Sunday, September 13, 2015

Roho ya Kayumbas: Sehemu ya 7



Mwaka 2007

Siku ya kufunguliwa shule inapofika, Kayumbas na Jennifer wanaamka mnamo saa kumi na mbili kasorobo kama mwaka uliopita  na kwenda kuchota ndoo tatu za maji kila mmoja. Kisha wanajiandaa na shule na inapofika saa kumi na mbili na nusu wanamuamsha Mjanja ambaye tofauti na siku zingine ambazo alikuwa akichukua muda mrefu kuamka anapoamshwa, siku hiyo ananyanyuka kitandani baada ya kuitwa mara moja tu. Anamuamkia Kayumbas ambaye ndiye amemuamsha na kujiandaa haraka haraka akiwa na hamu isiyoelezeka ya kuanza shule.
Ifikapo saa moja kasorobo watoto wote wanakuwa tayari na wanamuaga mama yao kwenda shule. Mama Kayumbas anaishia kumuangalia mwanaye Mjanja anavyotembea huku akichomekea chomekea sare zake za shule za rangi ya bluu na begi lake dogo likiwa mgongoni. Mama Kayumbas anajichekea mwenyewe kwa kuona mwanaye akiwa na hamu hiyo kubwa ya kusoma na kutumaini kwamba atafika mbali kwenye masomo.
Kayumbas naye anafarijika kuanza mwaka huu kwani safari zake kati ya nyumbani na shule sasa hazitakuwa za umbali mrefu kama zamani kwa kuwa Majaliwa ameshahamia shule yao baada ya kuanza darasa la kwanza. Pia shule ya awali ya Mjanja haipo mbali na nyumbani kwao. Hivyo anauanza mwaka akiwa na matumaini zaidi hasa anapoona anakaribia kumaliza elimu yake ya msingi mwaka mmoja baadae.
Faraja hiyo ya Kayumbas inaendelea hata anapofika shule na kuungana na wanafunzi wengine kufanya usafi wa shule ikiwa ni kufagia madarasa na uwanja pamoja na kumwagia maji bustani za shule. Usafi unamalizika majira ya saa mbili asubuhi na kisha wanakwenda kwenye gwaride ambapo wanakaribishwa tena shule, wanatambulishwa walimu wapya wawili na kisha kuelekezwa madarasa watakayokuwa wakiyatumia.
Wanapotoka gwaride, wanafunzi wanaingia kwenye madarasa waliyoelekezwa na kuanza kugombaniana nafasi za kukaa na kuhamisha madawati kutoka madarasa yaliyokuwa na madawati ya ziada kwenda kwenye madarasa yenye upungufu wa madawati wakisimamiwa na walimu wao. Bado shule ina upungufu wa madawati na wanafunzi kulazimika kubanana hadi wanafunzi sita kwenye dawati la wanafunzi wanne.
Mpaka inapofika mida ya saa nne kamili wanafunzi wanakuwa wametulia kwenye madarasa yao na walimu wa madarasa ya la tano hadi la saba kuwapa wanafunzi wanaowaamini na wenye miandiko mizuri kuandika majina ya wanafunzi wote wa darasa husika kwenye daftari la mahudhurio. Wanafunzi wanajipanga kwenye mistari wakifuatisha mpangilio wa herufi za mwanzo za majina yao na kujiandikisha majina yao kwenye madaftari hayo, zoezi linalochukua kama nusu saa kumalizika.

