Thursday, August 20, 2015

Roho ya Kayumbas: Sehemu ya 4



"Eee enhee, kwa hiyo uuu..uu..umekuwa wa ngapi shuleni?"
"Nimekuwa wa thaba."
"Iii..itabidi ni..ni..nikupe zawadi. Iii..iii..ikifika Jumaa..mosi  ni..ni..nikumbushe ni..ni..nikupe hela uu..uu..uende na mmm..mmama mm..m..mkanunue nguo."
"Na mimi baba."....... "Na mimiiii, nataka nguo mpya."
Wadogo zake Kayumbas: Mjanja na Majaliwa wanaingilia na mama yake huku akinyanyuka kwenda kumuwekea chakula mumewe anasema kiutani.
"Mwenzangu kazi unayo. Wao wanataka tu nguo mpya wakati hawajui mwenzao hajapata hivi hivi tu, amefanya kazi kubwa."
Mara Mjanja anaanza kulia na baba mtu anamnyanyua na kuanza kumbembeleza akisema,
"Wote humu mmm..mmm..mtapata nguo mmmpya. Hata mm..mimi ha..ha..hata mm..mmama yenu a..a..atapata nguo mmmpya. Uu..uu..umesikia Mja? Au..au..au mmmama yeye aaa..a..asipate?"
Mjanja anaitikia kwa kichwa na kuwafanya wote pale ndani wacheke wakati huo mama Kayumbas akimaliza kuweka chakula kwa ajili ya baba Kayumbas na kummiminia maji ili anawe. Kabla ya kuanza kula, anauliza
"Mm..mm..mmama Ka, ndo uu..uu..umemchinjia mmmwanao kuku?"
"Ndiyo baba Kayumbas. Nimeona nimpongeze mwanangu."
"Eeee vi..zuri." Baba Kayumbas anawageukia wadogo zake Kayumbas na kuwauliza,
"Jenni, Mmmja na Mmmawa si mmm..mm..mnamuona ka..ka yenu aaa...aa..aanavyojitahidi? Na..na..na nyie mmm..mm..mtafaulu mmkifika darasa la n..ne?"
"Mimi nitafaulu baba." "Hata mimi mwenyewe nitafaulu." Anajibu Jennifer akifuatiwa na Majaliwa.
"Yasije kuwa ni maneno tu wana oko. Ndiyo msome kama kaka yenu." Mama yao anakuwa ameingilia mama yao.
"Na mimi nataka niende shule." Anapaza sauti Mjanja ili aweze kusikika zaidi ya dada na kaka zake waliokuwa wakijimjibu baba yao.
"Utaenda tu mwanangu, Majaliwa akiingia tu darasa la kwanza na wewe unaanza chekechea." Anajibu mama Kayumbas.
"Eeeh eeeh naanza shule." Anashangilia Mjanja asijali kama ni usiku na hapo baba yake anamkemea,
"Aaa..a..acha kelele sasa, uu..uuusiku huu."
Wanaendelea na mazungumzo ya kawaida mpaka wanapokwenda kulala.

Kesho yake asubuhi wanapoamka, pilika pilika zinaanza kama kawaida. Mapema asubuhi Kayumbas na Jennifer wanakwenda kuchota maji kwenye nyumba moja iliyopo mtaa wa pili wa ule wakaao. Wanawahi mapema sana na kuanza kugonga geti ili wafunguliwe maji.
"Na nyie? Kila siku mnakuja asubuhi asubuhi ka wanga? Mnatusumbua bwana, sisi bado tumelala." Kayumbas na Jennifer wanakaa kimya kwani haikuwa mara ya kwanza kuambiwa hivyo na watu wa nyumba hiyo. Wanamsikiliza anavyolalamika mtu huyo huku akiwafungulia geti.
"Kwa nini msiwe mnakuja wakati jua limeshachomoza?" Anauliza mfanyakazi wa ndani wa nyumba hiyo aliyekuwa mwanamke mnene mnene wa miaka inayocheza karibu na ishirini hivi.
"Si kunakuwa na foleni muda huo?" Anajibu Jennifer kwa kujiamini.
"Si mtasubiria, mbona wenzenu wanasubiria?" Anajibu akionesha kukerwa na swali la Jennifer.
"Tutachelewa shule thatha." Anajibu Kayumbas huku akilisogelea bomba na kuweka ndoo yake kwa ajili ya kujaza maji.
"Basi muwe mnachota usiku mkalala na maji."
"Aah sisi tumezoea kuchota asubuhi, usiku tunakuwa tumechoka na kazi zingine." Anajibu Jennifer.
"Aya shauri yenu. Siku mtajikuta mkichoma mahindi hapa mpaka saa moja ndo mkafunguliwa."
Hawasemi neno tena na kuchota maji. Wanarudia tena na kisha Kayumbas kumalizia ndoo yake ya tatu wakati Jennifer akiishia kuchota ndoo mbili.
Baada ya kumaliza kuchota maji, Jennifer anafagia ndani na nje ya nyumba wakati Kayumbas akikimbia kwa baiskeli kwenda kununua mboga mboga kwa ajili ya biashara ya mama yake kutoka kwenye mashamba madogo madogo mbali kidogo kutoka wanapoishi ambapo magari hayawezi kufika. Mama yao anaosha vyombo na kuanza kupika chapati kwa ajili ya kuziuza.
Jennifer anapomaliza, anapika chai kabisa na hata Kayumbas anaporudi, wanafunzi hao watatu yaani Kayumbas, Jennifer na Majaliwa wanaoga kwa ajili ya kwenda shule. Wanakunywa chai na wanapokuwa tayari, mama yao anawapa Kayumbas na Jennifer nauli na shilingi mia kila mmoja kwa ajili ya kutumia huku akimpa Majaliwa shilingi hamsini kwa ajili hiyo hiyo ya kutumia.
Bila ya kusahau fagio zao isipokuwa kwa Majaliwa, wanamuaga mama yao na kwenda zao shule. Jenifer anakwenda kupanda gari kituo cha nyumbani kwao, umbali wa kama mita mia mbili hivi lakini Kayumbas inabidi ampeleke Majaliwa shule kwanza umbali wa kama mita mia tatu hivi na ndipo apande gari la kwenda shuleni kwake.

[Endelea kufuatilia simulizi hili litokanalo na matukio ya kweli...]

2 comments:

  • Hadithi na Simulizi