia mwenyewe hadi nilipofika nyumbani. Niliwakuta Shukuru na Lilian wakiwa wameshawasili pamoja na yule mdogo wake mke wangu, Jeni. Pia palikuwa na ndugu zake wengine  mke wangu pamoja na baadhi ya majirani na kufanya sebule ionekane haitoshi. Idadi kubwa ya wageni pale nyumbani ilinifanya niigize kana kwamba hakukuwa na tatizo kwani niliamini hakukuwa na mtu mwingine aliyegundua kwa sababu walimuona mtoto kwa mbali tu tena wale wachache waliolazimisha kumchungulia chumbani alikolazwa yule mtoto.
Nilipokea hongera zote nilizokuwa nikipewa na wageni nami pamoja na mke wangu tulikuwa tukiungana nao kumshukuru Mungu kwa kutujalia kupata mtoto lakini moyoni mwangu nilikuwa nikitafuta muda wa kuweza kuyamaliza matatizo yangu. Wakati wageni wakiendelea kufika mmoja mmoja, mdogo wangu aliniita kwa upole tuweze kutoka nje. Nikijua alichotaka kunieleza  na kwa vile nilikuwa nikiutaka mwanya huo, nilimfuata kwa haraka nasi tukaenda mpaka chumbani kwake.
"Kaka, inabidi tu kumshukuru Mungu kwa yote anayokujalia. Kwanza mkeo kushika mimba muda wote hata akajifungua salama ni jambo la kushukuru sana maana si wote wanaofanikiwa kufikia hapo. Najua kibinadamu hakuna aliyetegemea ulemavu lakini yote hiyo ni mipango ya Mungu, hakunala kufanya zaidi tu ya kumshukuru yeye."
Sikuamini kama wazo kubwa la mdogo wangu halikuwa kwenye kufanana sura na mwanangu bali ulemavu wake. Baada ya kumaliza kauli yake, sikuwa na hamu ya kujibu chochote nami niliishia tu kumtazama usoni nikishindwa kummaliza hadi aliponiuliza,
"Vipi kwani kaka, mbona hivyo?"
"Umemuona sura yule mtoto?"
Kwa mshangao mkubwa, akanijibu
"Ndiyo, kwani ina kasoro? Afu amekuchukua sura yako kabisa akaiacha ya mama yake."
Ilipita kama dakika moja nikiitafakari kauli yake kichwani huku sehemu zingine za mwili zikikusanya nguvu na baada ya kukusanya nguvu za kutosha, nilijikuta nikisimama na kumvamia mdogo wangu huku nikimkunja shingoni na kwa hasira nikafoka,
"Umewezaje kunisaliti Shukuru? Yani umesema unakaa kwa shughuli zako kumbe nia yako ni kutembea na mke wangu? Umewe..."
"Kaka, mimi nimetembea na mke wako?"
"Unaniuliza mimi! Mtoto amewaumbua huyu."
"Mungu wangu, yaani Baraka umefikia kunifikiria hivyo mimi? Mimi siwezi ..."
Ilimbidi asimame maana kulikuwa na hodi mlangoni kwake na alipofungua ndugu mmoja wa mke wangu alitutaarifu kuwa chai ilikuwa ipo tayari. Baada tu ya kuurudishia mlango, Shukuru akaniambia,
"Siwezi nikatembea na mke wako Baraka. Kama unaona sura inafanana zaidi na mimi ni upofu wako tu maana hata mimi na wewe tunafanana."
