Mchango wa
Hadhi(Wadhifa) katika kucheka.
Katika nakala iliyopita
kwenye mfululizo wa nakala hizi, tuliona jinsi uhusiano na hisia zilivyo na
mchango katika kumfanya mtu acheke awapo na watu fulani. Tuliona kwamba mtu
anacheka kirahisi awapo na familia yake ama kazini, yaani jinsi uimara wa
uhusiano ulivyo au hisia zilizopo ndiyo urahisi wa mtu kucheka ulivyo.
Katika nakala hii
tunageukia katika kitu kingine ambacho kina mchango mkubwa katika kumfanya mtu
acheke. Wengi tumewahi kulishuhudia hili ingawa kuna uwezekano hatukuliwekea
mkazo. Tumeona katika filamu nyingi, pale mkuu au bosi wa kikundi fulani
anapotokewa na kitu cha kuchekesha ambacho kinaweza kuwa kikimuaibisha kwa
namna moja au nyingine, wale wafuasi hucheka endapo tu mkuu wao ataanzisha au
kuruhusu wao kucheka na punde atakaponyamaza, basi nao hufuata.
Rafiki yangu mmoja
aliwahi kuniambia kauli moja, ‘Huhitaji kuwa mchekeshaji, ukishakuwa tajiri
basi watu karibu yako hujikuta wakicheka tu hata ukiongea pumba.’ Hakuwa
akikosea. Ukweli ni kwamba watu wawapo na watu wenye hadhi kubwa zaidi yao,
hujikuta katika hali ya kucheka zaidi kuliko wakiwa na watu wa hadhi ya chini
yao au hadhi sawa.
Umewahi kuona namna
watu waliokaa meza moja katika baa wanavyocheka? Au kikundi cha watu wa ofisi
moja wakicheka? Vicheko huongezeka na watu kuwa huru zaidi endapo mkuu au bosi
yupo katika kundi hilo. Mchango wa mkuu au bosi huyo katika kuwafanya watu
kucheka ni pale atakapotoa kichekesho ambacho anategemea watu wacheke au
atakapoanzisha kucheka kichekesho cha mtu mwingine.
Pia hili tunaweza
kuliona katika familia zetu na kama tunakumbuka kipindi tukiwa tunasoma.
Kichekesho hicho hicho kikitolewa na kaka au dada nyumbani kitachekesha tofauti
kama kitatolewa na mama au baba wa familia. Hivyo hivyo ndivyo ilivyo endapo
mwalimu atajaribu kutoa kichekesho kwa wanafunzi wake. Hata kama kichekesho
kitakuwa cha kawaida sana au hakichekeshi, bado wanafunzi watajikuta wakicheka.
La
kuzingatia… Kucheka uwapo na mtu mwenye hadhi zaidi
yako, ni jambo linalotakiwa kutokea bila ya kujifikiria. Kumbuka kucheka
kunatokea pale tu mtu awapo na furaha, hivyo kuonesha una furaha kuwa pamoja na
mtu huyo ni jambo la msingi. Huhitaji kujichekesha, lakini kuweka akilini
kwamba mtu uliyekaa naye ana hadhi zaidi yako na hivyo anakutendea wema kukaa
na wewe na kujaribu kukupa furaha kwa kukuchekesha, basi utajikuta ukivielewa
vichekesho vyake na kucheka bila pingamizi. Pia, unaweza kutazama namna watu wa kundi moja wanavyocheka na kutambua mkuu katika kikundi hicho.
Katika nakala ijayo;
Mchango wa matayarisho ya kucheka kabla ya kucheka…
No comments:
Post a Comment