'Triiiii triii triiii triiii triiii...'
Ni mara ya tatu simu ilikuwa ikiita na kunisumbua
usiku huo wa saa tano ambao nilikuwa nimechoka sana kwa kufanya kazi masaa
ishirini na nane mfululizo. Nilipanga nilale kama gogo usiku huo lakini simu
hii ilikuwa ikininyima raha bila ya
kujua nani aliyekuwa akipiga. Kabla ya kujua nini cha kufanya kuhusu simu hiyo,
mwenzangu niliyelala naye akanitingisha, "......"
Akaniita jina
fulani la kipekee nisilopenda wengine walichukue na kuniambia, "Kuna mtu
anasumbua kwenye simu yako."
Sauti hiyo ambayo siku zote napenda kuisikia, ikanifanya
ninyooshe mkono wangu na kuichukua simu.
"Haloo mkuu wangu, samahani kwa kuchelewa
kupokea." Ni simu ya rafiki yangu mkubwa kwenye maswala ya kikazi. Na
nilipoiona tu kuwa ni simu yake nikaelewa ni jambo muhimu.
"Sikutakiwa nikupigie mida hii Kenny, najua
utakuwa umepumzika lakini iko hivi bwana, imetokea tena Kenny na nilivyosikia
tu sikutaka kuchelewa kukupa taarifa."
"Imetokea tena, nini hiyo? Leo sijaangalia
taarifa ya habari."
"Ohooo Kenny? Inawezekanaje, ndiyo kipindi
hiki. Kuna habari uliikosa mwaka jana kipindi kama hiki, yametokea tena. Wahi
kuangalia kesho asubuhi kabla hujachelewa tena."
Akakata simu na kunifanya nikurupuke pale kitandani.
Sikuweza kusubiria asubuhi na hivyo kukimbilia runinga muda huo huo. Nikakuta
watu wakihojiwa hojiwa juu ya tukio moja kubwa ambalo sikulijua mara moja. Kati
ya waliohojiwa, hawa walikuwa na mambo muhimu sana.
Mama
yake: "Wamenipotezea
mwanangu hawa. Sijui ni mzimu gani unaoiwinda familia yangu lakini nina uhakika
hakufeli hivi hivi. Kuna mtu alichezea akili ya mwanangu lakini yeye mwenyewe
hakujua. Mwanangu alisoma kwa shida sana lakini kamwe hakuchoka kusoma. Wote
tulitegemea angefaulu kwa alama za juu lakini nashangaa kusikia eti amefeli....
Ndiyo, ameacha barua mbili, moja ya kwangu na nyingine amesema nimpe Mashoto...
Aseme nini zaidi ya kujilaumu na kunilaumu, lakini siwezi kusema sana kwa kiasi
fulani labda nilichangia."
Mjanja(mdogo
wake): "Kaka
ametukimbia na tutammis siku zote kwa sababu tulimtegemea aje kuwa baba wa
familia. Alikuwa kati ya watu wanaojipigia mstari na kuufuata mstari huo
wasijali pembeni kunatokea nini. Nilimpenda sana kaka yangu lakini sijui upande
wake... Ndiyo, mimi nilikuwa wa kwanza kuacha shule na kaka alinichukia sana
kwa sababu hiyo. Alitaka nisome, nakumbuka alivyokuwa akinipeleka shule utotoni
lakini.... Hapana, alikuwa tayari kuanza kufanya kazi zetu hizi zisizohitaji
elimu lakini nafikiri ni ile hali ya kuzidharau kazi hizi."
Mwalimu
wake: "Sijawahi
kufundisha mwanafunzi bora kama yeye. Hata kipindi mimi nasoma sikuwahi kumuona
kama yeye. Alikuwa na determination(malengo), alijua nini afanye kufikia
malengo yake na kikubwa zaidi, alimpenda kila mmoja. Alitaka anavyofanikiwa
yeye basi kila mmoja naye afanikiwe.... Yah, siwezi kuhesabu ni mara ngapi
aliwahi kunifuata akitaka nimsaidie ushauri lakini nilichokigundua ni kwamba
kulikuwa na ugumu sana kumshauri kinyume na malengo yake. Alijiamini kupita kiasi...
