Thursday, August 13, 2015

Damu Ya Ukoo Wangu: Sehemu Ya 4

Ilikuwa  alfajiri majira ya saa kumi na moja nikiwa bado nimelala fofofo, huku kaubaridi cha usiku kakiwa kameanza kupotea katika eneo tulilokuwa tukiishi lenye nyumba nyingi za karibu karibu, na ndege wasiopendwa na wengi aina ya kunguru wakianza kupiga kelele zao za kuamshana nilisikia kilio cha uchungu kutoka kwa mke wangu aitwaye Lilian, mtoto wa kingoni kutoka Songea. Niliamka kwa haraka na kwenda kuwasha taa. Baada ya kufikicha macho yangu nikaweza kuona jinsi mke wangu alivyokuwa akitaabika na huku matone ya damu yakiichafua shuka.
Nikatoka nje ya chumba chetu na kwenda kwa mdogo wangu aitwaye Shukuru aliyekuwa akiishi chumba cha nje cha nyumba yetu na kumgongea mlango kwa nguvu. Alipofungua mlango bila hata ya kuuliza nani aliyekuwa akigonga, moja kati ya vitendo vya kijasiri alivyokuwa akifanya Shukuru, nilimueleza kuwa wakati ulikuwa umewadia kwa mke wangu. Baada tu ya kumwambia habari hizo akaniambia nirudi kwa mke wangu tujiandae wakati yeye akifanya mipango ya kupata teksi.
Nilirudi kwa mke wangu kwa haraka na kumuomba ajitahidi kuvumilia wakati teksi ikija kwani hatukuwa mbali na barabarani na eneo hilo lilikuwa likiwahi kukicha kuliko sehemu nyingi zingine za Dar es Salaam. Huku nikimpa maneno ya kumtia nguvu mke wangu, nilimsaidia kunawa uso na wote kuvaa nguo za kiheshima. Hazikupita dakika tano nikasikia honi ikipigwa karibu na nyumba yetu eneo hilo la Kagera magomeni nami nikajua teksi yetu ilikuwa tayari imewasili. Shukuru alikuja kwa haraka akinisaidia kumpeleka mke wangu kwenye gari.
Baada ya hapo tulikwenda moja kwa moja hadi hospitali ya Magomeni na kumfikisha kwenye chumba cha kujifungulia. Mimi na mdogo wangu tulikaa kwenye benchi tukiongea mawili matatu lakini kichwani mwangu nilikuwa nikiomba tu mke wangu ajifungue salama.
Saa moja mbele alikuja muuguzi(nesi) na kututaarifu kuwa mke wangu alikuwa amejifungua salama na muda si mrefu angeweza kuruhusiwa kuondoka. Nilikumbatiana na mdogo wangu na hapo ndipo wazo la kuwaambia ndugu, jamaa na marafiki kuhusu habari njema likaniingia.   Nikiwa tayari nimewatumia ujumbe watu wote muhimu, nilimuona mke wangu akitoka na mtoto mchanga mikononi mwake, akimbeba kwa kumlaza mikononi mwake naye alikuwa ameinamisha kichwa chake kwa mtoto huyo. Kwa nilivyokuwa nimemzoea mke wangu nilijua alitamani kuniangalia na kunikaribisha kwenda kumuona yule mtoto lakini aliweza kuniangalia mara moja tu na kuendelea kuangalia chini bila ya kutembea wala kufanya lolote. Uso wake haukuwa na furaha niliyoitegemea na baada ya yeye kusimama, muuguzi ambaye alikuwa amemsindikiza nje ya chumba cha kujifungulia alishika njia na kurudi kwenye chumba hicho. Mimi pamoja na mdogo wangu tulikimbilia kumpokea tukifuatiwa na mdogo wake, Jeni ambaye tayari alishawasili hospitali. Tulipomfikia, macho yangu yalitua moja kwa moja kwenye uso wa mtoto huyo na ndipo butwaa liliponishika.
Mtoto yule alikuwa akifanana na mdogo wangu Shukuru zaidi kuliko mimi mwenyewe na wakati nikimtazama Shukuru nione angestuka vipi kwa hali hiyo, niliona akiwa ameweka umakini wake kwenye miguu ya yule mtoto ambayo ilikuwa imetolewa nje ya kitambaa, viungo vilivyokuwa vimeteka umakini wa mke wangu pia. Nikishindwa kujizuia, nilijikuta nikiitazama miguu hiyo na kuona kilichokuwa kikiwashangaza wenzangu. Miguu ilionekana wazi kuwa ni dhaifu, mguu wa kushoto ukiwa mfupi kuliko wa kulia na kila mguu ulikuwa na vidole sita. Kila mtu ambaye angemuona, angejua wazi kuwa mtoto yule angekuwa kilema wa miguu. Likawa tatizo juu ya tatizo na ndiyo ukawa mwanzo wa changamoto zilizoniangamiza, mwanzo wa kubadilika kwangu na ndiyo mwanzo wa simulizi langu hili.
Kwa hasira na kutokujielewa nilitoka eneo lile huku nikiacha sauti ya Shukuru na ya mke wangu, Lilian zikiniita wakati nikielekea nje ya hospitali. Bila ya kugeuka nyuma nilitembea pembezoni mwa ukuta wa ukingo wa hospitali hata kuvuka barabara na kwenda kituo cha magomeni usalama na kupanda gari kurudi nyumbani nikiwa sijui kilichokuwa kikiendelea nyuma yangu. Nikiwa kwenye gari niliwaza na kuona isingekuwa vema kurudi nyumbani moja kwa moja, hivyo niliposhuka magomeni kagera nikaingia zangu kwenye baa moja na kuagizia bia. Mdogo wangu na mke wangu walijaribu kunipigia lakini sikutaka kupokea simu za wasaliti na kuepusha usumbufu nikaizima simu yangu.
Bia pamoja na mziki wa taratibu uliokuwa ukipigwa kwenye baa hiyo vilinisaidia kupoteza muda na mawazo lakini kabla ya kufikia hali ya kutokujitambua, nilipata wazo la kwenda kuwafukuza wote wawili pale nyumbani. Niliondoka kwenye baa hiyo nikijiongelea na kujisikitikia mwenyewe hadi nilipofika nyumbani.

