Bia pamoja na mziki wa taratibu uliokuwa ukipigwa
kwenye baa hiyo vilinisaidia kupoteza muda na mawazo lakini kabla ya kufikia
hali ya kutokujitambua, nilipata wazo la kwenda kuwafukuza wote wawili pale
nyumbani. Niliondoka kwenye baa hiyo nikijiongelea na kujisikitikia mwenyewe
hadi nilipofika nyumbani. Niliwakuta Shukuru na Lilian wakiwa wameshawasili
pamoja na yule mdogo wake mke wangu, Jeni. Pia palikuwa na ndugu zake
wengine mke wangu pamoja na baadhi ya
majirani na kufanya sebule ionekane haitoshi. Idadi kubwa ya wageni pale
nyumbani ilinifanya niigize kana kwamba hakukuwa na tatizo kwani niliamini
hakukuwa na mtu mwingine aliyegundua kwa sababu walimuona mtoto kwa mbali tu
tena wale wachache waliolazimisha kumchungulia chumbani alikolazwa yule mtoto.
Nilipokea hongera zote nilizokuwa nikipewa na wageni
nami pamoja na mke wangu tulikuwa tukiungana nao kumshukuru Mungu kwa kutujalia
kupata mtoto lakini moyoni mwangu nilikuwa nikitafuta muda wa kuweza kuyamaliza
matatizo yangu. Wakati wageni wakiendelea kufika mmoja mmoja, mdogo wangu
aliniita kwa upole tuweze kutoka nje. Nikijua alichotaka kunieleza na kwa vile nilikuwa nikiutaka mwanya huo,
nilimfuata kwa haraka nasi tukaenda mpaka chumbani kwake.
"Kaka, inabidi tu kumshukuru Mungu kwa yote
anayokujalia. Kwanza mkeo kushika mimba muda wote hata akajifungua salama ni
jambo la kushukuru sana maana si wote wanaofanikiwa kufikia hapo. Najua
kibinadamu hakuna aliyetegemea ulemavu lakini yote hiyo ni mipango ya Mungu,
hakunala kufanya zaidi tu ya kumshukuru yeye."
Sikuamini kama wazo kubwa la mdogo wangu halikuwa
kwenye kufanana sura na mwanangu bali ulemavu wake. Baada ya kumaliza kauli
yake, sikuwa na hamu ya kujibu chochote nami niliishia tu kumtazama usoni
nikishindwa kummaliza hadi aliponiuliza,
"Vipi kwani kaka, mbona hivyo?"
"Umemuona sura yule mtoto?"
Kwa mshangao mkubwa, akanijibu
"Ndiyo, kwani ina kasoro? Afu amekuchukua sura
yako kabisa akaiacha ya mama yake."
Ilipita kama dakika moja nikiitafakari kauli yake
kichwani huku sehemu zingine za mwili zikikusanya nguvu na baada ya kukusanya
nguvu za kutosha, nilijikuta nikisimama na kumvamia mdogo wangu huku nikimkunja
shingoni na kwa hasira nikafoka,
"Umewezaje kunisaliti Shukuru? Yani umesema
unakaa kwa shughuli zako kumbe nia yako ni kutembea na mke wangu?
Umewe..."
"Kaka, mimi nimetembea na mke wako?"
"Unaniuliza mimi! Mtoto amewaumbua huyu."
"Mungu wangu, yaani Baraka umefikia kunifikiria
hivyo mimi? Mimi siwezi ..."
Ilimbidi asimame maana kulikuwa na hodi mlangoni
kwake na alipofungua ndugu mmoja wa mke wangu alitutaarifu kuwa chai ilikuwa
ipo tayari. Baada tu ya kuurudishia mlango, Shukuru akaniambia,
"Siwezi nikatembea na mke wako Baraka. Kama
unaona sura inafanana zaidi na mimi ni upofu wako tu maana hata mimi na wewe
tunafanana."
Sikutaka kuendeleza mazungumzo yaliyokuwa hayana
dalili za kufikia mwisho na kwa vile nilitaka niende kazini, nikaenda hadi
mlangoni alipokuwa amesimama na huku nikitazamana naye usoni nikamwambia,
"Ukweli nitaujua tu Shukuru na niamini mimi,
utajuta milele ikiwa kweli."
Nilipoingia ndani ya nyumba yetu nilikwenda kwenye
chumba cha kulia chakula na kupata kifungua kinywa. Kwa vile mke wangu alikuwa
akiongea na wageni, sikutaka kumtoa kwenye mazungumzo lakini nilipoingia
chumbani kujiandaa kwenda kazini, mke wangu naye aliingia na swali lake la
kwanza likawa,
"Mbona hivyo mume wangu? Tumekwenda wote
hospitali lakini kurudi ukatukimbia. Kweli yani shemeji yeye ndiyo wa
kunirudisha..."
Alishindwa kuendelea baada ya uchungu kumjaa na
kumfanya atoe chozi. Huruma iliniingia ghafla na hasa sikutaka wageni wahisi
kama kuna kitu hakipo sawa. Hivyo nikakaa pembeni yake kitandani na kumkumbatia
nikimwambia,
"Samahani mke wangu, sikupenda kufanya hivyo na
nashindwa kuelewa kwa nini niliwahi kuondoka hospitali. Tafadhali naomba
usinifikirie vibaya kabisa. Nakupenda sana mke wangu na sasa tumeanzisha
familia yenye watoto, naomba tuwe watu wa furaha kwa yote yale Mungu
anayotujalia."
Mke wangu aliniangalia shingo upande huku akitia
huruma. Nikiwa na hofu kama ameweza kugundua uwongo ndani yangu, nikaamua
kumuaga,
"Mke wangu, acha mimi niende kazini sasa.
Hongera kwa kujifungua salama, naomba uniangalizie mtoto wangu."
Kabla ya kuanza kuondoka nikambusu kwenye paji la
uso na ndipo taratibu nikauelekea mlango huku moyoni nikijalaumu kwa uwongo
wote niliousema kwake na kisha kwenda kazini.
Siku iliendelea kwa namna hiyo, kazini nikipokea
hongera nyingi kutoka kwa wenzangu na simu nyingi za pongezi kutoka kwa watu
mbalimbali ambapo kila pongezi niliyokuwa nikiipokea, moyoni nilikuwa
nikijiuliza watu hao wangesemaje endapo wangeelewa yaliyotokea. Maswali hayo
yalinitia hasira kwani niliamini watu hao wangeniona mimi mjinga na si kunionea
huruma endapo wangeujua ukweli.
Usiku ulipofika nikiwa chumbani na mke wangu tayari
kwa kulala, ndipo mke wangu akaanzisha tena mazungumzo juu ya yule mtoto.
"Mume wangu, hatukupata muda wa kuzungumza
kuhusu mtoto wetu. Niambie umemuonaje?"
Nilitamani niuone uso wa mke wangu vizuri jinsi
anavyoongea lakini kwa vile taa zilikuwa zimezimwa, giza likaninyima uwezo huo.
Nikiwa bado njia panda kama huo ndiyo ulikuwa muda muafaka wa kumuelezea mke
wangu wasiwasi wangu au la, nikatoa jibu lisilofungamana na upande wowote.
" Nashukuru tu Mungu mke wangu umenizalia
kidume atakayeweza kuendeleza jina langu. Ni mtoto mzuri tu ambaye hatuna budi
kumpokea kwa mikono minne, mi miwili na wewe miwili. Wewe umemuonaje?"
"Mimi nimemuona tofauti mume wangu.”
[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia
simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]
No comments:
Post a Comment