Hapana baada ya matokeo kutoka niliongea naye na kumuambia kwamba bado ana
nafasi, niliamini kwa moyo wake asingekata tamaa. Nilijitahidi kumpa moyo na kumsifia
kwa makubwa ya kukumbukwa aliyowahi kuyafanya lakini hakuwahi kutosheka...
Alitaka kila kitu na angepata kama angeendelea kuvumilia kidogo ."
Habisai(Mwanafunzi,
rafiki mkubwa): "Alikuwa
rafiki yangu mkubwa kuliko wote niliowahi kuwa nao maishani. Alikuwa akimjali
kila mtu na hata nilipokuwa nikijaribu kumshauri afuate mambo yake ili
afanikiwe zaidi yeye aliendelea kupigania yake na ya wengine.... Hamna,
isipokuwa tu kwamba hakuwa mtu wa kushaurika. Kwa nilivyomjua, mtu pekee
aliyekuwa na uwezo wa kumshauri akaeleweka alikuwa ni mama yake lakini si sisi
wanafunzi wala mwalimu.... Ndiyo ninayo, inabidi niipeleke kwa mwalimu lakini
siwezi kuitoa barua hiyo hapa."
Nansisca(Rafiki
wa karibu wa kike): "Mimi
hata sijielewi, najiuliza kama nimlilie yeye au nijililie mwenyewe. Nilimpenda
na naamini na yeye alinipenda pia lakini aliamua kunitesa. Hakutaka kunipa
uhakika kwamba ananipenda.... Siwezi kumchukia lakini kama nisingejuana naye
nina uhakika nisingefeli hivi.... Hapana, Rugame ndiye aliyekuwa akimkosesha
raha na nadhani hata hili tukio, anaweza akawa amemsumbua sumbua sana kwa vile
walishawahi kuahidiana hapo kabla kuhusu haya. "
Rugame(mwanafunzi
mwenzake): "Inaniuma
sana, siyo kwa sababu wenzangu wote wananitazama kwa jicho baya kwamba mimi
ndiyo nimesababisha lakini inaniuma. Alikuwa ni mshindani wangu, katika
kufanikiwa lazima kuwe na ushindani lakini kinachoniuma ni kwamba mwenzangu
alimaanisha kile alichokisema. Mimi nilidhani ni kuwekeana chachu tu ya
ushindani, kwamba hakuna ambaye angefanya aliyokuwa akisema... Ndiyo na
inaniuma sana kwa sababu jana tu nilikutana naye na kumuambia ukweli kwamba
ujinga wote tuliokuwa tumeongea mbele za watu na ahadi zote za kijinga kwamba
tusifanye na alinielewa hata kwa mara ya kwanza tukakumbatiana lakini nashangaa
leo amefanya hivi."
Mwanafunzi
mwenzake: "Sikuwa
karibu naye lakini najua wote darasani tulimpenda. Alikuwa kiongozi bora wa
kuigwa... Kila alichokifanya kilikuwa na mafanikio. Wengi hatukuwa wa kufaulu
hata kidogo lakini alituwezesha kupata japo 'D' moja. Kwa kweli nitamkumbuka
sana."
Nilijiuliza mhusika ni nani huyo na kuanza
kuifuatilia kiundani habari hiyo. Jina lake ni Kayumbas Mirambo na ameishi
maisha waliyoishi watu wakubwa waliofanikiwa duniani na niliposikia habari zake,
naona kwamba kila kitu kilichomfanya awe Kayumbas shujaa, mwanzo wake ni pale
alipofaulu darasa la nne kwenda la tano. Ulikuwa mwanzo wa mikakati yake,
mwanzo wa matumaini yake, mwanzo wa ushujaa wake na ndiyo mwanzo wa simulizi
langu hili.
[Endelea kufuatilia simulizi hili litokanalo na matukio ya kweli...]
No comments:
Post a Comment