Muda wa kurudi nyumbani
pia unapofika, Kayumbas inabidi ashuke vituo viwili kabla ya kufika kituo cha
nyumbani kwao kwa ajili ya kumpitia Majaliwa na ndipo arudi naye nyumbani.
Wanapofika nyumbani
siku hiyo, mama yake anamsimamisha Kayumbas asile kwanza akamtafute mdogo wake
wa mwisho, Mjanja kwani tangu saa nne asubuhi ya siku hiyo hakuonekana nyumbani.
Kayumbas anabadili nguo
zake kwa haraka na kwenda kwa majirani kuanza kumuulizia mdogo wake. Anazunguka
kwenye nyumba mbili tatu alizozipa nafasi kubwa ya mdogo wake kuwepo humo na
kwenye nyumba ya tatu anamkuta akiwa amekaa na baadhi ya watoto wengine
wakiangalia filamu ya ngumi iliyotafasiriwa kwa kiswahili.
Kayumbas anamuita mdogo
wake huyo na kwenda naye moja kwa moja nyumbani bila ya kumlaumu chochote
lakini anapofika nyumbani, anakaribishwa na swali la tahamaki kubwa kutoka kwa
mama yake.
"Wee! Umemkuta
wapi?"
"Alikuwa kwa akina
Kuruthumu." Kayumbas anahisi mikono ya mdogo wake ikianza kutetemeka na kuiachia
kabla ya mama yake kumuuliza swali lingine.
"Alikuwa
anaangalia video, si ndiyo?"
"Nilimkuta
anacheza na wenzake thebuleni." Kayumbas anajaribu kumtetea mdogo wake.
"Wewe, ulikuwa
unaangalia video eh?" Mama Kayumbas anamfuata Mjanja huku akiwa ameshika
fimbo mkononi na kumuuliza kwa ukali.
"Mmm mmm mm."
Mjanja anatingisha kichwa kukataa huku machozi yakimlengalenga.
"Wewe ulikuwa
unaangalia picha la Van Dame si ndiyo?"
"Aa aa,
sijaangalia kitu mimi unanionea." Anajaribu kukataa na mama yake
anamuuliza tena,
"Niambie
umeangalia picha gani?"
"Siijui."
"Manachulye
litondo." Anasema mama Kayumbas kwa hasira na akipunguza ukali wa sauti
yake anasema, "Nilijua tu, na wewe Kayumbas unajaribu kunidanganya.
Utampoteza mdogo wako kwa ajili ya huruma yako hiyo."
Anamshika Mjanja tayari
kwa kumchapa kwenye makalio na kumuuliza kwanza,
"Wewe nilikuambiaje
kuhusu kuangalia video kwa watu?"
"Nisamehe mamaaa.
Nilisahau leo, Juma aliniambia tucheze."
"Wewe kila siku
unajidai huelewi eeh. Huko shule utasoma nini kama huelewi kitu?"
Anamchapa na Mjanja
kulia kwa kelele kubwa ambazo zinasimamishwa na kukemewa kutoka kwa mamaye
akitakwa aache kelele. Baada ya kuridhika na adhabu hiyo, mama Kayumbas anasema
"Na akirudi baba
yako nitakusemea. Kama hawezi kuwanunulia tivii ajue namna ya kuwakataza kwenda
kukodolea macho za watu."
Baadaye Kayumbas
anamueleza mama yake kuhusu kuhitajika kwa shilingi mia mbili kila siku kwa
ajili ya masomo ya ziada maarufu kama twisheni kwani walimu wamewaambia kuwa
darasa la tano mpaka la saba linahitaji twisheni.
"Sawa mana oko
nimekusikia, tutakupa hiyo hela."
Anajibu kwa mkato
lakini moyoni anaanza kuwaza kama watakuwa na uwezo huo wa kutoa karibu mia
nane kila siku kwa ajili ya shule. Hofu inazidi kumuingia kwamba muda utafika
hela hiyo itaongezeka kwani Jennifer naye atahitajika hela ya twisheni pindi akifika
darasa la tano na pia muda Mjanja atakapoanza chekechea na Majaliwa kuanza la
kwanza.
Mawazo hayo yanamuondoa
umakini wake kwenye mambo yanayokuwa yakitokea muda huo na kuamua kwenda
chumbani kwake kupumzika kwa muda mpaka akili yake itulie. Akili hiyo inatulia
baada ya kutumaini kushauriana na mumewe mambo hayo muda ambao mumewe atarudi
kutoka kazini siku hiyo.
