Katika nakala iliyopita
katika mfululizo wa nakala hizi, nilizungumzia umuhimu wa kujua kuchekesha bila
ya kukariri vichekesho. Lakini, inanipasa kuelezea namna ya kutumia vichekesho
katika kuchekesha kwani ndiyo mwanzo wa kujijengea uwezo wa kuchekesha bila
kufikiria. Kabla sijaanza kuelezea namna ya kutumia vichekesho ili kuchekesha,
nikumbushe kuwa vichekesho kama mpangilio wa maneno pekee, vina mchango mdogo
sana katika kuchekesha.
Kama umewahi kuona watu
wakielezea jambo na kujikuta wakicheka wenyewe bila ya kukufanya wewe ucheke,
jua watu hao walishindwa kuvitumia vichekesho hivyo kuchekesha. Pia, wapo
wanaokujulisha kuwa wanatoa vichekesho ili kuchekesha lakini hata wanapomaliza
kuelezea vichekesho hivyo, msikilizaji unashindwa kuona kitu cha kuchekesha.
Sina shaka kwamba kila mtu ameshatokewa na hilo. Baadhi hujaribu kuelezea zaidi
vichekesho vyao pale wanapomaliza na kushindwa kuchekesha lakini hata kwa maelezo
ya mara ya pili, bado wapo ambao hufeli kutumia vichekesho hivyo kuchekesha.
Kitu cha kwanza kabisa
cha kuzingatia, ni kujua nini hasa ndiyo chanzo cha maelezo fulani kuwa vichekesho.
Lazima ujue nini kilichokufanya wewe uelewe kuwa maelezo fulani ni vichekesho
na mengine si vichekesho. Pia kama nilivyoelezea katika nakala zilizopita
katika mfululizo huu, lazima ujue ni hatua ipi kati ya zile hatua kuu tatu za
kufanya mtu acheke ndipo vichekesho hivyo utakavyotumia vitamhakikishia mtu
kuwa ni vichekesho.
Chanzo cha kuchekesha
kwa vichekesho, mara nyingi huwa ni mhusika ndani ya kichekesho kuelewa tofauti
jambo fulani mfano katika kichekesho kimoja, mteja wa kiume kufurahia kusikia
atapewa kampani na sekretari wakati bosi akifanya shughuli nyingine lakini
sekretari kumbe ni wa kiume na si wa kike au kichekesho kingine ni mchina
kupewa jukumu la ‘supplies’ yaani mahitaji na badala yake yeye kuelewa kuwa
jukumu lake ni kufanya ‘surprise’ yaani jambo zuri lisilotarajiwa..
Pia katika kutambua
hatua gani hasa ndiyo mihimili ya vichekesho, mara nyingi huwa ni katika ule
muda ambao mchekeshwaji anahusisha matokeo ya vichekesho yaani mwisho wa vichekesho
na ile picha au mwisho ambao yeye aliutabiri, ni vema kuhakikisha kuwa
usimuliaji wako wa vichekesho, hauingilii hatua hiyo kwa kujaribu kuchekesha
kabla ya hiyo hatua.
Kwa kutambua chanzo, ni
lazima umuwezeshe mlengwa kubaini chanzo kama ulivyoona wewe msimuliaji. Yaani
kwa mifano ya hapo juu, lazima uhakikishe mlengwa anatambua kuwa kuna ‘supplies’
na ‘surprise’ zenye matamshi yanayoendana lakini maana tofauti na kama kuna
sekretari wa kike na wa kiume kabla ya kufika kwa hatua uliyobaini kuwa ndipo
kuchekesha kutatokea.
Wanachokosea wengi ni
kudhani mlengwa ana uelewa kama aliokuwa nao yeye anayetoa vichekesho. Pia
mazingira yanapokuwa tofauti, labda vichekesho wewe ulivisoma lakini sasa
unasimulia, au wewe ulihusika katika vichekesho lakini sasa unamuelezea mtu ambaye
atakuwa msikilizaji tu, na namna nyingine nyingi. Hivyo jambo kuu au mzizi wa
yote ni kujiuliza mara mbili mbili, je mazingira na uelewa uliokuwa nao wakati
ukivipata vichekesho hivyo, ndiyo mazingira na uelewa uliopo wakati unavitoa
vichekesho hivyo? Mambo hayo yanapoendana, nina imani kuwa vichekesho vyako
vitafanya kazi yake ya kuchekesha.
Katika nakala
inayofuata katika mfululizo wa nakala hizi tutaangalia mambo ya kuepuka wakati
wa kutoa vichekesho… mifano iliyoelezewa hapo juu imetolewa kwa kirefu katika
facebook group, www.facebook.com/copykennytz
No comments:
Post a Comment