Kabla sijazungumzia
hatua za kufuata katika kuchekesha, ningependa kugusia hatua ambazo mtu hufuata
wakati wa kucheka. Si mara zote hatua hizi hufuatwa zote na si mara zote hatua
hizi hufuatwa kimpangilio. Lakini, izingatiwe kwamba zaidi ya asilimia
themanini wakati wa kucheka, hatua hizi hufuatwa.
Mara nyingi katika
kucheka, huanza kwa matayarisho au utayari wa kucheka. Ni mara chache sana mtu
hucheka bila ya kuwa ametayarishwa ingawa vichekesho visivyopitia mtu kutayarishwa
ndivyo husababisha kuchekesha zaidi. Kwa kupitia utayari huo, kucheka kunaweza
kutokea kwa namna mbili. Kwanza na mara nyingi ni pale mtu anapotayarishwa naye
kujua tukio linalofuata linahusisha kucheka. Mfano, watu wengi hupenda kusema,
“Ngoja, nikuchekeshe bwana…” au misemo inayoendana na huo. Mfano mwingine ni
pale mtu anaposoma kichekesho kwenye simu yake na kuanza kucheka akijua
unamuona. Kisha mtu huyo bila ya kupoteza muda, pengine bado akicheka
anamuonesha kichekesho hicho mtu mwingine. Kwa namna hii, mtu anakuwa
ametayarishwa kwa kucheka wazi wazi. Pili, ni pale mtu anapotayarishwa bila ya
kuwa na uhakika kama kauli zitahusisha kuchekesha au hapana. Utayarishaji huu
wa pili, ndio wenye nguvu zaidi katika kuchekesha. Mtu huhisi kitu fulani cha
kuchekesha kwamba kitatokea bila ya kuwa na uhakika Kisha kitu hicho kinapokuwa
kweli, ndipo mtu anajikuta katika hali ya kucheka.
Hatua ya pili katika
kucheka ni kusikia au kuona ama kusoma kichekesho. Hapa mtu husikia kauli au
mfuatano wa sentensi wenye lengo la kuchekesha. Sina haja ya kuelezea maana ya
kichekesho au namna vichekesho vilivyo kwani naamini hata mtoto atakayezaliwa
kesho anajua maana ya kichekesho.
Hatua ya tatu katika
kucheka ni mtu kukihusisha kichekesho na sehemu ya ubongo wake itakayokitafakari
kichekesho kile na kujenga uhusiano na picha fulani kichwani mwake.
Mchekeshwaji hujaribu kutafuta uhusiano baina ya kichekesho na matukio
yaliyowahi kutokea huko nyuma ama matukio aliyowahi kuyasikia na kuyajengea
picha kichwani au kujenga picha fulani kichwani akitumia wahusika na mandhari
anayoitambua vema. Yaani kujaribu kupata picha mtu anayemjua au mahali
anapopajua panatokea kilichoelezwa kwenye kichekesho hicho.
Hatua ya mwisho katika
kucheka, yaani kucheka kwenyewe kunategemea sana na hatua ya nyuma yake. Kama
mtu ataweza kujenga picha fulani au kukumbuka picha fulani inayoendana na
kichekesho kwa kutumia wahusika na mandhari aijuayo vema, basi mtu huyu lazima
atacheka.
Hatua za kufuata katika
kuchekesha…
Baada ya kuelewa hatua
zinazofuatwa mara nyingi katika kucheka, ni vema kuzingatia hatua hizo katika
kuchekesha pia. Yaani ili kujihakikishia kwamba kichekesho chako hakipotei
bure, ni vizuri kama utafuata hatua za kucheka ili kuchekesha.
Katika kumtayarisha mtu
kwa kucheka, ni busara kuanza kufanyia mazoezi kumtayarisha mtu bila kumuweka
wazi kwamba una nia ya kuchekesha. Baadhi ya watu husema kwamba Tanzania hatuna
watu wenye uwezo wa kuchekesha lakini nikitathmini, naona kwamba
kinachokosekana ni utayari wa watu kucheka na pengine ni kufeli katika
kuwatayarisha watu kucheka. Njia nzuri ya kutayarisha watu kucheka ni kuruka
hatua ya kutoa kichekesho na kumpa mlengwa muda wa kutengeneza picha kuhusu
maelezo. Yaani kumfanya mtu aende hatua ya tatu hapo juu kabla ya kupita ya
pili na kisha kuendelea na kichekesho. Ndiyo, wachekeshaji wengi hasa wale
wafanyao ana kwa ana mbele za watu, hutumia njia hiyo ya kutayarisha.
Umewahi kusikia mtu
akiuliza, “Niseme nisiseme?” na baada ya hapo kauli inayofuata inavunja watu
mbavu? Hapo, mtu hufanya watu kujenga picha mbali mbali na kwa namna moja ama
nyingine kuweka uwezekano wa kutokea kichekesho. Hivi karibuni, niliona njia
hiyo ikitumiwa na Mhe. Mbowe akitoa hotuba baada ya Mhe. Lowassa kuchukua kadi.
Baada ya kuongea mengi, alisema
“Katika ujio huu, kuna
mtu mmoja ningependa kumshukuru sana.” Akakaa kimya na kuuliza, “Niseme
nisiseme?” Bila shaka alijua alichokuwa akikifanya kwani baada ya kuambiwa
aseme(jambo lililokuwa halihitaji kuuliza), Mhe. Mbowe akasema anamshukuru Mhe.
Rais na kuweza kuangusha vicheko kwa wanaukawa.
Ukimaliza kumtayarisha
mlengwa kwa kucheka, kinachofuata ni kutoa kichekesho kwa namna inayotoa muda
mtu kuhusisha kichekesho na ile picha aliyoijenga kichwani. Yaani usikimbilie
kusema kichekesho chako mwanzo mpaka mwisho bila kuwa na vituo vya kumpa mtu
muda wa kubashiri mwisho wa maelezo yako kabla hujamaliza.
Kimsingi hizo ndizo
hatua za kufuata katika kuchekesha. Si nyingi lakini umakini na mazoezi
vinahitajika kabla ya vitu uwezo huo wa kuchekesha kukaa kwenye damu.
Katika nakala ijayo,
tutaangalia namna ya kuvitumia vichekesho ulivyoviona kwa ajili ya kuchekesha.
Hii ni changamoto kwa wengi lakini uvumbuzi unakuja hapa.
No comments:
Post a Comment