Mama Kayumbas anasubiri
sana siku hiyo hata inatimu saa tano kasorobo ndipo anaposikia hodi mlangoni
kwao. Muda huo watoto wote wanakuwa tayari wakikoroma na anapofungua mlango,
kabla hata ya salamu kauli yake ya kwanza inakuwa,
"Mbona umechelewa
hivi baba Kayu, imekuwaje huko?"
"Ka...ka..kazi leo
iii...ilikuwa ngumu mmma Ka. Tuu..tulikamatwa na...na...na trafiki mmm..mara
mbili kwa hiiiyo ii..iii...ikabidi tu...tu...tuongeze ruti ku...ku...kufidia."
"Pole mume wangu,
maisha tu hayo. Afu mwanao Kayumbas anahitaji mia mbili ya twisheni kila
siku."
"Sasa mm..mmke
wangu iii...i..ina ma..ma..maana hilo na...lo uu..uu..unahitaji kuniambia mmimi?
Uuu..uuu..we si uuu..mpe tu? Eee? Mm..mi naacha chote nii..nii..patacho mbona?."
"Siyo hivyo baba
Kayu, nilikuwa nakuambia tu mume wangu ili ukae ukijua hivyo."
"Sawa, tu..tu..tushirikiane
kuu..kuu..hakikisha watoto wetu wa...wa..wana..wana..pata elimu nzuri. Mmm..mmi
sijui ni..ni..nitajisss..sikiaje kuu..kuupandisha wa..watoto wa watu kwee..nye
gari yangu saa nyiii...ngine bu..bu..bure kabisa ili..ili..ili wakasome haa..ha..halafu
waa..wa..wanangu wenyewe sss...siyo wanafunzi."
"Watoto wetu
watasoma tu mume wangu, acha sisi tufanye tuwezalo na Iruwa ataweka mkono wake."
Baba Kayumbas
anamtazama machoni mama Kayumbas baada ya kusema kauli hiyo na mama Kayumbas
anapoona akiangaliwa hivyo, anatabasamu kidogo huku akimpiga kidogo begani baba
Kayumbas na kumuambia,
"Na wewee! Haya
Mungu ataweka mkono wake."
"Amina." Baba
Kayumbas anajibu kwa sauti na kwa haraka.
"Hivi, baba Kayu
kwa nini siku hizi hutaki kabisa kunisikia nikiongea maneno ya Kichaga?"
"Uuuu..uunawafanya
wa..waa.watoto nnnao waanze ku..ku..kusema maneno ya Kichaga."
"Kwani kuna ubaya
gani baba Kayu?"
"Baba yao
si...ssssisiyo mmm..mmchaga."
"Basi wafundishe
kikwenu."
"Mmmi
ssississi..kijui nnnna haina mmmmaana."
"Mmh ya kushindwa
hayo. Tuachane na hayo, swala lingine mume wangu ujue ni nini?"
"Enhee nii...ambie!"
"Hebu jitahidi
basi mwezi huu uwanunulie wanao tivii na wao waangalie. Ujue watakuwa watumwa
kwa ajili ya kuangalia video kwa watu?"
"Ha..haa..pana mke
wangu, ti..tii..tivii siyo mu..mu..mu..himu sss...saaana kwa sasa. Waa..waa..wangapi
ha..haawana tivii hadi leo? Aa..aangalau uuu..uu..ungeniambia tuujipange ku..ku..kukutafuta
ki..ki..kiwanja chetu tuu..tu..kajenga ki..banda kidogo... Mmmi nadhani.."
"Mume wanguu, au
kwa vile wewe hushindi hapa nyumbani ndiyo maana huoni karaha yake? Kila muda Mjanja
yupo kwa watu anaangalia mapicha, kama mzazi napenda kumuona mwanangu akifurahi
kukaa hapa nyumbani siyo kila dakika huyo, churupu kwa watu."
"Bado mmmdogo huyo
mmmke wangu, aa..aaa...atakuja kuacha sss..siiku moja. Mmm..mbona wee..weenzake
hawa..hawaafanyi hivyo?"
"Siyo kwamba
hawapendi, inawauma kukaa hivyo lakini ndiyo wafanyaje na mimi nimewakataza?
Tuwanunulie tivii bwana mbona hazina hata bei sana? Kama kuhama tutahama nazo
tu."
"Sssaawa mm..mke
wangu, ng'..ngoja nianze ku..kuuu..weka hiyo hela basi.”
[Endelea kufuatilia simulizi hili litokanalo na matukio ya kweli...]
unapost lin tena?
ReplyDelete