Wednesday, September 30, 2015

Damu Ya Ukoo Wangu: Sehemu ya 6



" Nashukuru tu Mungu mke wangu umenizalia kidume atakayeweza kuendeleza jina langu. Ni mtoto mzuri tu ambaye hatuna budi kumpokea kwa mikono minne, mi miwili na wewe miwili. Wewe umemuonaje?"
"Mimi nimemuona tofauti mume wangu."
Alisimama akisubiri nimuulize kwa nini jambo ambalo sikuligundua mapema na hivyo muda kupita kabla ya kumuuliza kwa nini na ndipo akanijibu,
"Samahani sana mume wangu nimekuzalia mtoto mlemavu. Inaniuma sana kushindwa kukuzalia mtoto kamilifu kama ulivyokuwa ukisubiria miaka yote tangu tulipooana."
"Mke wangu,.."
Niliita nikitaka kumkatisha kwani niliona si busara kumfanya ajione mwenye makosa mbele ya mipango ya Mungu. Tatizo langu lingejitokeza mbele nami nilikuwa nikiamini lenyewe haikuwa mipango ya Mungu bali ni shetani aliyelileta. Mke wangu baada ya kuona nataka kumkatisha, ndipo sauti yake ikaongezeka uchungu na kuendelea,
"Mume wangu najua jambo hilo limekuvunja sana moyo lakini tafadhali nipo chini ya miguu yako, naomba usimchukie mwanangu kwa kuwa ni kilema, mimi unaweza kunichukia lakini mwanangu hana makosa."
Hapo niligeuka na kulala kiubavu nikimtazama mke wangu kwa huruma. Nikaunyoosha mkono wangu kushika nywele zake nikizishika taratibu na kwa kujiamini nikamwambia,
"Siwezi kumchukia kwa vile ni kilema mke wangu, nakuhakikishia hilo. Wewe ondoa shaka kabisa kwenye jambo hilo."
"Ahsante mume wangu."
Sikusema kitu baada ya shukrani yake nami nikawa nikiwaza jinsi gani mke wangu alikuwa akijaribu kunifanya nimpende mtoto yule ambapo kiukweli nilishapoteza hamu ya kumpenda nikijua hakuwa mwanangu. Nililala tena chali na kuacha kumshika nywele. Baada ya kama dakika tano kupita bila ya kusemekana neno, mke wangu akaita,
"Mume wangu"
"Naam mke wangu"
Niliitika huku nikigeukia tena upande wake. Naye akaweka mkono wake shavuni kwangu na kuuliza,
"Mume wangu hivi kipi kilikukasirisha kule hospitali hadi ukaondoka?"
"Kwa nini unauliza mke wangu, sikukasirika kitu."
"Usinifiche mume wangu. Unajua namna ninavyokupenda mpenzi, nisingependa kukufanya ukasirike hata mara moja mume wangu. Niambie tu kama ni kwa sababu ya ukilema sema tu, mimi mbona ni muelewa."
"Aahsh"
Nilitoa pumzi kwanza kama vile mtu aliyeshangazwa na kuchoshwa sana na kisha nikamuambia,
"Mke wangu naomba uachane na hayo. Cha msingi ni kwamba sina hasira tena na haikuwa kwa vile mtoto ni kilema kwani kama ni ukilema basi bado ningekuwa na hasira maana ukilema haujatoka lakini ona ninavyofurahi mke wangu."
"Huniamini mume wangu. Hudhani kama naweza kukabiliana na kueleza ukweli ndiyo maana unanikwepa na kujaribu kupata ukweli kwa njia zingine."
"Ukweli upi?"
Nilishajua alichokuwa akiongelea ila kwa vile niliona ameanzisha mwenyewe, hivyo ni bora angemaliza mwenyewe.
"Najua unajiuliza kama kweli huyu mtoto ni wako au wa shemeji kwa vile amefanana zaidi na shemeji kuliko wewe."
"Si mimi tu, kila mtu atakayemuona atajiuliza hivyo hivyo kasoro nyie wawili tu."
"Shemeji hahusiki kabisa na mtoto huyu mume wangu, naomba uniamini. Nimekuwa mwaminifu kwako siku zote na hakuna mahusiano yoyote kati yangu na shemeji. Namuheshimu naye ananiheshimu sana. Huyu ni mtoto wetu mume wangu."
"Usijaribu kunishawishi mke wangu, kama ni kweli nitajua tu. Nisiijue damu yangu?"
"Haya usiku mwema lakini kumbuka huyu ni mwanao."
Nikiwa nimelala usiku wa manane, nilijigeuza mwili wangu nami nikahisi mkono wangu ukitua juu ya kitu fulani kigumu ambacho hakikuwa cha kawaida. Ubaridi nilioupata ulifanya macho yangu yafunguke ghafla na kuona vivuli viwili vya watu wakiwa wanamvuta mwanangu huku mke wangu akijitahidi kumzuia mtoto na kuniita kwa kelele. Kuitwa huko nilihisi tu kutokana na namna mke wangu alivyokuwa akitanua mdomo lakini haikutoka sauti yoyote. Watu hao tayari walishafika karibu na mlango wa chumbani naye mke wangu akiwa kama hatua mbili kutoka kitandani.
Niliamka kwa haraka lakini kabla sijafanikiwa kusimama, nikahisi mkono wangu ukivutwa kunizuia nisiende kumsaidia mke wangu. Niligeuka kwa hasira kuangalia nani aliyekuwa akinishika. Hapakuwa na mtu na si kwa sababu ya kuwa na giza bali kweli hapakuwa na mtu kwa maana hata kuona kivuli chake haikuwezekana.
Niliogopa sana na kujaribu kuuvuta mkono wangu kuhakikisha kama kweli nilikuwa nimevutwa na mtu asiyeonekana au ni mawazo yangu tu. Nilijaribu kuuvuta mkono wangu nami nikagundua kuwa kweli ulikuwa umeshikiliwa na mkono wa huyo mtu asiyeonekana, mikono iiyokomaa na ya baridi kama imewekwa kwenye jokofu. Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kwani mke wangu alionekana kushindwa kuwazuia wale watu naye alikuwa akinitegemea mimi. Kwa namna alivyokuwa akiniangalia, alionesha kutokufurahishwa na kitendo cha mimi kutokwenda akishindwa kujua nilikuwa nimezuiliwa. Nilianza kuhisi moyo ukiniuma kwa hofu kuwa mke wangu angedhani nimefanya makusudi.
Ghafla nikasikia sauti ikininong'oneza,
"Usiende kumsaidia mkeo. Mnajitilia mikosi na huyo mtoto, siyo halali yenu huyo. Waachieni waende naye."

[Nini kitafuata..? Endelea kufuatilia simulizi hili. Pia nakala zipo tayari madukani.]

No comments:

Post a Comment

  • Hadithi na Simulizi