[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]

Wednesday, August 12, 2015

Umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho…



Kuchekesha bila kukariri vichekesho haimaanishi kuwa na uwezo wa kutunga vichekesho vipya au kuvibadilisha vichekesho vilivyopo. Ninachojaribu kumaanisha kwa umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho ni sababu za kuchekesha bila ya kutumia vichekesho(kifungu cha kauli zenye lengo la kuchekesha.)
Miaka mingi iliyopita, nikiwa mtu ninayejali mambo ya muhimu peke yake, sikuona umuhimu wa kuchekesha wala kucheka vichekesho vya watu. Sisemi maisha yalikuwa mabaya au magumu lakini hali ya sasa ni nzuri zaidi kuliko huko nyuma. Muda ulivyokuwa ukienda mbele nilianza kuona umuhimu wa kujua kuchekesha, acha ile mara moja mara mbili ambayo mtu yeyote anaweza kuchekesha. Nilitamani kuwa na uwezo wa kuchekesha kwa haraka zaidi na mazingira magumu zaidi. Unajua nilichokifanya?
Nilianza kutembelea mitandao mbali mbali inayoandika vichekesho na kuanza kuvikariri vichekesho hivyo. Ingawa vichekesho hivyo vilikuwa kwa lugha ya kiingereza, niliweza kuvibadilisha na kuvisimulia kwa Kiswahili kwa namna ambayo ilichekesha. Kadiri siku zilivyokwenda nami nikawa nikitafuta vichekesho hivyo kwa udi na uvumba ili wale waliouona uwezo wangu wa kuchekesha wasiache kunisikia nikichekesha. Halikuwa jambo baya lakini vichekesho hivyo vikawa kama vikijirudia rudia na kuniboa. Hapo ndipo nikaona umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho.
Umuhimu hasa ni kuwa na uwezo wa kuchekesha muda wote na mahali popote. Lakini bado kuna haja ya kuzungumzia umuhimu wa kuchekesha kwa ujumla wake. Katika hali ya kawaida, faida kubwa ya kuchekesha ni kujenga na/au kuimarisha mahusiano baina ya watu. Ipo wazi kwamba watu wanaochekesha huwa na mahusiano na watu wengi zaidi kuliko wale wasiochekesha lakini ikumbukwe pia kuwa kuchekesha kila wakati huweza kufanya watu wakutoe maana, yaani uonekane mtu asiyeweza kuwa makini. Kama ni mfanyakazi, kumchekesha bosi wako kutaimarisha uhusiano wako na bosi huyo na unajuaje faida ya kuwa karibu zaidi na bosi wako kuliko wafanyakazi wengine?
Umuhimu mwingine wa kuchekesha ni kutumiwa kama ajira. Mifano hai ipo kwa wale wenye vipindi vya kuchekesha na kila stesheni, ina vipindi hivyo. Naomba nisihi kwamba kuchekesha siyo tu kutakupatia ajira ya kuchekesha, bali ajira nyingi zinazohusisha kuhudumia watu wengi basi kuchekesha kwako, kutakuongezea uwezekano wa wewe kupata ajira. Kwani hujawahi kusikia watu wakati wakitafuta mwongozaji wa sherehe wakisema, “Wee? Kuna MC huyo anaitwa Kafupi, yaani balaa kwa kuchekesha. Tumchukue huyo huyo.” Pia hujakutana na wagonjwa wanaompendelea daktari fulani kwa sababu anaongea nao vizuri? Anawachekesha?
