Thursday, August 20, 2015

Roho ya Kayumbas: Sehemu ya 4



"Eee enhee, kwa hiyo uuu..uu..umekuwa wa ngapi shuleni?"
"Nimekuwa wa thaba."
"Iii..itabidi ni..ni..nikupe zawadi. Iii..iii..ikifika Jumaa..mosi  ni..ni..nikumbushe ni..ni..nikupe hela uu..uu..uende na mmm..mmama mm..m..mkanunue nguo."
"Na mimi baba."....... "Na mimiiii, nataka nguo mpya."
Wadogo zake Kayumbas: Mjanja na Majaliwa wanaingilia na mama yake huku akinyanyuka kwenda kumuwekea chakula mumewe anasema kiutani.
"Mwenzangu kazi unayo. Wao wanataka tu nguo mpya wakati hawajui mwenzao hajapata hivi hivi tu, amefanya kazi kubwa."
Mara Mjanja anaanza kulia na baba mtu anamnyanyua na kuanza kumbembeleza akisema,
"Wote humu mmm..mmm..mtapata nguo mmmpya. Hata mm..mimi ha..ha..hata mm..mmama yenu a..a..atapata nguo mmmpya. Uu..uu..umesikia Mja? Au..au..au mmmama yeye aaa..a..asipate?"
Mjanja anaitikia kwa kichwa na kuwafanya wote pale ndani wacheke wakati huo mama Kayumbas akimaliza kuweka chakula kwa ajili ya baba Kayumbas na kummiminia maji ili anawe. Kabla ya kuanza kula, anauliza
"Mm..mm..mmama Ka, ndo uu..uu..umemchinjia mmmwanao kuku?"
"Ndiyo baba Kayumbas. Nimeona nimpongeze mwanangu."
"Eeee vi..zuri." Baba Kayumbas anawageukia wadogo zake Kayumbas na kuwauliza,
"Jenni, Mmmja na Mmmawa si mmm..mm..mnamuona ka..ka yenu aaa...aa..aanavyojitahidi? Na..na..na nyie mmm..mm..mtafaulu mmkifika darasa la n..ne?"
"Mimi nitafaulu baba." "Hata mimi mwenyewe nitafaulu." Anajibu Jennifer akifuatiwa na Majaliwa.
"Yasije kuwa ni maneno tu wana oko. Ndiyo msome kama kaka yenu." Mama yao anakuwa ameingilia mama yao.
"Na mimi nataka niende shule." Anapaza sauti Mjanja ili aweze kusikika zaidi ya dada na kaka zake waliokuwa wakijimjibu baba yao.
"Utaenda tu mwanangu, Majaliwa akiingia tu darasa la kwanza na wewe unaanza chekechea." Anajibu mama Kayumbas.
"Eeeh eeeh naanza shule." Anashangilia Mjanja asijali kama ni usiku na hapo baba yake anamkemea,
"Aaa..a..acha kelele sasa, uu..uuusiku huu."
Wanaendelea na mazungumzo ya kawaida mpaka wanapokwenda kulala.

