Friday, August 14, 2015

Kusema pole siyo kazi, kazi kutoa pole… Jinsi ya kutoa pole kistaarabu.



Watanzania ni wakarimu sana, kila mtu analisifia hilo. Ni jambo la ukweli na la kupewa sifa. Hata mtoto mdogo wa kitanzania anatambua ya kuwa jambo lolote linaloonesha kuwa la kutokufurahisha linapomtokea mtu, basi jambo zuri na la kwanza kabla ya yote ni kumpatia pole mtu aliyefikwa na janga hilo. Matokeo yake ni kwamba tumekuwa kama mashine, yaani ukiona mtu anasikitika basi wewe ni … ‘pole…’ na imepita hiyo.
Sisemi tuache kusema pole kwani vipo vingi vya kurekebisha na inategemea na mtu. Wapo baadhi ya watu ambao kiukweli hupenda kusikia wakiambiwa pole na hivyo kusema pole kwao, hufanya kazi bila matatizo. Lakini linapotokea tatizo kubwa kama ugonjwa au msiba, basi lazima kuwa makini katika kutoa pole. Mfano tuchukulie swala la msiba, mtu wa kwanza kasema pole akaeleweka. Akaenda wa pili naye akaeleweka. Wa tatu, nne na kuendelea. Wewe unasikia kutoka kwa mtu na kwenda kutoa pole kama ya ishirini hivi. Je, unadhani kufika pale na kusema maneno yale yale, “Nasikia umefiwa na [ndugu] yako. Dah, jamani hivi ameondoka kweli, pole sana.” Kutamfanya mfiwa akumbuke kwamba uliguswa? Au unajisikiaje unaporudi kutoka kwenye mazishi mkoani halafu unamwambia mtu kuwa ulikwenda kuzika, halafu unachosikia ni, “Pole ndugu yangu.”? Ongeza thamani ya utu wako kwa kutoa pole kistaarabu.
Mtu aliyestaarabika, hudadisi tatizo na ukubwa wake kabla ya kutoa pole. Pole ya kistaarabu pia huambatana na maneno ya kuisindikiza yaani huvalishwa nguo. Lakini pia katika hali ya kawaida, inaweza kukulazimu kutoa pole zaidi ya moja kama mtu apokeaye pole hiyo atakuwa akisimulia mfuatano wa matatizo au matukio yanayokulazimu kumuonea huruma. La kukumbuka ni kwamba, hata ukitoa pole mia kwa mtu mmoja katika muda mmoja, ni vema pole hizo zikawa zikitofautiana usemaji au utolewaji wake.
Ushauri wangu: Jifunze kutumia kauli ya, “Pole kwa …” ukimalizia na jambo linalokufanya umuonee huruma huyo mtu. Kisha, jifunze kutokukimbilia kusema pole kwani muda mwingi inamkatisha tamaa yule anayekusimulia majanga yake. Kwa kujifunza taratibu unaweza kugundua ni muda upi muafaka wa kutoa pole wakati mtu akikusimulia matatizo yake. Lakini kama unayajua matatizo kabla ya kuambiwa na huyo mtu, pengine umesikia kutoka kwa watu, ni vema kuanza na ‘Pole kwa…’ kisha kuanza kudadisi ukubwa wa tatizo na kama suluhisho limepatikana au la. Lakini katika yote, usisahau kutoa pole mara ujuapo ukubwa wa tatizo hata kama suluhisho limeshapatikana.
Katika nakala ijayo katika mfululizo wa nakala hizi za Lugha ya Maneno tutaangalia Namna ya kupokea pole kwani Kusikia ukiambiwa pole siyo kazi, kazi kuipokea pole unayopewa.

No comments:

Post a Comment

  • Hadithi na Simulizi