Nimeanza na hali ya kawaida, nikafuata yenye umuhimu kidogo na sasa nizungumzie umuhimu wa kuchekesha katika hali ambayo watu wengi hushindwa kufikiria umuhimu wa kuchekesha katika mazingira hayo. Hapa ndipo hasa penye umuhimu wa kuchekesha bila ya kukariri vichekesho. Nazungumzia kuchekesha kama njia ya kukwepa hali tata upande wako. Inaweza kuwa kukwepa swali gumu kwenye mahojiano, kuinua au kubadili mkondo wa ushindi kwenye majibizano na hata kuficha ubaya unaotaka kujitokeza.
Pata picha unakwenda kwenye masaili(mahojiano) ya kazi na umeme umekatika siku hiyo. Ukaenda na shati lililojikunja sana ukiiamini elimu na ujuzi wako kuliko umaridadi wako lakini kati kati ya intavyu, mmoja wa wanaokuhoji akakuuliza, “Kwa nini umevaa shati lililojikunja sana wakati unajua unakwenda kwenye intavyu?”
Katika hali ya kawaida mtu anaweza kujaribu kutoa sababu nyingi, ‘umeme umekatika, nimeibiwa shati langu nililotayarisha, nje tu ya ofisi nimemwagiwa juisi hivyo hili siyo langu.. n.k) ambazo zinaweza kuzua maswali mengine na mwisho wa siku kuonekana mtu ambaye hukujiandaa mapema au kwa kiingereza naomba niseme, ‘careless.’(keyales). Kwa mimi ningejibu au ningeshauri mtu yeyote ili kuondoa umakini wa wale wanaokuuliza katika jambo hilo kwa namna inayofanana na jibu hili.
“Ooh, huu ni utamaduni kwetu. Bibi yangu mzaa babu aliniambia nikitaka kufanikiwa kwenye intavyu kama hizi, nisipige pasi nguo.” Kama bahati mbaya kuna mdudu kwenye nguo na umeulizwa, unaweza sema, “Ooh, kuna mtu ananitakia kila la kheri kutoka kijijini kwetu.”

Kuna kipindi nilikuwa katika masaili ya kupewa ufadhili wa masomo nao ungetegemea uwezo wangu wa kufaulu. Matokeo yangu ya mtihani wa Taifa yalikuwa mazuri lakini mfadhili hakuamini mara moja na katika kutokuamini kwake akauliza, “Lakini nasikia shuleni kwenu wasimamizi wa necta huwa wanalipwa.”
Nadhani unaweza kujua kwamba kukataa kungeleta maswali zaidi na kukubali kungeashiria nisiaminiwe kwa matokeo tu ya necta. Bila ya kutetereka nilimjibu,
“Yah, ofkoz huwa wanalipwa.” Nikavuta muda kidogo na kumalizia, “Na Necta (yaani baraza la mitihani) lakini.” Wote katika chumba walicheka na kutohoji tena kuhusu maswala hayo.
Sasa tumeona umuhimu wa kujua kuchekesha bila ya kukariri vichekesho, katika nakala ijayo tutaona hatua zinazofuatwa katika kucheka na hivyo hatua za kufuata katika kuchekesha…