Kesho yake asubuhi wanapoamka, pilika pilika zinaanza kama kawaida. Mapema asubuhi Kayumbas na Jennifer wanakwenda kuchota maji kwenye nyumba moja iliyopo mtaa wa pili wa ule wakaao. Wanawahi mapema sana na kuanza kugonga geti ili wafunguliwe maji.
"Na nyie? Kila siku mnakuja asubuhi asubuhi ka wanga? Mnatusumbua bwana, sisi bado tumelala." Kayumbas na Jennifer wanakaa kimya kwani haikuwa mara ya kwanza kuambiwa hivyo na watu wa nyumba hiyo. Wanamsikiliza anavyolalamika mtu huyo huku akiwafungulia geti.
"Kwa nini msiwe mnakuja wakati jua limeshachomoza?" Anauliza mfanyakazi wa ndani wa nyumba hiyo aliyekuwa mwanamke mnene mnene wa miaka inayocheza karibu na ishirini hivi.
"Si kunakuwa na foleni muda huo?" Anajibu Jennifer kwa kujiamini.
"Si mtasubiria, mbona wenzenu wanasubiria?" Anajibu akionesha kukerwa na swali la Jennifer.
"Tutachelewa shule thatha." Anajibu Kayumbas huku akilisogelea bomba na kuweka ndoo yake kwa ajili ya kujaza maji.
"Basi muwe mnachota usiku mkalala na maji."
"Aah sisi tumezoea kuchota asubuhi, usiku tunakuwa tumechoka na kazi zingine." Anajibu Jennifer.
"Aya shauri yenu. Siku mtajikuta mkichoma mahindi hapa mpaka saa moja ndo mkafunguliwa."
Hawasemi neno tena na kuchota maji. Wanarudia tena na kisha Kayumbas kumalizia ndoo yake ya tatu wakati Jennifer akiishia kuchota ndoo mbili.
Baada ya kumaliza kuchota maji, Jennifer anafagia ndani na nje ya nyumba wakati Kayumbas akikimbia kwa baiskeli kwenda kununua mboga mboga kwa ajili ya biashara ya mama yake kutoka kwenye mashamba madogo madogo mbali kidogo kutoka wanapoishi ambapo magari hayawezi kufika. Mama yao anaosha vyombo na kuanza kupika chapati kwa ajili ya kuziuza.
Jennifer anapomaliza, anapika chai kabisa na hata Kayumbas anaporudi, wanafunzi hao watatu yaani Kayumbas, Jennifer na Majaliwa wanaoga kwa ajili ya kwenda shule. Wanakunywa chai na wanapokuwa tayari, mama yao anawapa Kayumbas na Jennifer nauli na shilingi mia kila mmoja kwa ajili ya kutumia huku akimpa Majaliwa shilingi hamsini kwa ajili hiyo hiyo ya kutumia.
Bila ya kusahau fagio zao isipokuwa kwa Majaliwa, wanamuaga mama yao na kwenda zao shule. Jenifer anakwenda kupanda gari kituo cha nyumbani kwao, umbali wa kama mita mia mbili hivi lakini Kayumbas inabidi ampeleke Majaliwa shule kwanza umbali wa kama mita mia tatu hivi na ndipo apande gari la kwenda shuleni kwake.

[Endelea kufuatilia simulizi hili litokanalo na matukio ya kweli...]

Tuesday, August 18, 2015

Lessons from movies

Don't miss my next lessons from these movies: 
·        Focus(2015) 
·        Good People(2014)
·        Final Girl(2014)
·        Reclaim(2014)

Know the single sentence that when it's said, it proves that the woman should be avoided. The type of women to avoid from Focus.

Know how best you can make your request work on someone who was completely disagreeing with you. The lesson from Good People(2014)

Know how to set up the safe and secured environment for someone to tell you their dark secrets. The lesson from Final Girl(2014)

Know how being GOOD is good and help your life being spared. Lesson from Reclaim(2014)

Friday, August 14, 2015

Kusema pole siyo kazi, kazi kutoa pole… Jinsi ya kutoa pole kistaarabu.