Sikutaka kuendeleza mazungumzo yaliyokuwa hayana dalili za kufikia mwisho na kwa vile nilitaka niende kazini, nikaenda hadi mlangoni alipokuwa amesimama na huku nikitazamana naye usoni nikamwambia,
"Ukweli nitaujua tu Shukuru na niamini mimi, utajuta milele ikiwa kweli."
Nilipoingia ndani ya nyumba yetu nilikwenda kwenye chumba cha kulia chakula na kupata kifungua kinywa. Kwa vile mke wangu alikuwa akiongea na wageni, sikutaka kumtoa kwenye mazungumzo lakini nilipoingia chumbani kujiandaa kwenda kazini, mke wangu naye aliingia na swali lake la kwanza likawa,
"Mbona hivyo mume wangu? Tumekwenda wote hospitali lakini kurudi ukatukimbia. Kweli yani shemeji yeye ndiyo wa kunirudisha..."
Alishindwa kuendelea baada ya uchungu kumjaa na kumfanya atoe chozi. Huruma iliniingia ghafla na hasa sikutaka wageni wahisi kama kuna kitu hakipo sawa. Hivyo nikakaa pembeni yake kitandani na kumkumbatia nikimwambia,
"Samahani mke wangu, sikupenda kufanya hivyo na nashindwa kuelewa kwa nini niliwahi kuondoka hospitali. Tafadhali naomba usinifikirie vibaya kabisa. Nakupenda sana mke wangu na sasa tumeanzisha familia yenye watoto, naomba tuwe watu wa furaha kwa yote yale Mungu anayotujalia."
Mke wangu aliniangalia shingo upande huku akitia huruma. Nikiwa na hofu kama ameweza kugundua uwongo ndani yangu, nikaamua kumuaga,
"Mke wangu, acha mimi niende kazini sasa. Hongera kwa kujifungua salama, naomba uniangalizie mtoto wangu."
Kabla ya kuanza kuondoka nikambusu kwenye paji la uso na ndipo taratibu nikauelekea mlango huku moyoni nikijalaumu kwa uwongo wote niliousema kwake na kisha kwenda kazini.
Siku iliendelea kwa namna hiyo, kazini nikipokea hongera nyingi kutoka kwa wenzangu na simu nyingi za pongezi kutoka kwa watu mbalimbali ambapo kila pongezi niliyokuwa nikiipokea, moyoni nilikuwa nikijiuliza watu hao wangesemaje endapo wangeelewa yaliyotokea. Maswali hayo yalinitia hasira kwani niliamini watu hao wangeniona mimi mjinga na si kunionea huruma endapo wangeujua ukweli.
Usiku ulipofika nikiwa chumbani na mke wangu tayari kwa kulala, ndipo mke wangu akaanzisha tena mazungumzo juu ya yule mtoto.
"Mume wangu, hatukupata muda wa kuzungumza kuhusu mtoto wetu. Niambie umemuonaje?"
Nilitamani niuone uso wa mke wangu vizuri jinsi anavyoongea lakini kwa vile taa zilikuwa zimezimwa, giza likaninyima uwezo huo. Nikiwa bado njia panda kama huo ndiyo ulikuwa muda muafaka wa kumuelezea mke wangu wasiwasi wangu au la, nikatoa jibu lisilofungamana na upande wowote.
" Nashukuru tu Mungu mke wangu umenizalia kidume atakayeweza kuendeleza jina langu. Ni mtoto mzuri tu ambaye hatuna budi kumpokea kwa mikono minne, mi miwili na wewe miwili. Wewe umemuonaje?"
"Mimi nimemuona tofauti mume wangu.”