"Mmh, Shoga! Huyu wewe au kopi yako?" Msichana mmoja kwenye dawati la mbele ya lile alilokaa Kayumbas anamuuliza mwenzake wakati akiiangalia picha ya rafiki yake huyo.
"Mimii huyoo. Yani siku hiyo ukumbini kila mtu alikuwa akitamani kunichombeza."
"Mmh, toka hukoo. Unapenda kujisifia sana shoga yangu. Yaani watu wasimuangalie..."
"Haa! Sasa unabisha?" Anatoa picha zingine na kumpa huku akimwambia,
"Haya hebu angalia mwenyewe picha hizo halafu uniambie kama kuna kasoro."
Wakati wale wasichana wakiendelea kusifiana, kwenye dawati alilokaa Kayumbas wenzake wawili wanakuwa wanaulizana,
"Halafu kamanda sijakuona kabisa likizo hii, siyo kawaida yako. Ulijichimbia wapi kamanda?"
"Aaah, Tanga hiyo mzee."
"Duuh, na wewe mshikaji umefikia kwenda Tanga? Kweli dunia imeisha. Nani huyo ulienda kumpiga ndumba?(kumroga)"
"Ndumba wapii? Mabinti wa Kitangaa, ooh, wanajua kujipamba, ooh, kwa mapozi wanatambaa, kwa mapenzi mi nitawafuata Tangaa"
"Mmh, wimbo nishausahau huo wewe bado unaukumbuka tu?"
Kabla ya kumjibu mwenzake anakatishwa na Kayumbas anayemstua na kumuuliza,
"Oya, twisheni ilikuwaje likizo?"
"Thafi tu mshikaji."
"Oya nilishakuambia utani huo thipendi."
"Utani ufanyaje?"
Yule mwenzao wa pembeni naye anaingilia kwa kumuonya mwenzake,
"Kamanda acha kumzingua Kayumbas bwana."
"Hamna uthinimaindi wala nini Kayumbas, mimi nakutania tu kwa kuwa wewe mshikaji wangu yani. Yani nakufili ile kinyama, wewe hujui tu."
"Poa yaishe, niazime madaftari yako ya twisheni."
"Sasa hapa thina mshikaji, nitakuletea kesho."
"Wewe endelea tu, thiku utashangaa nakuthemea kwa mwalimu."
Kayumbas anaachana nao na wao kuendelea kupigiana hadithi za Tanga na za yaliyotokea kipindi cha twisheni na zamu ya kufanya usafi shuleni.
Dakika kumi na tatu kabla ya kufika saa saba kamili ambao ndio muda wa masomo kuisha, anaingia mwalimu mmoja ambaye ni maarufu miongoni mwa wanafunzi hata kwa wale ambao hajawahi kuwafundisha. Ni mwalimu mwenye urefu wa wastani, mnene kidogo na umri kati ya miaka thelathini hadi arobaini. Kinachompa umaarufu shuleni ni vitu viwili, ukali na mavazi yake japokuwa tabia yake ya kuvaa sketi fupi ndiyo hasa iliyowafanya wanafunzi kutaka kumjua pale tu wamuonapo mara ya kwanza.
"Moja... mbili... tatu." Anasema kiranja wa darasa mara mwalimu huyo anapoingia darasani na wanafunzi wote wanasimama na kusema kwa pamoja,
"Elimuu ni msingii wa maiisha. Shikaamoo mwaaalim."
"Marahaba, hamjambo?"
"Hatujamboo mwaalim."
Mwalimu huyo anapita mpaka mbele ya darasa na kuandika tarehe ya siku hiyo ubaoni na kuchora mstari wa pambizo kabla ya kuwageukia wanafunzi na kuwaambia,
"Haya kaeni chini. Mimi ndiye nitakayekuwa nikiwafundisha somo la Maarifa ya Jamii na huwa sipendelei kusumbuana na wanafunzi. Si mmeshasikia habari zangu kutoka kwa kaka na dada zenu?"
"Ndiyoo."
Mara minong'ono inaanza kwa baadhi ya wanafunzi wakiwaelezea wenzao yale waliyoyasikia kuhusu mwalimu huyo na bila ya kupoteza hata sekunde mwalimu anaikemea,
"Nadhani hamjanijua nyie. Nikiwa darasani sitaki kusikia minong'ono ya aina yoyote ile. Siyo kuongea, mnielewe vizuri hapo, hata ile minong'ono siitaki. Nina aleji na kelele."
"Hahaha" Baadhi ya wanafunzi wanacheka na mwalimu anaendelea,
"Haya, nimeuliza kama mmesikia kuhusu mimi mkasema ndiyo, sasa kama hulijui jina langu wewe mwenyewe simama juu."
Wanasimama wanafunzi wanaokaribia ishirini kati ya wanafunzi wote tisini na mbili wa darasa hilo ukiwa ndiyo mkondo wenye wanafunzi wachache kuliko mikondo yote minne ya darasa la sita. Anawatazama wanafunzi hao kama vile akiwashangaa na kumwambia mwanafunzi mmoja aliyekuwa amesimama kutoka dawati la mbele,
"Hebu nenda pale ofisi ya walimu uulizie meza ya Madam" Anavuta sekunde kadhaa bila ya kusema neno na kuwageukia wanafunzi wengine waliokaa na kuwauliza, "Madam nani kwa nyie mnaonijua?"
"Madam Pendeeekiiii." Wanafunzi wachache wanajibu kwa sauti ya juu, wakijivunia kumjua mwalimu huyo kwa wale wasiomjua.
"Umesikia? Ulizia meza ya Madam Pendeki, kuna mwanzi wangu juu ya meza uniletee nipate wa kuwasimulia wenzao. Si huwa mnalinganisha fimbo za walimu kujua zipi zinauma sana, na mimi nataka mnilinganishe sasa."
Wanafunzi waliosimama kwa waliokaa wanaanza kutahamaki na kumuogopa mwalimu huyo.

[Endelea kufuatilia simulizi hili litokanalo na matukio ya kweli...]

No comments:

Post a Comment

  • Hadithi na Simulizi