Maiti ilikuwa
ikitolewa wodini kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti. Taratibu huku
hofu ikiwa inanizidi nami nikihisi bora ya kufa kama mke wangu akifa kwa sababu
yangu nilijongea kwenye machela hiyo. Nilipoikaribia sikuweza kutembea taratibu
tena bali nilijikuta nikipiga hatua mbili za haraka na kuivamia maiti ile
nikiifunua sehemu ya kichwani. Japo mikono ya wauguzi ilijitahidi kuwahi
kunizuia kutokuifunia maiti hiyo, nilifanikiwa kuona paji la uso pamoja na
nywele. Nashukuru Mungu haikuwa maiti ya mke wangu na ahueni niliyoipata
ilinifanya nishushe pumzi kwa nguvu na moyo kuhema kama vile mtu aliyekoswa na
risasi.
Bado nikiwa
ninahema nilihisi mikono ikinishika karibu na mabega yangu na kunifanya nigeuke
nyuma. Shukuru, mama bonge, Jeni pamoja na Tumsifu walikuwa wamesimama nyuma
yangu wakinitazama kwa shauku kubwa. Shukuru ambaye ndiye alikuwa amenishika
akauliza,
"Ni
mwenyewe?"
Nikijitahidi
kutabasamu ili kuwatoa shaka, nilitikisa kichwa changu bila ya kutoa neno. Wote
waliweza kuona kuwa nimeyaelekeza macho yangu kwa yule daktari ambaye tayari
alikuwa akiondoka sasa. Shukuru ambaye muda huo alikuwa mbele yangu, aligeuka
nyuma na kuanzisha safari ya kumfuata yule daktari. Mimi ndiye nikawa nyuma
nikiwafuatia wenzangu taratibu kujipa nafasi ya kuweza kutafakari nini cha
kufanya.
Tukiwa
tunamuelekea yule daktari, Shukuru akiwa kama hatua tano kumfikia huku mama
bonge, Jeni na Tumsifu wakiwa nyuma ya Shukuru kwa kama mita nano na mimi nyuma
yao kama hatua nane, nilistushwa na sauti niliyoisikia ndani ya kichwa changu.
'Kuna haja ya wewe kuongea na daktari?'
Nilisimama
nikihisi mpinzani wangu alikuwa akijaribu kuongea na mimi japo nilijua
asingeweza kuwa yeye. Nilivyosimama sikusikia tena sauti yoyote bali sehemu ya
ubongo wangu ilikuwa ikiniambia kuwa kweli hakukuwa na sababu ya kumuona
daktari. Baada ya kukubaliana na wazo hilo nikahisi kitu kikiniambia moyoni,
'Mke wako anakufa na wewe umesimama tu kama vile hujui
cha kufanya?'
'Usiutese moyo wako, acha moyo wako ukuongoze sasa kwa
kuwa ukifuatisha ubongo wako utakuja kuumia sana moyo. Usitake watu wakuone
mwema wakati unajitengenezea madonda moyoni, upendo wako upo kwa mkeo na si kwa
Matata.'
Roho ya kishetani ilikuwa ikizidi kuniingia
akilini na tayari nilishakata shauri, nikashika njia kwa haraka bila hata ya
kugeuka nyuma kutoka nje ya hospitali hiyo nikijificha nisionwe na ndugu na
jamaa pale hospitali.
Soma nyuma.
[Nini kitafuata..? Endelea
kufuatilia simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]
No comments:
Post a Comment