Watanzania ni wakarimu sana, kila mtu analisifia hilo. Ni jambo la ukweli na la kupewa sifa. Hata mtoto mdogo wa kitanzania anatambua ya kuwa jambo lolote linaloonesha kuwa la kutokufurahisha linapomtokea mtu, basi jambo zuri na la kwanza kabla ya yote ni kumpatia pole mtu aliyefikwa na janga hilo. Matokeo yake ni kwamba tumekuwa kama mashine, yaani ukiona mtu anasikitika basi wewe ni … ‘pole…’ na imepita hiyo.
Sisemi tuache kusema pole kwani vipo vingi vya kurekebisha na inategemea na mtu. Wapo baadhi ya watu ambao kiukweli hupenda kusikia wakiambiwa pole na hivyo kusema pole kwao, hufanya kazi bila matatizo. Lakini linapotokea tatizo kubwa kama ugonjwa au msiba, basi lazima kuwa makini katika kutoa pole. Mfano tuchukulie swala la msiba, mtu wa kwanza kasema pole akaeleweka. Akaenda wa pili naye akaeleweka. Wa tatu, nne na kuendelea. Wewe unasikia kutoka kwa mtu na kwenda kutoa pole kama ya ishirini hivi. Je, unadhani kufika pale na kusema maneno yale yale, “Nasikia umefiwa na [ndugu] yako. Dah, jamani hivi ameondoka kweli, pole sana.” Kutamfanya mfiwa akumbuke kwamba uliguswa? Au unajisikiaje unaporudi kutoka kwenye mazishi mkoani halafu unamwambia mtu kuwa ulikwenda kuzika, halafu unachosikia ni, “Pole ndugu yangu.”? Ongeza thamani ya utu wako kwa kutoa pole kistaarabu.
Mtu aliyestaarabika, hudadisi tatizo na ukubwa wake kabla ya kutoa pole. Pole ya kistaarabu pia huambatana na maneno ya kuisindikiza yaani huvalishwa nguo. Lakini pia katika hali ya kawaida, inaweza kukulazimu kutoa pole zaidi ya moja kama mtu apokeaye pole hiyo atakuwa akisimulia mfuatano wa matatizo au matukio yanayokulazimu kumuonea huruma. La kukumbuka ni kwamba, hata ukitoa pole mia kwa mtu mmoja katika muda mmoja, ni vema pole hizo zikawa zikitofautiana usemaji au utolewaji wake.
Ushauri wangu: Jifunze kutumia kauli ya, “Pole kwa …” ukimalizia na jambo linalokufanya umuonee huruma huyo mtu. Kisha, jifunze kutokukimbilia kusema pole kwani muda mwingi inamkatisha tamaa yule anayekusimulia majanga yake. Kwa kujifunza taratibu unaweza kugundua ni muda upi muafaka wa kutoa pole wakati mtu akikusimulia matatizo yake. Lakini kama unayajua matatizo kabla ya kuambiwa na huyo mtu, pengine umesikia kutoka kwa watu, ni vema kuanza na ‘Pole kwa…’ kisha kuanza kudadisi ukubwa wa tatizo na kama suluhisho limepatikana au la. Lakini katika yote, usisahau kutoa pole mara ujuapo ukubwa wa tatizo hata kama suluhisho limeshapatikana.
Katika nakala ijayo katika mfululizo wa nakala hizi za Lugha ya Maneno tutaangalia Namna ya kupokea pole kwani Kusikia ukiambiwa pole siyo kazi, kazi kuipokea pole unayopewa.

Thursday, August 13, 2015

Hatua za kufuata katika kuchekesha… Njia maridadi ya kutoa kichekesho

Kabla sijazungumzia hatua za kufuata katika kuchekesha, ningependa kugusia hatua ambazo mtu hufuata wakati wa kucheka. Si mara zote hatua hizi hufuatwa zote na si mara zote hatua hizi hufuatwa kimpangilio. Lakini, izingatiwe kwamba zaidi ya asilimia themanini wakati wa kucheka, hatua hizi hufuatwa.
Mara nyingi katika kucheka, huanza kwa matayarisho au utayari wa kucheka. Ni mara chache sana mtu hucheka bila ya kuwa ametayarishwa ingawa vichekesho visivyopitia mtu kutayarishwa ndivyo husababisha kuchekesha zaidi. Kwa kupitia utayari huo, kucheka kunaweza kutokea kwa namna mbili. Kwanza na mara nyingi ni pale mtu anapotayarishwa naye kujua tukio linalofuata linahusisha kucheka. Mfano, watu wengi hupenda kusema, “Ngoja, nikuchekeshe bwana…” au misemo inayoendana na huo. Mfano mwingine ni pale mtu anaposoma kichekesho kwenye simu yake na kuanza kucheka akijua unamuona. Kisha mtu huyo bila ya kupoteza muda, pengine bado akicheka anamuonesha kichekesho hicho mtu mwingine. Kwa namna hii, mtu anakuwa ametayarishwa kwa kucheka wazi wazi. Pili, ni pale mtu anapotayarishwa bila ya kuwa na uhakika kama kauli zitahusisha kuchekesha au hapana. Utayarishaji huu wa pili, ndio wenye nguvu zaidi katika kuchekesha. Mtu huhisi kitu fulani cha kuchekesha kwamba kitatokea bila ya kuwa na uhakika Kisha kitu hicho kinapokuwa kweli, ndipo mtu anajikuta katika hali ya kucheka.
Hatua ya pili katika kucheka ni kusikia au kuona ama kusoma kichekesho. Hapa mtu husikia kauli au mfuatano wa sentensi wenye lengo la kuchekesha. Sina haja ya kuelezea maana ya kichekesho au namna vichekesho vilivyo kwani naamini hata mtoto atakayezaliwa kesho anajua maana ya kichekesho.
Hatua ya tatu katika kucheka ni mtu kukihusisha kichekesho na sehemu ya ubongo wake itakayokitafakari kichekesho kile na kujenga uhusiano na picha fulani kichwani mwake. Mchekeshwaji hujaribu kutafuta uhusiano baina ya kichekesho na matukio yaliyowahi kutokea huko nyuma ama matukio aliyowahi kuyasikia na kuyajengea picha kichwani au kujenga picha fulani kichwani akitumia wahusika na mandhari anayoitambua vema. Yaani kujaribu kupata picha mtu anayemjua au mahali anapopajua panatokea kilichoelezwa kwenye kichekesho hicho.
Hatua ya mwisho katika kucheka, yaani kucheka kwenyewe kunategemea sana na hatua ya nyuma yake. Kama mtu ataweza kujenga picha fulani au kukumbuka picha fulani inayoendana na kichekesho kwa kutumia wahusika na mandhari aijuayo vema, basi mtu huyu lazima atacheka.

