Mwaka 2006
Majira ya saa nne
wakati jua likianza kuchoma maeneo ya Yombo-Buza katika wilaya ya Temeke, Kayumbas
anarejea nyumbani kutoka shuleni alipokuwa amekwenda kupata matokeo yake ya
mtihani wa Taifa wa darasa la nne. Uso wake umetandwa na furaha na anamkuta
mama yake akitwanga kisamvu nje ya nyumba waliyopanga.
Nyumba hiyo iliyojengwa
maalumu kwa kupangisha imejificha kutoka barabarani nayo ina vyumba kumi na
mbili, vinne vikiwa uwani mwa nyumba kubwa. Imechukua wapangaji wa familia tatu
tofauti, akina Kayumbas wakiwa familia mojawapo.
Kwa mbali kidogo kutoka
alipo mama yake, yupo mdogo wake aitwaye Mjanja
akipiga mswaki. Huku akishangilia, Kayumbas anamkimbilia mama yake na
anapomfikia wanakumbatiana.
"Mana oko,
imekuwaje huko?"
"Nimefaulu mama kuingia
daratha la tano."
"Mbuta!
Mana oko umefaulu kweli unatania?"
"Kweli mama
nimefaulu."
Mama Kayumbas anambusu
mwanawe huyo kwenye paji la uso akimshika kichwa kwa mikono yote miwili.
Anamuachia na kunyoosha mikono juu kumshukuru Mungu.
"Aika Iruwa."
Mdogo mtu anafanya haraka na kumaliza kupiga
mswaki kabla ya kuwakimbilia mama na kaka yake na kuwauliza,
"Kuna nini?"
Kayumbas anamtazama
mdogo wake usoni huku akitabasamu kidogo na kisha kumrudia kumuangalia mama
yake anayempapasa Mjanja kichwani. Mjanja naye anamkumbatia mama yake kiunoni
na kuegemeza kichwa chake kwenye sehemu ya mapaja ya mama yake.
"Kaka yako
amefaulu mtihani Mjanja."
Mama Kayumbas anamjibu Mjanja
sababu ya furaha yao na hapo hapo Mjanja anamuachia mama yake na kuanza kuruka
ruka akishangilia,
"eeeeh eeeh eeh.
Kaka amefaulu."
Kayumbas na mama yake
wanacheka namna Mjanja anavyoshangilia kana kwamba anafahamu vema maana ya
kufaulu. Kisha mama Kayumbas anamwambia mwanawe,
"Mana oko, na
imani yangu kwa Iruwa idhihirishwe kupitia kwako. Naamini Iruwa atakuongoza
mpaka siku ya mwisho nawe utafaulu vema, nasi wazazi wako tupo kukusaidia
kuyafikia malengo yake kwako. Chochote utakachohitaji mana oko, usisite
kutuambia. Tutakupatia kila utakacho usije ukaanguka.'
Kayumbas anamjibu mama
yake, "Thawa mama nimekuelewa, nitakuja kufaulu tu."
Mama Kayumbas baada ya
kuisikia kauli hiyo kutoka kwa mwanawe, anarudi nyuma kidogo na kumuangalia juu
mpaka chini kama anayemtathmini na huku akitabasamu, anamsogelea tena na
kumuwekea mikono mabegani akisema,
"Mana oko leo
nakuchinjia kuku, umenifurahisha sana. Soma mana oko kwa bidii, yani mi nataka mana
oko usije ukaishi maisha haya tunayoishi sisi. Kufanikiwa kwako ndiyo mwongozo
kwa wadogo zako. Yani, hebu muangalie baba yako, hana hata heshima hapa mtaani
unadhani kwa nini?"
Kayumbas anatingisha
kichwa chake huku akisema,
"Hamna thifahamu
mama."
Jibu hilo linamfanya mama yake amalizie,
"Pesa hizo mana oko, baba yako hana pesa
za kumpatia heshima hapa. Hivyo mana oko wewe soma uje upate kazi nzuri na
uishi maisha mazuri ya kuheshimika."
"Mama, mimi
nitathoma hadi nimalize madaratha yote."
"Mana oko, si
unajua elimu ni bahari lakini? Sio lazima mpaka uzeekee shuleni, wewe ukifika
zako chuo tu inatosha. Utaishi vizuri tu."
"Thawa mama lakini
mimi nataka nithome kila kinachothomeka hata nikimaliza chuo kikuu."
"Hapo umenena mana
oko, na uwe rafiki na walimu wako ili wakuongoze vizuri, usije ukamchukia
mwalimu wako hata akufanye nini."
"Thawa mama."
"Haya nenda
uendelee na shughuli zako mana oko."
[Endelea kufuatilia simulizi hili litokanalo na matukio ya kweli...]
No comments:
Post a Comment