Roho ya kishetani
ilikuwa ikizidi kuniingia akilini na tayari nilishakata shauri, nikashika njia
kwa haraka bila hata ya kugeuka nyuma kutoka nje ya hospitali hiyo nikijificha
nisionwe na ndugu na jamaa pale hospitali. Nilipanda gari hadi kariakoo ambako
nikachukua gari ya ubungo na kushukia magomeni Kagera ambako ndiyo nyumbani.
Niliingia ndani na kumkuta mtoto wangu Matata akiwa amejilaza kwenye malu malu
akichora chora kwenye gazeti. Aliponiona tu akaniamkia,
“Shikamoo ba mkubwa.”
Japo alikuwa ni
mwanangu wa damu, alikuwa amefanana sana na Shukuru na kutokana na baadhi ya
mambo yaliyotokea huko nyuma, mtoto huyu alijua Shukuru ndiyo baba yake. Na
wote kasoro Shukuru na mke wangu tulifanywa tudhanie hivyo.
“Marahaba. Njoo ulale
huku muda umefika wa kulala mchana.”
Nilijibu kwa sauti ya
kawaida nikijitahidi kuficha hasira zilizokuwa zimetokana na hali mbaya ya mke
wangu na kwamba zilisababishwa na mtoto huyo Matata. Mtoto ambaye nilichukua
muda kuamini ni damu yangu naye akawa akihitajika dunia nyingine. Nilijitahidi
kumzuia abaki dunia yetu ya kawaida lakini maji yalikuwa yamenifikia shingoni,
nilishindwa kuruhusu kupoteza kila kitu kwa ajili yake.
Mtoto huyo alionesha
kutokupendezewa na swala la kulala muda ule lakini kwa vile alikuwa akiniogopa,
alishindwa kubisha na kunifuata mpaka chumbani. Hiyo ilikuwa muhimu ili mimi
kuweza kukamilisha makubaliano na nguvu ambayo ilikuwa ikimuua mke wangu kwa
kuinyima almasi yake. Nguvu hiyo ndiyo ilikuwa mpinzani wangu na muda wa wote
kushinda ulikuwa umefika.
Sehemu ya moyo wangu
ilikuwa ikinikataza lakini sehemu iliyobaki ilinionesha nuru na mafanikio ya
mimi kuweka makubaliano na nguvu hiyo. Nililala chali kitandani nikijihisi mtu
katili na asiyefaa kwenye jamii. Uwoga ulikuwa ukiongezeka ndani yangu na
kunifanya nianze kumuonea huruma mtoto huyo. Ule upande wa pili nao ulikuwa
ukiniambia nisipofanya makubaliano basi nitakuwa sijawatendea haki watu wengi.
‘Lakini
kwa nini ruhusa lazima itoke kwangu?’
‘Labda
kwa vile mimi ndiyo mtoto wa kwanza wa familia yetu.’
‘Sasa
ndiyo nimtoe kafara hata mtoto wa Shukuru?’
‘Siyo
kafara, hiyo ni sadaka kwa Shukuru na msaada kwa Matata. Huku atateseka tu bora
akawaongoze huko wamtakapo’
Maswali yalinifululiza
kichwani na kujaribu kujijibu mwenyewe. Nilipofikia hapo, nikajikuta nikipata
wazo ambalo nilijua lingeweza kumaliza maamuzi yangu. Nilimgeukia Matata
aliyekuwa amefumba macho kujaribu kutafuta usingizi.
“Matata mwanangu, najua
wewe bado mdogo kuelewa hivi vitu lakini kama ni kweli basi utanielewa.
Nimejitahidi kufanya kile ambacho ndugu yeyote angekifanya lakini naogopa
ninaweza nikawa kweli nikikosea. Naomba unioneshe kama walichokisema kuhusu
wewe ni ukweli au walidanganya.”
Nilipomaliza kuongea
maneno hayo juu ya sikio la kulia la Matata, nilinyanyuka na kwenda nje ambapo
nilichukua kijiti na kuingia nacho chumbani. Kisha nikachukua peni na karatasi
na kuviweka vitu vyote pamoja, peni na kijiti vikiwa juu ya karatasi.
“Matata, chagua kitu
cha kuchorea kwenye karatasi.”
Nilimuamsha mtoto huyo
na kumuomba hivyo huku nikimuashiria kwa mikono achague kati ya peni na kijiti.
Matata alianza kufurahi akichukua kijiti na kukishikilia kwa nguvu mkononi.
Macho yalinitoka kama
mjusi aliyebanwa na mlango nisiamini nilichokiona. Hatimaye niliweza kuelewa
chanzo cha matatizo kwani maelezo ya yule mchawi yalikuwa yakijihakikisha
ukweli wake sasa. Matata tayari alishafumba macho namoyo wangu tayari ulishafanya maamuzi.
[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia
simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]
No comments:
Post a Comment