Hatua za kufuata katika kuchekesha…
Baada ya kuelewa hatua zinazofuatwa mara nyingi katika kucheka, ni vema kuzingatia hatua hizo katika kuchekesha pia. Yaani ili kujihakikishia kwamba kichekesho chako hakipotei bure, ni vizuri kama utafuata hatua za kucheka ili kuchekesha.
Katika kumtayarisha mtu kwa kucheka, ni busara kuanza kufanyia mazoezi kumtayarisha mtu bila kumuweka wazi kwamba una nia ya kuchekesha. Baadhi ya watu husema kwamba Tanzania hatuna watu wenye uwezo wa kuchekesha lakini nikitathmini, naona kwamba kinachokosekana ni utayari wa watu kucheka na pengine ni kufeli katika kuwatayarisha watu kucheka. Njia nzuri ya kutayarisha watu kucheka ni kuruka hatua ya kutoa kichekesho na kumpa mlengwa muda wa kutengeneza picha kuhusu maelezo. Yaani kumfanya mtu aende hatua ya tatu hapo juu kabla ya kupita ya pili na kisha kuendelea na kichekesho. Ndiyo, wachekeshaji wengi hasa wale wafanyao ana kwa ana mbele za watu, hutumia njia hiyo ya kutayarisha.
Umewahi kusikia mtu akiuliza, “Niseme nisiseme?” na baada ya hapo kauli inayofuata inavunja watu mbavu? Hapo, mtu hufanya watu kujenga picha mbali mbali na kwa namna moja ama nyingine kuweka uwezekano wa kutokea kichekesho. Hivi karibuni, niliona njia hiyo ikitumiwa na Mhe. Mbowe akitoa hotuba baada ya Mhe. Lowassa kuchukua kadi. Baada ya kuongea mengi, alisema
“Katika ujio huu, kuna mtu mmoja ningependa kumshukuru sana.” Akakaa kimya na kuuliza, “Niseme nisiseme?” Bila shaka alijua alichokuwa akikifanya kwani baada ya kuambiwa aseme(jambo lililokuwa halihitaji kuuliza), Mhe. Mbowe akasema anamshukuru Mhe. Rais na kuweza kuangusha vicheko kwa wanaukawa.
Ukimaliza kumtayarisha mlengwa kwa kucheka, kinachofuata ni kutoa kichekesho kwa namna inayotoa muda mtu kuhusisha kichekesho na ile picha aliyoijenga kichwani. Yaani usikimbilie kusema kichekesho chako mwanzo mpaka mwisho bila kuwa na vituo vya kumpa mtu muda wa kubashiri mwisho wa maelezo yako kabla hujamaliza.
Kimsingi hizo ndizo hatua za kufuata katika kuchekesha. Si nyingi lakini umakini na mazoezi vinahitajika kabla ya vitu uwezo huo wa kuchekesha kukaa kwenye damu.
Katika nakala ijayo, tutaangalia namna ya kuvitumia vichekesho ulivyoviona kwa ajili ya kuchekesha. Hii ni changamoto kwa wengi lakini uvumbuzi unakuja hapa.


  • Hadithi na Simulizi