Wednesday, August 12, 2015

Roho ya Kayumbas: Sehemu ya 3



Baada ya shangwe hizo na wosia, Kayumbas anaingia ndani na kubadili nguo zake akivaa nguo chakavu kidogo maalumu kwa kushindia. Kisha anamsaidia mama yake kutayarisha mboga za majani kwa ajili ya kuziuza kwa kuzitembeza. Anapomaliza kumpangia mboga hizo yakiwemo majani ya maboga, kisamvu, matembele na spinachi kwenye beseni analotumia mama yake kubebea, Kayumbas anarudi ndani na kubadili tena nguo kwa ajili ya kwenda kumchukua mdogo wake aliyeko shule ya awali umbali wa maili kadhaa.
Kayumbas anapotoka tayari kwa kumfuata mdogo wake huyo aliyeitwa Majaliwa, mama yake ambaye alikuwa akibandika maji baada ya kumaliza kumfunga kamba kuku aliyemnunua kwa mmoja wa majirani anamwambia,
"Yani mana oko nafurahishwa sana na juhudi zako. Naamini Iruwa hatakutupa kamwe."
"Mama, nitajituma kwa juhudi zote na mengine nitamuachia Mungu."
"Ila Kayu..."
Anamuita na kumvuta hadi anapokuwa karibu naye, anamshika mikono yote miwili na huku akimuangalia machoni anamuambia kwa upole.
"Unajua ya Iruwa mengi, ila naomba moyo huu wa kuwasaidia wadogo zako uendelee nao usije ukachoka hata kama Iruwa atatuchukua mapema mkabaki ninyi wenyewe."
"Mamaaa..." Anaita Kayumbas kwa sauti ya kulalamika na anapomuona mama yake akimsikiliza, anaendelea, "uthitheme hivyo mama."
"Usiogope Kayu mana oko, nakuambia tu ujue ninachokutakia katika maisha."
"Thawa mama lakini hata hivyo thiyo vizuri. Naweza kwenda mama?"
"Safari njema mana oko."
Shughuli zinaendelea na inapofika saa mbili kasorobo usiku, baba Kayumbas anarudi nyumbani na kukuta familia yake ikiwa imekusanyika sebuleni na nyuso za furaha zikiwa zimewatawala. Baada ya kupokea salamu mbali mbali kutoka kwa familia yake, anamchukua Mjanja aliye mdogo kuliko wote na kumrusha juu mara mbili kisha anambusu na kumuweka chini.
Mama Kayumbas anatazamana na Kayumbas na kisha kumtazama baba Kayumbas hadi anapofanikiwa kuangaliana naye na kusema,
"Baba Kayumbas umesikia alichokifanya mwanao?"
"Mm.. mmwa...mwanangu yupi huyo?" Anauliza baba Kayumbas akiwa na shauku ya kutaka kujua ambapo mama Kayumbas anamgeukia Kayumbas na kumwambia,
"Kayumbas hebu mwambie baba yako habari nzuri naye afahamu."
"Enhee, uuu.. umee.. umeokota aaa..aalmasi nini?" Anaingilia kati baba Kayumbas akitaka kumuharakisha Kayumbas kumfahamisha lakini anaonywa na mama Kayumbas.
"Eeeh eeh baba Kayumbas! Utawafundisha watoto kuwaza hela za bahati nasibu. Lazima utoke jasho ndiyo ufanikiwe. Siyo kwa kuokota."
"Natania tu. Ka si.. si.. si uuu..uumemuuuelewa mama yako?" Baba Kayumbas anajaribu kuufuta usemi wake na kutaka kujua kama Kayumbas aliyekuwa akimuita 'Ka' kwa ajili ya kumrahisishia maongezi, alikuwa ameielewa falsafa ya mama yake ambapo Kayumbas akamjibu,
"Ndiyo baba nimemuelewa."
"Enhee, ni..ni..ambie hizo ha... ha..habari."
"Nimefaulu mtihani wa taifa wa daratha la nne."
"Enheee, heee ni..ni..nilikwambia mimi mmm..mm..ma Ka. Anasimama kidogo na kwa sauti iliyojaa msisitizo anasema, "Mtoto tumepata." Kimya kingine cha sekunde kadhaa na kisha anamalizia, "Ho..ho..hongera sana mmm..m..mwanangu, yani ho..ho..hongera sana."
"Athante baba."Anaitikia Kayumbas na kisha baba yake anauliza,
"Eee enhee, kwa hiyo uuu..uu..umekuwa wa ngapi shuleni?"

