Mchango wa Uhusiano na
Hisia katika kucheka.
Nakubali kwamba kucheka
ni jambo zuri lakini kucheka bila sababu za msingi ni kutokujielewa. Kuna mambo
mengi yanayoingiliana na kupelekea mtu kucheka na vinapokosekana vingi vya vitu
hivyo lakini bado mtu akaonekana akicheka, basi huyo atakuwa hajielewi na kuwa
akijichekesha. Wengi wanadhani kwamba kucheka ni matokeo ya kueleweka kwa
kichekesho na kutokufahamu kwamba kichekesho ni sehemu ndogo tu na inayokuja
kwenye hatua za mwisho mwisho kati ya mambo ya msingi ya kusababisha kicheko.
Katika mfululizo wa
nakala hizi, lengo ni kuainisha sababu za msingi za kicheko ili kuongeza ama
kupunguza wastani wako wa kucheka. Usicheke kwa nadra wala usicheke daima,
cheka kwa wastani. Msemo usemao kucheka kunaongeza siku za kuishi, usikufanye
utake kucheka kila dakika na kuondoa maana halisi ya kicheko.
Jambo la msingi kama si
lenye ushawishi mkubwa la kutambua kuhusu kucheka ni kwamba kucheka ni tendo
linalohusisha sana hisia kabla ya kitu chochote. Hisia hupelekea kuwepo kwa
uhusiano baina ya watu wasiojuana lakini pia ni matokeo ya uhusiano baina ya
watu wa familia moja ama ndugu ama majirani, yaani watu waliolazimika kuwa
pamoja na kujuana.
Ni rahisi na jambo la
kawaida kucheka unapokuwa na mtu mwenye uhusiano naye hata kwa jambo ambalo
kiukweli si kichekesho. Watu wengi hucheka zaidi wakiwa nyumbani, kisha kazini
kuliko wawapo njiani au kwa watu wasiowajua. Wewe ni shahidi yangu katika hilo.
Kama hutaki hilo, na hili je? ‘Katika kundi la watu wengi waliotawanyika, watu
watakaokuwa wakicheka zaidi kwenye mazungumzo yao ni wale wenye uhusiano wa
kimapenzi kuliko wenye uhusiano wa namna nyingine na mwisho ni kwa wale
wasiojuana kabisa.’
Kumbuka kuwa hata kwa
wachekeshaji, ni rahisi mtu kucheka kwa yule mchekeshaji ambaye amejiwekea
hisia kuwa ni mchekeshaji mzuri kuliko kwa wale ambao bado hajajua uwezo wao wa
kuchekesha(hana hisia zozote juu yao) au anaowajua kama wasio na uwezo wa
kuchekesha(ana hisia mbaya juu yao). Yaani ni kwamba mtu hucheka kirahisi kwa
mchekeshaji ambaye kuna uhusiano uliojificha kwamba huyu ni mchekeshaji na
mimi ni mchekeshwaji wake.
La
kuzingatia… Unaweza kutumia kicheko chako au cha
mtu mwingine kwako(ipo zaidi kwenye nakala zangu za kuchekesha) kupima hali au maendeleo ya uhusiano
wenu. Pia waweza kutumia kucheka ili kuongeza nguvu ya uhusiano wako na mtu
mwingine (lakini epuka kujichekesha). Katika nakala zangu za kuchekesha, utaweza
kujifunza namna ya kujijengea uwezo huo wa kucheka kwa watu unaotaka kuongeza
uhusiano nao bila ya kujichekesha.
Katika nakala ijayo;
mchango wa hadhi(wadhifa) katika kucheka.
No comments:
Post a Comment