Watu wengi katika taifa
hili wamejiwekea mazoea hasi kwa jinsi yao ya kupokea pole. Wengine wamekwenda
mbali zaidi kiasi cha kwamba kudhania kuwa wakiwa na matatizo, mtu wa karibu
yao ni lazima atoe pole. Yaani wanachukulia kuambiwa pole ni haki yao na hivyo
kukosa ustaarabu wa kuonesha kuheshimu huruma ya mtu atoaye pole.
Ukimuuliza mtu yoyote,
ukiambiwa pole utajibu nini? Jibu lake bila shaka litakuwa ni ‘asante’. Jambo
la kujiuliza ni kwamba, unaposema ‘asante’ baada ya kuambiwa pole, una uhakika
ina utofauti na ile ya mtu akikuambia ‘hongera’? Katika hatua za kuboresha
lugha yako ya kistaarabu, hasa kwa jinsi ya kuipokea pole, huo ndiyo mwanzo.
Yaani hakikisha namna unavyoipokea pole kwa kusema ‘asante’ iwe tofauti na kama
mtu angekuambia ‘hongera’ baada ya kufanikiwa jambo.
Katika kuimarika kwa
lugha yako kwa jinsi ya kuipokea pole, basi ni vema uzingatie taratibu zile za
kutoa pole katika nakala hizi. Yaani usitoe ‘asante’ tupu. Jambo unaloweza
kuzingatia ili kufanikisha jitihada za kutotoa ‘asante’ tupu ni kugundua kuwa
mpaka mtu anakuambia pole, basi ameguswa kwa namna fulani na matatizo yako.
Asante yako ni vema ukailenga kwa namna mtu alivyoguswa na matatizo yako. Faida
za kufanya hivi ni kumfanya mtu aliyetoa pole kuona kuwa umethamini mchango
wake au hisia zake katika matatizo yako na kukufikiria kama mtu atayeweza
kuthamini na kusaidia katika matatizo yake.
Katika hatua za mwanzo
za kutotoa ‘asante’ tupu, unaweza kujifunza kutumia maneno, ‘asante au
nashukuru kwa kuguswa.’ Hapo unamfanya mtu atoaye pole aamini kuwa hakufanya
vile kana kwamba ni desturi bali moyo wake umekuwa wa kikarimu na kuweza
kugundua au kuguswa na matatizo yako. Yaani si watu wote watakaotoa pole kwako,
bali wachache kama yeye.
Zaidi ya kauli hiyo,
‘asante au nashukuru kwa kuguswa’, katika jinsi ya kuipokea pole unaweza
kuivalisha ‘asante’ yako mavazi mazuri zaidi au ya kiufalme. Hapo ndipo
unapoweza kupeleka mahusiano(urafiki) katika hatua nyingine au kufufua au
kuimarisha uhusiano au urafiki. Hatua hii ya kuvalisha mavazi, si ya
kuikimbilia kwa haraka kwani unapokosea, inaweza kuleta picha tofauti zaidi. Katika
hatua za mwanzo, unaweza kutumia kauli zinazoendana na namna hii, ‘Nashukuru
kwa kunifariji. Kiukweli unaelezea hali
mbaya uliyokuwa nayo mwanzo na kisha kuelezea hali mpya iliyo bora baada ya
kupokea pole’ au kauli ndogo kama ‘sikudhania kama jambo hili lingekugusa.
Lakini nashukuru kwamba na wewe umeona jinsi gani linavyonisumbua…’
Nimalizie na kuvisha
mavazi ya kiufalme ‘pole’ itokayo kwa mtu unayemjali sana, au mtu aliyetoa
‘pole’ ambayo maneno yake yalifanya usahau shida uliyo nayo, kwa jinsi hii ya
kuipokea ‘pole’, ni vema kuitumia mara chache iwezekanavyo. Jinsi hii inakuwa
na maelezo mengi ambayo yanazungumzia sifa za ujumla, labda baada ya mtu
kuguswa mara nyingi na matatizo yako au kuonesha msaada mkubwa katika matatizo
yako. Maelezo haya nahisi yashatumiwa mara nyingi na hivyo swala la
kuyaainisha. Unaweza kusema kitu kinachoendana na ‘Nashukuru kwa kuguswa, tena
nashukuru sana. Yaani katika watu wangu wa karibu, wewe…’
La kuzingatia: Hata uwe
na matatizo kiasi gani, kupewa pole si haki yako. Hivyo ukipewa ‘pole’,
shukuru. Ukiwa unapokea pole, jitahidi kujua nini kimemgusa mtu huyo hata kutoa
pole na shukuru kufuatia kuguswa huko. Mfano katika msiba, mtu anaweza kuguswa
kwa namna kifo kilivyotokea, au familia anayoiacha marehemu, au maisha
aliyoishia marehemu(labda muda mfupi) n.k. lakini kwa namna yoyote ile,
wataunganishwa na neon ‘pole’. Kazi yako ni kugundua kipi kimemgusa hasa.
‘Pole’ ya kipekee ni vema ikapokea shukrani ya kipekee, na ni vema kukumbuka
‘pole’ siyo ‘mchango wa kutatua matatizo’ ni kuguswa na kutoa kauli za
kufariji.
Katika nakala ijayo
katika mfululizo wa nakala hizi, jinsi ya kuomba radhi.
No comments:
Post a Comment