Wednesday, August 12, 2015

Umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho…



Kuchekesha bila kukariri vichekesho haimaanishi kuwa na uwezo wa kutunga vichekesho vipya au kuvibadilisha vichekesho vilivyopo. Ninachojaribu kumaanisha kwa umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho ni sababu za kuchekesha bila ya kutumia vichekesho(kifungu cha kauli zenye lengo la kuchekesha.)
Miaka mingi iliyopita, nikiwa mtu ninayejali mambo ya muhimu peke yake, sikuona umuhimu wa kuchekesha wala kucheka vichekesho vya watu. Sisemi maisha yalikuwa mabaya au magumu lakini hali ya sasa ni nzuri zaidi kuliko huko nyuma. Muda ulivyokuwa ukienda mbele nilianza kuona umuhimu wa kujua kuchekesha, acha ile mara moja mara mbili ambayo mtu yeyote anaweza kuchekesha. Nilitamani kuwa na uwezo wa kuchekesha kwa haraka zaidi na mazingira magumu zaidi. Unajua nilichokifanya?
Nilianza kutembelea mitandao mbali mbali inayoandika vichekesho na kuanza kuvikariri vichekesho hivyo. Ingawa vichekesho hivyo vilikuwa kwa lugha ya kiingereza, niliweza kuvibadilisha na kuvisimulia kwa Kiswahili kwa namna ambayo ilichekesha. Kadiri siku zilivyokwenda nami nikawa nikitafuta vichekesho hivyo kwa udi na uvumba ili wale waliouona uwezo wangu wa kuchekesha wasiache kunisikia nikichekesha. Halikuwa jambo baya lakini vichekesho hivyo vikawa kama vikijirudia rudia na kuniboa. Hapo ndipo nikaona umuhimu wa kujua kuchekesha bila kukariri vichekesho.
Umuhimu hasa ni kuwa na uwezo wa kuchekesha muda wote na mahali popote. Lakini bado kuna haja ya kuzungumzia umuhimu wa kuchekesha kwa ujumla wake. Katika hali ya kawaida, faida kubwa ya kuchekesha ni kujenga na/au kuimarisha mahusiano baina ya watu. Ipo wazi kwamba watu wanaochekesha huwa na mahusiano na watu wengi zaidi kuliko wale wasiochekesha lakini ikumbukwe pia kuwa kuchekesha kila wakati huweza kufanya watu wakutoe maana, yaani uonekane mtu asiyeweza kuwa makini. Kama ni mfanyakazi, kumchekesha bosi wako kutaimarisha uhusiano wako na bosi huyo na unajuaje faida ya kuwa karibu zaidi na bosi wako kuliko wafanyakazi wengine?
Umuhimu mwingine wa kuchekesha ni kutumiwa kama ajira. Mifano hai ipo kwa wale wenye vipindi vya kuchekesha na kila stesheni, ina vipindi hivyo. Naomba nisihi kwamba kuchekesha siyo tu kutakupatia ajira ya kuchekesha, bali ajira nyingi zinazohusisha kuhudumia watu wengi basi kuchekesha kwako, kutakuongezea uwezekano wa wewe kupata ajira. Kwani hujawahi kusikia watu wakati wakitafuta mwongozaji wa sherehe wakisema, “Wee? Kuna MC huyo anaitwa Kafupi, yaani balaa kwa kuchekesha. Tumchukue huyo huyo.” Pia hujakutana na wagonjwa wanaompendelea daktari fulani kwa sababu anaongea nao vizuri? Anawachekesha?
Nimeanza na hali ya kawaida, nikafuata yenye umuhimu kidogo na sasa nizungumzie umuhimu wa kuchekesha katika hali ambayo watu wengi hushindwa kufikiria umuhimu wa kuchekesha katika mazingira hayo. Hapa ndipo hasa penye umuhimu wa kuchekesha bila ya kukariri vichekesho. Nazungumzia kuchekesha kama njia ya kukwepa hali tata upande wako. Inaweza kuwa kukwepa swali gumu kwenye mahojiano, kuinua au kubadili mkondo wa ushindi kwenye majibizano na hata kuficha ubaya unaotaka kujitokeza.
Pata picha unakwenda kwenye masaili(mahojiano) ya kazi na umeme umekatika siku hiyo. Ukaenda na shati lililojikunja sana ukiiamini elimu na ujuzi wako kuliko umaridadi wako lakini kati kati ya intavyu, mmoja wa wanaokuhoji akakuuliza, “Kwa nini umevaa shati lililojikunja sana wakati unajua unakwenda kwenye intavyu?”
Katika hali ya kawaida mtu anaweza kujaribu kutoa sababu nyingi, ‘umeme umekatika, nimeibiwa shati langu nililotayarisha, nje tu ya ofisi nimemwagiwa juisi hivyo hili siyo langu.. n.k) ambazo zinaweza kuzua maswali mengine na mwisho wa siku kuonekana mtu ambaye hukujiandaa mapema au kwa kiingereza naomba niseme, ‘careless.’(keyales). Kwa mimi ningejibu au ningeshauri mtu yeyote ili kuondoa umakini wa wale wanaokuuliza katika jambo hilo kwa namna inayofanana na jibu hili.
“Ooh, huu ni utamaduni kwetu. Bibi yangu mzaa babu aliniambia nikitaka kufanikiwa kwenye intavyu kama hizi, nisipige pasi nguo.” Kama bahati mbaya kuna mdudu kwenye nguo na umeulizwa, unaweza sema, “Ooh, kuna mtu ananitakia kila la kheri kutoka kijijini kwetu.”

Kuna kipindi nilikuwa katika masaili ya kupewa ufadhili wa masomo nao ungetegemea uwezo wangu wa kufaulu. Matokeo yangu ya mtihani wa Taifa yalikuwa mazuri lakini mfadhili hakuamini mara moja na katika kutokuamini kwake akauliza, “Lakini nasikia shuleni kwenu wasimamizi wa necta huwa wanalipwa.”
Nadhani unaweza kujua kwamba kukataa kungeleta maswali zaidi na kukubali kungeashiria nisiaminiwe kwa matokeo tu ya necta. Bila ya kutetereka nilimjibu,
“Yah, ofkoz huwa wanalipwa.” Nikavuta muda kidogo na kumalizia, “Na Necta (yaani baraza la mitihani) lakini.” Wote katika chumba walicheka na kutohoji tena kuhusu maswala hayo.
Sasa tumeona umuhimu wa kujua kuchekesha bila ya kukariri vichekesho, katika nakala ijayo tutaona hatua zinazofuatwa katika kucheka na hivyo hatua za kufuata katika kuchekesha…

No comments:

Post a Comment

  • Hadithi na Simulizi