[Endelea kufuatilia simulizi hili litokanalo na matukio ya kweli...]

kennytz na Kenneth Paul

Blogu ya kennytz inayomilikiwa na Kenneth Paul ni blogu ya Kitanzania yenye dhumuni la kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili. Katika kennytz, utapata kusoma masimulizi mbalimbali yanayoandikwa na Kenneth Paul ambaye ni msomi mwenye upeo mkubwa wa kuelewa lugha. Masimulizi ya Kenneth Paul utakayoyasoma katika kennytz yatakuwa yakitumia lugha ya Kiswahili yenye usanifu mkubwa ili kupitia masimulizi hayo, uweze kupata picha yaani ufahamu juu ya matumizi sahihi ya lugha yetu ya Kiswahili. Hata hivyo baadhi ya masimulizi yanaweza kuwa katika lugha ya Kiingereza kwa ajili ya kutoa burudani kwa wale wapenzi wasiofahamu lugha ya Kiswahili.
Pia katika kennytz, kuna kipengele cha kucheka na kuchekesha ambapo kurasa zake zinalenga maswala ya vichekesho. Kenneth Paul ni kati ya watu wenye uwezo mkubwa wa kuchekesha na kupitia utaalamu wa Kenneth Paul wa kudadisi na kupembua mambo, amejaribu kutafuta mambo mbali mbali yanayohusiana na swala la kucheka na kuchekesha watu.
Kennytz itakupa mafunzo ya lugha ya maneno, yaani kusikiliza kwa umakini maneno watumiayo watu ili kuelewa dhamira ya mazungumzo. Vile vile katika kujifunza huko, utaweza kujua maneno sahihi ya kutumia ili kuweza kufanikisha malengo ya kauli zako, kama ni kuchekesha, kuuliza swali, kutoa taarifa, kuomba msamaha, kushawishi na mengine mengi.
Kennytz pia inajaribu kuelezea mafunzo mbali mbali kutoka katika filamu ndani na nje ya Tanzania. Kenneth Paul ni mpenzi wa filamu na amekuwa akijifunza mengi kuhusu maisha kupitia filamu. Lakini Kenneth Paul amekuwa akishangazwa na namna watu wanavyochukulia kwamba filamu zipo tu kwa ajili yta kuburudisha na si kufundisha. Hivyo Kenneth Paul anafichua mafunzo mbali mbali kutoka katika filamu kupitia kennytz ambayo yatasaidia watu katika maisha.
Karibu na tembelea kennytz ya Kenneth Paul mara kwa mara kwa ajili ya burudani na mafunzo.

