Utangulizi...
Katika hospitali kuu ya Muhimbili karibu na wodi
ya wagonjwa mahututi, nilisimama huku nikishindwa kuelewa kama kweli yalikuwa
yakitokea au ndiyo mipango ya Mungu ilikuwa ikitimia. Niligeuka kujaribu kuona
kama wenzangu niliokuwa nimeongozana nao bado walikuwa na matumaini au kama
walishayapoteza kama mimi.
Dada wa mke wangu ambaye
alikuwa akiitwa mama Saida lakini kutokana na unene wake wengi tulikuwa
tukimuita mama Bonge pamoja na mdogo wake mke wangu aliyekuwa akiitwa Jenifer
tukilifupisha jina lake na kumuita Jeni, hawakuweza kuyazuia machozi kuwatoka.
Walikuwa wamejiinamia kwenye benchi huku vitenge vyao vikiwa mikononi mwao kwa
ajili ya kujifuta machozi. Mdogo wangu wa kike, jina lake Tumsifu alikuwa kati
kati yao akijitahidi kuwapa moyo kuhusu mdogo wao.
Mdogo wangu Shukuru yeye
alikuwa karibu yangu akitembea hapa na pale kujiongezea ujasiri. Hao ndio
niliokuwa nimeongozana nao na hakukuwa na mtu aliyeonesha kuwa na matumaini
kuhusu kupona kwa mgonjwa wetu ambaye alikuwa mahututi. Wote walikuwa
wakisubiri kudra za mwenyezi Mungu kumponyesha mgonjwa wetu.
Pilika pilika za watu katika
hospitali hiyo ya taifa hazikuisha. Wauguzi, madaktari, wagonjwa na ndugu wa
wagonjwa mbalimbali walikuwa wakipishana kuelekea huku na kule mbele ya eneo
tulilokuwepo. Sura za huzuni ndizo zilizokuwa zikionekana eneo hilo isipokuwa
kwa madaktari na wauguzi waliozoea kuona hali mbaya za binadamu.
Baada ya muda mrefu kupita
mimi na Shukuru tukiwa tumesimama wakati mama bonge, Jeni na Tumsifu wakiwa
wamejiinamia kwenye benchi karibu na wodi ya wagonjwa mahututi, wakapita watu
wakivuta machela moja na juu ya machela hiyo alikuwepo kijana mmoja akiwa
anavuja damu kichwani naye uso wake ulikuwa huonekani kutokana na lijeraha
likubwa alilolipata. Wauguzi wawili walikuwa wakijaribu kuizuia damu hiyo huku
akiendelea kupelekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Wagonjwa waliokuwa
wakipelekwa kwenye wodi hiyo kweli walikuwa na hali mbaya na mgonjwa wetu naye,
hakuwa wa kutofautishwa.
Baada ya kumuona kijana yule,
niliangalia chini nikiwaza kama ingekuwa vema kwangu kufanya ningechopaswa
kufanya au kuwa na huzuni, kusubiria neema ya Mola bila ya kujishughulisha kama
wengine. Nilijua fika kwamba mke wangu alikuwa katika hali mbaya na juhudi za
madaktari zisingeweza kuzaa matunda yoyote. Walikuwa wakijitahidi
kumshughulikia kwa elimu yao ya kisayansi lakini mimi nilijua sayansi
iliyohitajika ilikuwa ile ya giza, sayansi ya kiroho na si ya kimwili.
Nilitamani kuingia wodini
nione jinsi matibabu yalivyokuwa yakiendelea lakini nilishindwa kutokana na
mlango kufungwa. Akili ya ghafla iliniingia nami nikaifuatilia kwa haraka ile
machela mpaka walipofika mlangoni ambapo ndugu wa yule kijana, mimi nikidhaniwa
mmoja wao tukaombwa na muuguzi tuondoke eneo lile kwani tayari alishawafikia
madaktari. Wale ndugu walianza kuondoka naye muuguzi akajua wote tungeondoka
lakini mimi niliendelea kusubiri hata walipofungua mlango kumuingiza yule
kijana nikalazimisha kuchungulia na kuona mke wangu akiwa amezungukwa na
madaktari na wauguzi huku wagonjwa wengine wakiwa wameachwa kando. Niliamini
hiyo ilitokana na hali yake kuwa mbaya zaidi kuliko wengine lakini haikupita
hata nusu dakika kabla sijaombwa kuondoka eneo lile tena kwa sauti ya
kukaripiwa.
Nikiwa nasogea mbali na eneo
hilo, hasira zilianza kunipanda kichwani na kuanza kujiwazia.
‘Umeniulia kopiraiti yangu nikakuvumilia na sasa unataka unichukulie na mke
wangu?’
Nilitamani niweze kumfuata Shukuru
ili tuweze kushauriana juu ya nini cha kufanya lakini ubinafsi ulikuwa
umenitawala. Nililichukulia jambo hilo kama mashindano na nilitaka kuwa timu ya
peke yangu. Niliutaka ushindi zaidi ya kitu chochote nao haukuwa ushindi wa
peke yangu bali hata adui yangu naye angeshinda kwa namna hiyo. Ama si hivyo
basi tungeshindwa wote, yalikuwa ni mashindano ya kipekee na niliokuwa
nikishindana nao hawakuwa watu wa kawaida.
Bado nikiwa sijapata maamuzi
ya moja kwa moja nikamuona daktari mmoja akitoka kwenye wodi ile ya wagonjwa
mahututi akiwa ameinamisha kichwa chini. Nilipoziona ndevu na sharubu zake
pamoja na mawani yake machoni niliweza kumgundua kuwa ndiye daktari aliyekuwa
akimuhudumia mke wangu. Sasa alikuwa ametoka nje nami nikapata wazo la ghafla
kuwa alikuwa amemaliza kazi yake lakini kabla sijamfuata kumuulizia hali ya mke
wangu nikamuona muuguzi mmoja akimfuata na kusimama mbele yake. Alionesha
kumbembeleza kitu fulani na daktari huyo alitingisha tu kichwa huku akitanua
mikono yake kufanya ishara ya kutokujua cha kufanya. Niliogopa sana na
nikajikuta nikielekea pale walipo kwa haraka lakini hatua mbili kabla ya
kuwafikia, nilijihisi nikipooza(kuparalaizi) miguu nilipoona machela ikitoka
wodi ile nayo ikiwa na mtu aliyefunikwa shuka jeupe mwili mzima.
[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia
simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]
No comments:
Post a Comment