Monday, August 3, 2015

Kuchekesha kufuatia sababu za watu kucheka…



Sababu za watu kucheka...
Furaha ni moja ya vitu vichache na muhimu ambavyo watu wote wanaweza kumiliki bila ya kugombania vyanzo vyake. Watu wote wanaweza kuwa na furaha hata kama kutakuwa na tofauti nyingi kama za kipato, jinsia, rangi ya ngozi, uwezo wa viungo vya mwili na vitu vingine.
Kwa vile kucheka ni njia namba moja ya kuonesha kuwa na furaha, haina budi watu kuwa na utayari wa kucheka wanapokuwa na furaha. Pamoja na utayari huo, lazima kuwe na chanzo cha mtu kucheka. Chanzo hicho mara nyingi ni mtu kuchekesha kwa maandishi au matamshi au maigizo. Kitu ambacho wengi wanakosea nacho nimekigusia katika nakala zangu za kucheka ni watu kudhania kwamba swala la mtu kucheka ni matokeo ya uzuri au kueleweka kwa kichekesho pekee.  
Kila mtu amezaliwa akiwa na uwezo wa kuchekesha lakini wengi hucheka mara nyingi kuliko kuwawezesha wengine kucheka. Mfululizo wa nakala hizi unakusudia kukupa uwezo wa kuchekesha kufuatia sababu za watu kucheka hata katika mazingira yasiyokuwa na utayari wa watu kucheka au kupokea kichekesho. Kama tulivyoona hapo awali kwamba kucheka si matokeo ya kichekesho pekee, basi ili kuweza kuchekesha haina budi kuzingatia sababu kuu zinazomwezesha mtu kucheka. Baada ya kuona sababu hizo, katika nakala zijazo tutaanza kuona ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa wachekeshaji asilia, yaani wale wa wakati wote bila kutegemea kuwa na kichekesho kizuri akilini.
Sababu ambayo wataalamu wengi wa kisayansi wanaamini ya kuwa namba moja ya mtu kucheka ni kwamba watu hucheka ili kutengeneza mahusiano katika jamii. Ni ishara itumiwayo kumualika mtu kuanzisha mahusiano na pia katika kuendeleza mahusiano. Hii hudhihirika pawapo na vichekesho bubu, yaani watu wawili wanaweza kuangaliana tu na mmoja kuanza kumchekea mwenzake. Hiyo hasa hutokea kwa jinsia mbili tofauti. Kuchekesha kwa kutumia njia hii, ipo nje ya malengo ya blogu.
Sababu nyingine inayoweza kushika namba mbili ni kucheka baada ya kuwa na uelewa unaofanana na mtu mwingine. Kucheka kwa namna hii, hakutegemei sana uzuri wa kichekesho. Watu wawili au zaidi wanapoona tukio fulani linalofanana na tukio jingine lililowahi kutokea, basi huangaliana walionapo tukio hilo la sasa na kisha kucheka baada ya kuhisi kwamba wote wamekumbuka tukio hilo la nyuma. Kwa kumuelewa vizuri mlengwa wa kuchekesha kwako, unaweza kuitumia njia hii.
Sababu nyingine ya kucheka ni kichekesho chenyewe. Hapa sina haja ya kuelezea sana kwa sasa kwani kila mtu anaelewa kwamba usomapo au kusikia au kuona kichekesho fulani basi mtu hujikuta akicheka. Lakini mimi bado najiuliza swali moja, ‘Je, mtu ukiwa peke yako na ukiwa na mtu mwingine jirani, kwa nini inakuwa rahisi kucheka uwapo na mtu kuliko ukiwa mwenyewe?’ Katika nakala zijazo, nitajikita katika kipengele hiki ambacho wengi wanakichukulia kama mzizi wa kuchekesha.
Sababu nyingine kubwa ambayo mara zote hufanya watu kucheka, ni kutokufikirika kwa jambo linalofanyika. Lugha inaweza kuwa ngumu lakini nazungumzia pale watu wanapocheka na mmoja kusema, ‘Dah, sijui huyu jamaa alikuwa anafikiria nini.’ Au ‘Duh, sijui hawa watu huwa wanafikiria nini.’ Sifa za jambo hilo ni kuwezekana kufanyika lakini watu kikawaida huwa hawalifanyi. Hii ni njia ya uhakika ya kuchekesha ambayo nitaielezea katika nakala zijazo.
Nakala hii inakuwa ndefu na sasa nifupishe sababu mbili za mwisho zilizobaki zinazomfanya mtu acheke lakini haziwezi kutumika kuchekesha. Sababu hizi ndiyo hasa pale tunasema kujichekesha. Moja ni mtu kucheka kufuatia kukosa kile alichokuwa akikitarajia. Kwa mfano mtu aulizwapo swali gumu au aonapo dalili za kushindwa anaweza kucheka bila ya kuwepo kichekesho, kicheko chenye chembe chembe za kujibeza. Na mwisho ni mtu kucheka ama kujichekesha kuficha hisia mbaya alizokuwa nazo. Mtu anaweza kucheka atokewapo na jambo baya kama vile kutukanwa na mwenzake ili kuficha hisia za kukasirika kwake. Njia hizi mbili za mwisho ni ngumu kuzitumia katika kuchekesha.
Katika nakala ijayo katika nakala hizi za kuchekesha, tutaona umuhimu wa kujua kuchekesha..

No comments:

Post a Comment

  • Hadithi na Simulizi