Monday, August 3, 2015

Kuchekesha kufuatia sababu za watu kucheka…



Sababu za watu kucheka...
Furaha ni moja ya vitu vichache na muhimu ambavyo watu wote wanaweza kumiliki bila ya kugombania vyanzo vyake. Watu wote wanaweza kuwa na furaha hata kama kutakuwa na tofauti nyingi kama za kipato, jinsia, rangi ya ngozi, uwezo wa viungo vya mwili na vitu vingine.
Kwa vile kucheka ni njia namba moja ya kuonesha kuwa na furaha, haina budi watu kuwa na utayari wa kucheka wanapokuwa na furaha. Pamoja na utayari huo, lazima kuwe na chanzo cha mtu kucheka. Chanzo hicho mara nyingi ni mtu kuchekesha kwa maandishi au matamshi au maigizo. Kitu ambacho wengi wanakosea nacho nimekigusia katika nakala zangu za kucheka ni watu kudhania kwamba swala la mtu kucheka ni matokeo ya uzuri au kueleweka kwa kichekesho pekee.  
Kila mtu amezaliwa akiwa na uwezo wa kuchekesha lakini wengi hucheka mara nyingi kuliko kuwawezesha wengine kucheka. Mfululizo wa nakala hizi unakusudia kukupa uwezo wa kuchekesha kufuatia sababu za watu kucheka hata katika mazingira yasiyokuwa na utayari wa watu kucheka au kupokea kichekesho. Kama tulivyoona hapo awali kwamba kucheka si matokeo ya kichekesho pekee, basi ili kuweza kuchekesha haina budi kuzingatia sababu kuu zinazomwezesha mtu kucheka. Baada ya kuona sababu hizo, katika nakala zijazo tutaanza kuona ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa wachekeshaji asilia, yaani wale wa wakati wote bila kutegemea kuwa na kichekesho kizuri akilini.
Sababu ambayo wataalamu wengi wa kisayansi wanaamini ya kuwa namba moja ya mtu kucheka ni kwamba watu hucheka ili kutengeneza mahusiano katika jamii. Ni ishara itumiwayo kumualika mtu kuanzisha mahusiano na pia katika kuendeleza mahusiano. Hii hudhihirika pawapo na vichekesho bubu, yaani watu wawili wanaweza kuangaliana tu na mmoja kuanza kumchekea mwenzake. Hiyo hasa hutokea kwa jinsia mbili tofauti. Kuchekesha kwa kutumia njia hii, ipo nje ya malengo ya blogu.
Sababu nyingine inayoweza kushika namba mbili ni kucheka baada ya kuwa na uelewa unaofanana na mtu mwingine. Kucheka kwa namna hii, hakutegemei sana uzuri wa kichekesho. Watu wawili au zaidi wanapoona tukio fulani linalofanana na tukio jingine lililowahi kutokea, basi huangaliana walionapo tukio hilo la sasa na kisha kucheka baada ya kuhisi kwamba wote wamekumbuka tukio hilo la nyuma. Kwa kumuelewa vizuri mlengwa wa kuchekesha kwako, unaweza kuitumia njia hii.
Sababu nyingine ya kucheka ni kichekesho chenyewe. Hapa sina haja ya kuelezea sana kwa sasa kwani kila mtu anaelewa kwamba usomapo au kusikia au kuona kichekesho fulani basi mtu hujikuta akicheka. Lakini mimi bado najiuliza swali moja, ‘Je, mtu ukiwa peke yako na ukiwa na mtu mwingine jirani, kwa nini inakuwa rahisi kucheka uwapo na mtu kuliko ukiwa mwenyewe?’ Katika nakala zijazo, nitajikita katika kipengele hiki ambacho wengi wanakichukulia kama mzizi wa kuchekesha.
Sababu nyingine kubwa ambayo mara zote hufanya watu kucheka, ni kutokufikirika kwa jambo linalofanyika. Lugha inaweza kuwa ngumu lakini nazungumzia pale watu wanapocheka na mmoja kusema, ‘Dah, sijui huyu jamaa alikuwa anafikiria nini.’ Au ‘Duh, sijui hawa watu huwa wanafikiria nini.’ Sifa za jambo hilo ni kuwezekana kufanyika lakini watu kikawaida huwa hawalifanyi. Hii ni njia ya uhakika ya kuchekesha ambayo nitaielezea katika nakala zijazo.
Nakala hii inakuwa ndefu na sasa nifupishe sababu mbili za mwisho zilizobaki zinazomfanya mtu acheke lakini haziwezi kutumika kuchekesha. Sababu hizi ndiyo hasa pale tunasema kujichekesha. Moja ni mtu kucheka kufuatia kukosa kile alichokuwa akikitarajia. Kwa mfano mtu aulizwapo swali gumu au aonapo dalili za kushindwa anaweza kucheka bila ya kuwepo kichekesho, kicheko chenye chembe chembe za kujibeza. Na mwisho ni mtu kucheka ama kujichekesha kuficha hisia mbaya alizokuwa nazo. Mtu anaweza kucheka atokewapo na jambo baya kama vile kutukanwa na mwenzake ili kuficha hisia za kukasirika kwake. Njia hizi mbili za mwisho ni ngumu kuzitumia katika kuchekesha.
Katika nakala ijayo katika nakala hizi za kuchekesha, tutaona umuhimu wa kujua kuchekesha..
  • Hadithi na Simulizi