Thursday, August 13, 2015

Damu Ya Ukoo Wangu: Sehemu Ya 4

Ilikuwa  alfajiri majira ya saa kumi na moja nikiwa bado nimelala fofofo, huku kaubaridi cha usiku kakiwa kameanza kupotea katika eneo tulilokuwa tukiishi lenye nyumba nyingi za karibu karibu, na ndege wasiopendwa na wengi aina ya kunguru wakianza kupiga kelele zao za kuamshana nilisikia kilio cha uchungu kutoka kwa mke wangu aitwaye Lilian, mtoto wa kingoni kutoka Songea. Niliamka kwa haraka na kwenda kuwasha taa. Baada ya kufikicha macho yangu nikaweza kuona jinsi mke wangu alivyokuwa akitaabika na huku matone ya damu yakiichafua shuka.
Nikatoka nje ya chumba chetu na kwenda kwa mdogo wangu aitwaye Shukuru aliyekuwa akiishi chumba cha nje cha nyumba yetu na kumgongea mlango kwa nguvu. Alipofungua mlango bila hata ya kuuliza nani aliyekuwa akigonga, moja kati ya vitendo vya kijasiri alivyokuwa akifanya Shukuru, nilimueleza kuwa wakati ulikuwa umewadia kwa mke wangu. Baada tu ya kumwambia habari hizo akaniambia nirudi kwa mke wangu tujiandae wakati yeye akifanya mipango ya kupata teksi.
Nilirudi kwa mke wangu kwa haraka na kumuomba ajitahidi kuvumilia wakati teksi ikija kwani hatukuwa mbali na barabarani na eneo hilo lilikuwa likiwahi kukicha kuliko sehemu nyingi zingine za Dar es Salaam. Huku nikimpa maneno ya kumtia nguvu mke wangu, nilimsaidia kunawa uso na wote kuvaa nguo za kiheshima. Hazikupita dakika tano nikasikia honi ikipigwa karibu na nyumba yetu eneo hilo la Kagera magomeni nami nikajua teksi yetu ilikuwa tayari imewasili. Shukuru alikuja kwa haraka akinisaidia kumpeleka mke wangu kwenye gari.
Baada ya hapo tulikwenda moja kwa moja hadi hospitali ya Magomeni na kumfikisha kwenye chumba cha kujifungulia. Mimi na mdogo wangu tulikaa kwenye benchi tukiongea mawili matatu lakini kichwani mwangu nilikuwa nikiomba tu mke wangu ajifungue salama.
Saa moja mbele alikuja muuguzi(nesi) na kututaarifu kuwa mke wangu alikuwa amejifungua salama na muda si mrefu angeweza kuruhusiwa kuondoka. Nilikumbatiana na mdogo wangu na hapo ndipo wazo la kuwaambia ndugu, jamaa na marafiki kuhusu habari njema likaniingia.   Nikiwa tayari nimewatumia ujumbe watu wote muhimu, nilimuona mke wangu akitoka na mtoto mchanga mikononi mwake, akimbeba kwa kumlaza mikononi mwake naye alikuwa ameinamisha kichwa chake kwa mtoto huyo. Kwa nilivyokuwa nimemzoea mke wangu nilijua alitamani kuniangalia na kunikaribisha kwenda kumuona yule mtoto lakini aliweza kuniangalia mara moja tu na kuendelea kuangalia chini bila ya kutembea wala kufanya lolote. Uso wake haukuwa na furaha niliyoitegemea na baada ya yeye kusimama, muuguzi ambaye alikuwa amemsindikiza nje ya chumba cha kujifungulia alishika njia na kurudi kwenye chumba hicho. Mimi pamoja na mdogo wangu tulikimbilia kumpokea tukifuatiwa na mdogo wake, Jeni ambaye tayari alishawasili hospitali. Tulipomfikia, macho yangu yalitua moja kwa moja kwenye uso wa mtoto huyo na ndipo butwaa liliponishika.
Mtoto yule alikuwa akifanana na mdogo wangu Shukuru zaidi kuliko mimi mwenyewe na wakati nikimtazama Shukuru nione angestuka vipi kwa hali hiyo, niliona akiwa ameweka umakini wake kwenye miguu ya yule mtoto ambayo ilikuwa imetolewa nje ya kitambaa, viungo vilivyokuwa vimeteka umakini wa mke wangu pia. Nikishindwa kujizuia, nilijikuta nikiitazama miguu hiyo na kuona kilichokuwa kikiwashangaza wenzangu. Miguu ilionekana wazi kuwa ni dhaifu, mguu wa kushoto ukiwa mfupi kuliko wa kulia na kila mguu ulikuwa na vidole sita. Kila mtu ambaye angemuona, angejua wazi kuwa mtoto yule angekuwa kilema wa miguu. Likawa tatizo juu ya tatizo na ndiyo ukawa mwanzo wa changamoto zilizoniangamiza, mwanzo wa kubadilika kwangu na ndiyo mwanzo wa simulizi langu hili.
Kwa hasira na kutokujielewa nilitoka eneo lile huku nikiacha sauti ya Shukuru na ya mke wangu, Lilian zikiniita wakati nikielekea nje ya hospitali. Bila ya kugeuka nyuma nilitembea pembezoni mwa ukuta wa ukingo wa hospitali hata kuvuka barabara na kwenda kituo cha magomeni usalama na kupanda gari kurudi nyumbani nikiwa sijui kilichokuwa kikiendelea nyuma yangu. Nikiwa kwenye gari niliwaza na kuona isingekuwa vema kurudi nyumbani moja kwa moja, hivyo niliposhuka magomeni kagera nikaingia zangu kwenye baa moja na kuagizia bia. Mdogo wangu na mke wangu walijaribu kunipigia lakini sikutaka kupokea simu za wasaliti na kuepusha usumbufu nikaizima simu yangu.
Bia pamoja na mziki wa taratibu uliokuwa ukipigwa kwenye baa hiyo vilinisaidia kupoteza muda na mawazo lakini kabla ya kufikia hali ya kutokujitambua, nilipata wazo la kwenda kuwafukuza wote wawili pale nyumbani. Niliondoka kwenye baa hiyo nikijiongelea na kujisikitikia mwenyewe hadi nilipofika nyumbani.

[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]

No comments:

Post a Comment

  • Hadithi na Simulizi