Kwa nini uhitaji au kwa nini usihitaji kubobea katika lugha
ya maneno…
Nianze kwa kukumbushia kuwa lugha ya maneno
inadhamiria kukupa ujuzi na uwezo wa kunasa baadhi ya maneno mtu asemayo kupitia
kauli zake yanayobeba dhamira halisi aliyo nayo. Pia itakusaidia kuweza
kufikisha dhamira yako namna unavyotaka bila ya kuwepo kwa makundi au tafakari
tofauti za kauli zako.
Si kwamba bila kuwa na ujuzi sahihi wa lugha ya
maneno basi hutaweza kuwaelewa watu au watu kutokuzielewa kauli zako, lakini
hii inalenga zaidi kwenye dhamira ya ndani au tafakari iliyo sahihi zaidi. Si
wote watakaohitaji ujuzi huu nawe usijisikie vibaya utakapoona kuwa haina
umuhimu kuwa nao. Kwa wewe unayeona umuhimu, ninakukaribisha sana katika safari
hii na nikuhakikishie kuwa utaanza kuona mabadiliko baada ya nakala chache tu.
Ujuzi ni kama utajiri, kama watu wote tukiwa matajiri basi neno hilo ‘utajiri’
halitakuwa na maana. Ndivyo ilivyo kwa upande wa ujuzi, kama watu wote tukijua
kwa kiwango sawa, basi ujuzi wetu hautakuwa na maana. Chaguo ni lako kupenda
kujua au kuchukia kujua.
Je, uko tayari kujua?
Vuta na kushusha pumzi, fumba macho na tafakari kwa muda.
Kumbuka kuwa tendo moja linakuwa na matokeo tofauti kwa watu tofauti. Pata
picha ametokea kichaa aliyekonda sana na kukuchanja kwa kutumia kiwembe ambacho
kinaonekana wazi kimeshatumika. Je, katika swala la Ukimwi hofu yako kubwa
itatokana na tafakari ipi kati ya hizi?
‘Bora hata nisiende kupima, nisije kujipa mawazo
kama nitakuta ninao.’
‘Bora nikapime ili nijijue afya yangu, kuliko kuishi
kwa mawazo siku zote kwa sababu sijui kama ninao au sina.’
Hivyo ndivyo watu wanavyotofautiana na hakuna namna
ya kumbadilisha mtu mawazo yake kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Kama wewe
una mawazo kama ya mwanzo katika mfano huo, basi nikutahadharishe kuwa na umakini
zaidi utakapozijaribu njia hizi. Pale unapokata shauri kuanza kuzitumia njia
hizi, basi ni kheri kujiamini na kuamini kile utakachokinasa kutoka katika
maneno yatakayotumiwa. Changamoto kubwa iliyopo katika matumizi ya lugha ya
maneno ni watu kupingana na ukweli utokanao na maneno wanayoyatumia.
Msanii mmoja katika wimbo wake aliokuwa akiwahasa
vijana wa kiume katika mahusiano, alitahadharisha akisema, ‘gusa unase…’ Siku
moja alipohojiwa maana ya maneno hayo akakiri ya kuwa maana halisi aliyokuwa
ameifikiria yeye mwenyewe, iligundulika kuwa dhaifu kwa mashabiki wake ambao
walimpa maana inayofaa kutokana na maneno yale naye akakubaliana nao.
Maneno na vitu vingine vidogo vidogo hubeba dhamira
halisi wakati kauli kwa ujumla, hubeba ujumbe ambao mtu anapenda ukufikie.
Katika mojawapo ya nakala zijazo, nitakuelezea mbinu mojawapo isemayo, ‘Sikiliza
wasichokisema, kila mtu husikia wanachokisema.’
Lakini kabla ya kujikita zaidi katika kujua dhamira
za watu kupitia nakala za pata ujumbe sahihi, nishauri watu kuanza na nakala za
staarabika na staarabisha pamoja na za toa ujumbe sahihi. Katika staarabika na
staarabisha, maneno mbali mbali yatumikayo kimazoea au vibaya, yatakuwa
yakielezewa matumizi sahihi.
Usikose nakala zinazofuata…
Staarabika na Staarabisha: Kusema pole siyo kazi,
kazi kutoa pole… pia Kusikia pole si kazi, kazi kuipokea pole.
Toa ujumbe sahihi: Unatoa taarifa au unauliza swali!
Hatutaki kusikia taarifa ya swali…
No comments:
Post a Comment