[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]

Thursday, August 13, 2015

Damu Ya Ukoo Wangu: Sehemu Ya 4

Ilikuwa  alfajiri majira ya saa kumi na moja nikiwa bado nimelala fofofo, huku kaubaridi cha usiku kakiwa kameanza kupotea katika eneo tulilokuwa tukiishi lenye nyumba nyingi za karibu karibu, na ndege wasiopendwa na wengi aina ya kunguru wakianza kupiga kelele zao za kuamshana nilisikia kilio cha uchungu kutoka kwa mke wangu aitwaye Lilian, mtoto wa kingoni kutoka Songea. Niliamka kwa haraka na kwenda kuwasha taa. Baada ya kufikicha macho yangu nikaweza kuona jinsi mke wangu alivyokuwa akitaabika na huku matone ya damu yakiichafua shuka.
Nikatoka nje ya chumba chetu na kwenda kwa mdogo wangu aitwaye Shukuru aliyekuwa akiishi chumba cha nje cha nyumba yetu na kumgongea mlango kwa nguvu. Alipofungua mlango bila hata ya kuuliza nani aliyekuwa akigonga, moja kati ya vitendo vya kijasiri alivyokuwa akifanya Shukuru, nilimueleza kuwa wakati ulikuwa umewadia kwa mke wangu. Baada tu ya kumwambia habari hizo akaniambia nirudi kwa mke wangu tujiandae wakati yeye akifanya mipango ya kupata teksi.
Nilirudi kwa mke wangu kwa haraka na kumuomba ajitahidi kuvumilia wakati teksi ikija kwani hatukuwa mbali na barabarani na eneo hilo lilikuwa likiwahi kukicha kuliko sehemu nyingi zingine za Dar es Salaam. Huku nikimpa maneno ya kumtia nguvu mke wangu, nilimsaidia kunawa uso na wote kuvaa nguo za kiheshima. Hazikupita dakika tano nikasikia honi ikipigwa karibu na nyumba yetu eneo hilo la Kagera magomeni nami nikajua teksi yetu ilikuwa tayari imewasili. Shukuru alikuja kwa haraka akinisaidia kumpeleka mke wangu kwenye gari.
Baada ya hapo tulikwenda moja kwa moja hadi hospitali ya Magomeni na kumfikisha kwenye chumba cha kujifungulia. Mimi na mdogo wangu tulikaa kwenye benchi tukiongea mawili matatu lakini kichwani mwangu nilikuwa nikiomba tu mke wangu ajifungue salama.
Saa moja mbele alikuja muuguzi(nesi) na kututaarifu kuwa mke wangu alikuwa amejifungua salama na muda si mrefu angeweza kuruhusiwa kuondoka. Nilikumbatiana na mdogo wangu na hapo ndipo wazo la kuwaambia ndugu, jamaa na marafiki kuhusu habari njema likaniingia.   Nikiwa tayari nimewatumia ujumbe watu wote muhimu, nilimuona mke wangu akitoka na mtoto mchanga mikononi mwake, akimbeba kwa kumlaza mikononi mwake naye alikuwa ameinamisha kichwa chake kwa mtoto huyo. Kwa nilivyokuwa nimemzoea mke wangu nilijua alitamani kuniangalia na kunikaribisha kwenda kumuona yule mtoto lakini aliweza kuniangalia mara moja tu na kuendelea kuangalia chini bila ya kutembea wala kufanya lolote. Uso wake haukuwa na furaha niliyoitegemea na baada ya yeye kusimama, muuguzi ambaye alikuwa amemsindikiza nje ya chumba cha kujifungulia alishika njia na kurudi kwenye chumba hicho. Mimi pamoja na mdogo wangu tulikimbilia kumpokea tukifuatiwa na mdogo wake, Jeni ambaye tayari alishawasili hospitali. Tulipomfikia, macho yangu yalitua moja kwa moja kwenye uso wa mtoto huyo na ndipo butwaa liliponishika.
Mtoto yule alikuwa akifanana na mdogo wangu Shukuru zaidi kuliko mimi mwenyewe na wakati nikimtazama Shukuru nione angestuka vipi kwa hali hiyo, niliona akiwa ameweka umakini wake kwenye miguu ya yule mtoto ambayo ilikuwa imetolewa nje ya kitambaa, viungo vilivyokuwa vimeteka umakini wa mke wangu pia. Nikishindwa kujizuia, nilijikuta nikiitazama miguu hiyo na kuona kilichokuwa kikiwashangaza wenzangu. Miguu ilionekana wazi kuwa ni dhaifu, mguu wa kushoto ukiwa mfupi kuliko wa kulia na kila mguu ulikuwa na vidole sita. Kila mtu ambaye angemuona, angejua wazi kuwa mtoto yule angekuwa kilema wa miguu. Likawa tatizo juu ya tatizo na ndiyo ukawa mwanzo wa changamoto zilizoniangamiza, mwanzo wa kubadilika kwangu na ndiyo mwanzo wa simulizi langu hili.
Kwa hasira na kutokujielewa nilitoka eneo lile huku nikiacha sauti ya Shukuru na ya mke wangu, Lilian zikiniita wakati nikielekea nje ya hospitali. Bila ya kugeuka nyuma nilitembea pembezoni mwa ukuta wa ukingo wa hospitali hata kuvuka barabara na kwenda kituo cha magomeni usalama na kupanda gari kurudi nyumbani nikiwa sijui kilichokuwa kikiendelea nyuma yangu. Nikiwa kwenye gari niliwaza na kuona isingekuwa vema kurudi nyumbani moja kwa moja, hivyo niliposhuka magomeni kagera nikaingia zangu kwenye baa moja na kuagizia bia. Mdogo wangu na mke wangu walijaribu kunipigia lakini sikutaka kupokea simu za wasaliti na kuepusha usumbufu nikaizima simu yangu.
Bia pamoja na mziki wa taratibu uliokuwa ukipigwa kwenye baa hiyo vilinisaidia kupoteza muda na mawazo lakini kabla ya kufikia hali ya kutokujitambua, nilipata wazo la kwenda kuwafukuza wote wawili pale nyumbani. Niliondoka kwenye baa hiyo nikijiongelea na kujisikitikia mwenyewe hadi nilipofika nyumbani.

[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]
  • Hadithi na Simulizi