Roho ya Kayumbas: Sehemu ya 3



Baada ya shangwe hizo na wosia, Kayumbas anaingia ndani na kubadili nguo zake akivaa nguo chakavu kidogo maalumu kwa kushindia. Kisha anamsaidia mama yake kutayarisha mboga za majani kwa ajili ya kuziuza kwa kuzitembeza. Anapomaliza kumpangia mboga hizo yakiwemo majani ya maboga, kisamvu, matembele na spinachi kwenye beseni analotumia mama yake kubebea, Kayumbas anarudi ndani na kubadili tena nguo kwa ajili ya kwenda kumchukua mdogo wake aliyeko shule ya awali umbali wa maili kadhaa.
Kayumbas anapotoka tayari kwa kumfuata mdogo wake huyo aliyeitwa Majaliwa, mama yake ambaye alikuwa akibandika maji baada ya kumaliza kumfunga kamba kuku aliyemnunua kwa mmoja wa majirani anamwambia,
"Yani mana oko nafurahishwa sana na juhudi zako. Naamini Iruwa hatakutupa kamwe."
"Mama, nitajituma kwa juhudi zote na mengine nitamuachia Mungu."
"Ila Kayu..."
Anamuita na kumvuta hadi anapokuwa karibu naye, anamshika mikono yote miwili na huku akimuangalia machoni anamuambia kwa upole.
"Unajua ya Iruwa mengi, ila naomba moyo huu wa kuwasaidia wadogo zako uendelee nao usije ukachoka hata kama Iruwa atatuchukua mapema mkabaki ninyi wenyewe."
"Mamaaa..." Anaita Kayumbas kwa sauti ya kulalamika na anapomuona mama yake akimsikiliza, anaendelea, "uthitheme hivyo mama."
"Usiogope Kayu mana oko, nakuambia tu ujue ninachokutakia katika maisha."
"Thawa mama lakini hata hivyo thiyo vizuri. Naweza kwenda mama?"
"Safari njema mana oko."
Shughuli zinaendelea na inapofika saa mbili kasorobo usiku, baba Kayumbas anarudi nyumbani na kukuta familia yake ikiwa imekusanyika sebuleni na nyuso za furaha zikiwa zimewatawala. Baada ya kupokea salamu mbali mbali kutoka kwa familia yake, anamchukua Mjanja aliye mdogo kuliko wote na kumrusha juu mara mbili kisha anambusu na kumuweka chini.
Mama Kayumbas anatazamana na Kayumbas na kisha kumtazama baba Kayumbas hadi anapofanikiwa kuangaliana naye na kusema,
"Baba Kayumbas umesikia alichokifanya mwanao?"
"Mm.. mmwa...mwanangu yupi huyo?" Anauliza baba Kayumbas akiwa na shauku ya kutaka kujua ambapo mama Kayumbas anamgeukia Kayumbas na kumwambia,
"Kayumbas hebu mwambie baba yako habari nzuri naye afahamu."
"Enhee, uuu.. umee.. umeokota aaa..aalmasi nini?" Anaingilia kati baba Kayumbas akitaka kumuharakisha Kayumbas kumfahamisha lakini anaonywa na mama Kayumbas.
"Eeeh eeh baba Kayumbas! Utawafundisha watoto kuwaza hela za bahati nasibu. Lazima utoke jasho ndiyo ufanikiwe. Siyo kwa kuokota."
"Natania tu. Ka si.. si.. si uuu..uumemuuuelewa mama yako?" Baba Kayumbas anajaribu kuufuta usemi wake na kutaka kujua kama Kayumbas aliyekuwa akimuita 'Ka' kwa ajili ya kumrahisishia maongezi, alikuwa ameielewa falsafa ya mama yake ambapo Kayumbas akamjibu,
"Ndiyo baba nimemuelewa."
"Enhee, ni..ni..ambie hizo ha... ha..habari."
"Nimefaulu mtihani wa taifa wa daratha la nne."
"Enheee, heee ni..ni..nilikwambia mimi mmm..mm..ma Ka. Anasimama kidogo na kwa sauti iliyojaa msisitizo anasema, "Mtoto tumepata." Kimya kingine cha sekunde kadhaa na kisha anamalizia, "Ho..ho..hongera sana mmm..m..mwanangu, yani ho..ho..hongera sana."
"Athante baba."Anaitikia Kayumbas na kisha baba yake anauliza,
"Eee enhee, kwa hiyo uuu..uu..umekuwa wa ngapi shuleni?"

[Endelea kufuatilia simulizi hili litokanalo na matukio ya kweli...]
  • Hadithi na Simulizi